Habari

YST yachangia maendeleo ya sayansi mkoani Lindi

Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania Young Scientists Tanzania (YST) imeendesha mashindano ya kuhamasisha na kuwanoa wanafunzi wa sekondari kwenye sekta ya sayansi kwa kushindanisha shule 15 za Wilaya ya Lindi katika kubuni tafiti bora za kisayansi.

Mashindano hayo yaliambatana na utoaji wa tuzo na zawadi kwa wanafunzi walioibuka washindi kwa kubuni tafiti bora na zenye tija ikiwa ni sehemu ya kuleta hamasa kwa wanafunzi wengine kupenda sayansi ya vitendo na kubuni tafiti zilizo bora.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Afisa Elimu Mkoa wa Lindi Mwl Joseph Mabeyo ametoa pongezi nyingi kwa Taasisi ya YST kwa kuja na ubunifu wa kuanzisha mashindano ya kuhamasisha sayansi kwa wanafunzi kwani yanasaidia kuwajengea uwezo vijana wa kuwa wanasayansi mashuhuri na kuwa na vipaji vya kutumia teknolojia kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa vijana kuwekeza muda wao kwenye sayansi hasa kwa kuwa taifa linauhitaji mkubwa wa wanasayansi watakaochagiza maendeleo endelevu ya viwanda na uzalishaji kwa kutumia sayansi. Jitihada hizi zimekuja kwa wakati sahihi ambapo Dunia iko kwenye mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia.

“Nimeridhishwa sana na kazi kubwa ya YST ya kuhamasisha maendeleo ya sayansi kwa vijana hasa kwa Mkoa wa Lindi, niwasihi vijana kuwekeza nguvu zenu na muda kwenye sayansi kwa kuwa ndio njia itakayoweza kuwainua katika taaluma yenu na katika maendeleo yenu,” amesema Mwl Mabeyo.

“Kupitia mradi huu wapo wanafunzi ambao waliweza kutengeneza dawa ya kufukuza mbu kwa kutumia mimea ya asili ambayo ilisaidia na inaendelea kusaidia jamii kwa kiasi kikubwa kukabiliana na magonjwa ya malaria, hii ni hatua nzuri sana,” ameeleza Mwl Mabeyo.

Mgeni rasmi alishiriki katika kutoa tuzo kwa wanafunzi washindi wa jumla kutoka shule ya sekondari Nkowe ambao ni Daniel Mlelwa na Janerose Augustin waliobuni mradi wa kutengeneza dawa ya tumbo na kuzuia kuharisha kwa kutumia magome ya mwembe.

Shule 15 za Mkoa wa Lindi zilishiriki katika mashindano hayo, ambapo shule sita zilifuzu kushiriki mashindano ya sayansi kitaifa yanayotarajiwa kufanyika Mwezi Desemba mwaka huu.

Akimkaribisha Ofisa Elimu Mkoa wa Lindi, Mwanzilishi mwenza wa YST, Dkt. Gozibert Kamugisha amesema kuwa mashindano haya yanaongeza hamasa kwa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi pamoja na kubuni tafiti zilizo bora na zenye tija kwa jamii.

“Zipo tafiti muhimu za kibunifu ambazo zimeleta mafanikio kwa jamii ya sasa ikiwemo mradi wa kufukuza mbu ambao ulibuniwa na mwanafunzi wa sekondari na kwa sasa upo sokoni unatoa huduma kwa wananchi, kupitia ubunifu huu wanafunzi wameweza kuwa na ujuzi wa kubuni tafiti mbalimbali zilizo na bora na zenye manufaa kwa jamii,” amesema.

Ameongeza kuwa hii ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono adhma ya Serikali ya kukuza maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa wanafunzi ili kupata wabunifu wa kuchagiza maendeleo ya viwanda nchini.

“Niwatake wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kuunga mkono jitihada hizi na kuwaendeleza vijana hawa wabunifu kwenye fani hii ya sayansi ili ubunifu wao usipotee,” ameeleza Dkt. Kamugisha.

Kwa upande wake Mshauri wa Masuala ya Kijamii kutoka Kampuni ya Shell Tanzania Ndugu Msomisi Mbenna amesema kuwa Kampuni ya Shell imekuwa mdhamini wa muda mrefu wa mashindano haya ya Wanasayansi kwa lengo la kupata wabunifu wa sayansi watakaoweza kuchangia kwenye maendeleo ya uchumi wa teknolojia.

“Tunafurahi kuendelea kuunga mkono juhudi hizi za YST kwa kuwa ni mojawapo ya mradi wenye matokeo chanya na yanayoonekana kuleta tija,” ameeleza Msomisi.

Ameongeza kuwa program hii ya YST tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, imesaidia kukuza ujuzi na ubunifu kwa wanafunzi wengi wa sekondari pamoja na kuleta hamasa ya kubuni tafiti mbalimbali za sayansi zenye kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents