Habari

Daktari achunguzwa kwa kifo cha kichanga

DAKTARI wa watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anachunguzwa kwa madai kwamba anahusika na kifo cha mtoto mchanga hospitalini hapo kutokana na kujihusisha na ajira nyingine ya kudumu kwenye hospitali binafsi ya Aga Khan, Dar es Salaam kinyume cha sheria, HabariLeo imebaini.

Maulid Ahmed


DAKTARI wa watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anachunguzwa kwa madai kwamba anahusika na kifo cha mtoto mchanga hospitalini hapo kutokana na kujihusisha na ajira nyingine ya kudumu kwenye hospitali binafsi ya Aga Khan, Dar es Salaam kinyume cha sheria, HabariLeo imebaini.


“Uchunguzi unaendelea. Kamati ya Nidhamu inalishughulikia na tumeanza kumchukulia hatua za kinidhamu,” Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Leonard Lema aliiambia HabariLeo katika mahojiano maalumu bila kutaja hatua hizo huku akiahidi kuelezea baadaye baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa suala hilo.


Profesa Lema alisema daktari huyo anatakiwa ajieleze kwa maandishi huku uchunguzi ukiendelea na iwapo itathibitika aliajiriwa sehemu mbili adhabu yake ni kumtaka aache kazi Aga Khan au kufukuzwa kazi na kutakiwa kulipa fedha zote alizochukua kama mshahara wakati akifanya kazi sehemu mbili kutokana na kitendo hicho kuhesabika kama wizi. Vile vile anaweza kupewa adhabu nyingine kali na wanataaluma wenzake ikiwamo kusimamishwa udaktari.


Imebainika kwamba daktari huyo, ambaye kutokana na sababu za kisheria kwa sasa tutamtaja kwa jina la Dk M, aliajiriwa na hospitali ya Muhimbili Novemba mwaka jana ikiwa ni miezi miwili baada ya kuajiriwa na hospitali ya Aga Khan.


Gazeti hili limefahamishwa kwa uhakika kwamba kutokana na kuhangaika katika ajira hizo mbili, Julai mwaka huu anadaiwa kusababisha kifo cha mtoto mchanga wa siku moja ambaye alikosa huduma kwa vile hakuwapo zamu kama alivyopaswa.


Alipoulizwa na HabariLeo kuhusiana na tuhuma hizo, Dk. M alikiri kuwahi kuwa na ajira sehemu mbili na kuongeza; “Mimi niliomba kazi sehemu mbalimbali na nikapata Aga Khan lakini baadaye nikapata Muhimbili na hapo lengo langu likawa kubaki Muhimbili kwa sababu ni serikalini na ninataka baadaye nisome. Unajua private (hospitali binafsi) huwezi kusoma.


“Lengo langu si kufanya kazi sehemu zote ila nilichelewa kuacha kazi Aga Khan unajua nilikuwa kwenye hatua za kuacha siku nyingi lakini sasa nimeshaacha na kubaki hapa Muhimbili,”alisema


Kuhusu tuhuma za kuboronga kazi na kusababisha kifo alisema; “Hiyo Julai 11 mimi sikuwa zamu hivyo ni tuhuma za uongo na hakuna ushahidi wowote na katika kipindi hicho sijawahi kuharibu kazi Muhimbili. Lakini sasa wanachunguza tuhuma hizo na ukweli utajulikana”.


Alisema alikuwa anakwenda Aga Khan kufanya kazi siku ambazo hayupo zamu Muhimbili na muda wa baada ya kazi na kwamba hakuwahi kwenda Aga Khan muda anaotakiwa kuwa Muhimbili.


Kwa mujibu wa taratibu na mkataba wa ajira, daktari aliyeajiriwa katika hospitali ya serikali haruhusiwi kuajiriwa katika hospitali nyingine isipokuwa anaweza kufanya kazi baada ya muda wa kazi. Pia ukiajiriwa Aga Khan huruhusiwi kufanya kazi katika hospitali nyingine.


Uchunguzi wa HabariLeo umeonyesha kwamba akiwa hospitali ya Muhimbili, daktari huyo anafanya kazi katika kitengo cha watoto sehemu ya upasuaji wakati kwa upande wa Aga Khan alikuwa akifanya kazi za udaktari wa kawaida.


“Dk. M anapokuwa Muhimbili hufanya kazi kwa uficho hata kutovaa koti la madaktari kwa hofu ya Aga Khan kufahamu kuwa ameajiriwa sehemu nyingine,” kilisema chanzo cha habari.


Inadaiwa daktari huyo alipokuwa zamu Muhimbili na wakati huohuo kuhitajika Aga Khan, alikuwa akiwaacha watoto wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji kwa dharura, hali ambayo inadaiwa kusababisha kifo cha Julai 11 mwaka huu.


Mtoto aliyekufa anadaiwa alizaliwa huku utumbo wake ukiwa umejikunja na ilitakiwa afanyiwe upasuaji ili kuunyoosha lakini Dk M alipopigiwa simu inadaiwa alishindwa kutoka Aga Khan kwenda kuokoa maisha ya kichanga hicho.


“…badala yake alimpigia simu kiongozi wake na mtoto huyo alipochukuliwa kupelekwa chumba cha upasuaji alishakata roho na mambo yakaisha hivi hivi,” kilisema chanzo cha habari. Inadaiwa wakati wote huo, Dk. M amekuwa akilindwa na mmoja wa madaktari wa juu hospitalini hapo.


Baada ya gazeti hili kufuatilia taarifa hizo katika hospitali ya Aga Khan na Muhimbili, uongozi wa hospitali hizo ulikiri kumuajiri daktari huyo.


Kwa upande wa Aga Khan, mmoja wa viongozi wake ambaye hakupenda kuandikwa gazetini alisema hospitali hiyo ilimuajiri Dk. M Agosti mwaka jana kwa mkataba wa miaka miwili na katika kipindi chote hicho hawakuwa wanafahamu kama ameajiriwa Muhimbili.


“Utaratibu wetu wa ajira ni kwamba huruhusiwi kuajiriwa sehemu nyingine na tumemuajiri yeye kwa mkataba wa miaka miwili. Wewe ndiyo unatupa taarifa za kuwa ameajiriwa sehemu nyingine lakini tutamuita…,” alisema kiongozi huyo.


Kufuatia ufuatiliaji huo wa HabariLeo uongozi wa hospitali hiyo ulimuita na kumuuliza. Alikanusha na siku iliyofuata, Septemba 14, aliandika barua ya kuacha kazi.


Mwandishi wa habari hizi alipofuatilia Muhimbili, Mkurugenzi Mtendaji Profesa Lema alikiri kuwa Dk. M ni mfanyakazi wake aliyeajiriwa Novemba mwaka jana.


“Mimi sifahamu kama ana ajira mbili na kwa uraratibu wa serikali huruhusiwi kuajiriwa sehemu mbili. Mimi nina madaktari 300 na wafanyakazi wote jumla ni 2,600 siwezi kufahamu mambo yote lakini nashukuru kwa kuniletea taarifa hizo na sasa hivi nitafuatilia na kukupa taarifa,” alisema.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents