Habari

Waziri Ndalichako aelekeza ukaguzi maalum matumizi fedha za Uviko-19 ukarabati wa chuo cha watu wenye ulemavu Yombo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Prof. Joyce Ndalichako ameelekeza kufanyika kwa Ukaguzi Maalum juu ya matumizi ya kiasi cha fedha shilingi milioni 694.

Fedha zimetumika kwa ajili ya Mradi wa ukarabati wa chuo cha Marekebisho na Ufundi Stadi Yombo kwa Watu Wenye Ulemavu, jijini Dar es salaam kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Mhe. Waziri Ndalichako ametoa maelekezo hayo Leo tarehe 1 Agosti, 2022 baada ya kufanya Ukaguzi wa ukarabati wa chuo hicho na kuonesha kutoridhishwa na gharama zilizotumika kununua vifaa pamoja na ubora wa vifaa vilivyotumika katika ukarabati huo.

“Bei hizi sio za uhalisia kabisa, kuweka Wire mesh kwenye dirisha moja shilingi laki Tano, gharama hiyo ni sawa na gharama ya kutengeneza dirisha kamili jipya”

Mhe. Ndalichako amesisitiza yapo mapungufu makubwa ambayo ameyabaini ikiwemo kutozingatiwa kwa makadirio ya Ujenzi (BOQ), hali iliyosababisha kiasi cha fedha zilizotengwa kuisha ikiwa bado ukarabati wa ujenzi wa chuo hicho haujakamilika.

Mhe. Ndalichako amefafanua kuwa ukokotoaji wa gharama hauna uhalisia kwa mujibu wa taratibu za kutumia “Force account”.

“Kila item inayonunuliwa imewekewa labour charge 30/%, na Contingency ya 15%, na 10% ya supervison, Sasa kwa ununuzi wa extension cable, labor charge na supervision ya nini?”

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe.Ngw’ilabuzu Ndatwa Ludigija, amesisitiza kuwa ataendelea kufuatilia mradi huo ili gharama zake ziendane na thamani ya fedha zilizotengwa.

Fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, katika chuo hicho zinahusika katika ujenzi wa; Majengo ya Mabweni 2, Jengo la Darasa la Kilimo, Majengo 2 ya Nyumba za Watumishi, Jengo la Zahanati, Kituo Cha Kutwa kulelea Watoto na Karakana ya Umeme.

Related Articles

Back to top button