Tupo Nawe

Exclusive: Uchambuzi wa album ya Navy Kenzo ‘Above In A Minute’ (track by track)

Baada ya kuizungumzia kwa kipindi kirefu, hatimaye Navy Kenzo wameachia album yao mpya ‘Above In A Minute.’ Kuachia kwa album hiyo kumewafanya waufunge mwaka 2016 kwa kishindo, lakini pia kuufungua mwaka mpya 2017 kwa kishindo zaidi.

Ni hakika kuwa AIM inakuja kuwa album itakayotumika kama mfano halisi, wa muhimu na wa uhakika kuwa inawezekana bado kwa wasanii wa Tanzania kuachia album, zikauza na zikafanikiwa licha ya kutoweka kwa mfumo wa usambazaji wa album uliosababishwa na sababu chungu mzima.

Navy Kenzo wamethubutu na wameweza. AIM inawaweka katika daraja lao pekee kwa Tanzania. Ukichanganya na tuzo walizoshinda mwaka jana pamoja na nomination katika tuzo zinazoheshimika kama MTV MAMA, video za nyimbo zao 3 (Game, Kamatia na Feel Good), zilizoshika chati mbalimbali za TV na kuvutia views zaidi ya milioni 4.9 kwa pamoja katika mtandao wa Youtube, album yao, AIM sasa inawafanya rasmi kuwa kundi la muziki la pili lenye mafanikio zaidi Afrika Mashariki baada ya Sauti Sol la Kenya.

Kabla sijaanza kuchambua ngoma 11 zilizomo ndani, nakiri kuwa AIM ndio album niliyoifurahia kuisikiliza mwanzo hadi mwisho mara nyingi na kwa kurudia sana. Nimekuwa nikipata album nyingi za wasanii wa Marekani ambazo huishia kusikiliza nyimbo chache tu za zingine nikishindwa kuzimaliza kutokana na kuwa mbovu, lakini si kwa AIM. AIM si album ya mchezo mchezo, sio compilation ya nyimbo za kujazilia album. Lahasha, hii ni album kali na bora kabisa niliyowahi kuisikia katika miaka mingi.

Huwezi kupeleka wimbo wowote mbele, kila wimbo uliomo kwenye album ni hit na unaweza kutoka kama radio single na ukafanya vizuri hadi kushika charts. Nyimbo nyingi kwenye album hii zimetayarishwa na Nahreel, kasoro Done, Young na Feel Good Remix.

Na tuanze uchambuzi huu:

1. LINI F/ ALIKIBA

Nawapongeza Navy Kenzo kwa uamuzi wa kuifanya Lini kama ngoma ya kuifungua album hii. Lini ni wimbo mtamu, chotara wa dancehall, R&B na Bongo Flava. Aika ndiye anayeufungua wimbo huu wa mapenzi kwa verse tamu inayokuja kupokelewa na kibridge kifupi cha Nahreel chenye ladha ya dancehall.

Kwenye chorus wanashirikiana wote watatu, huku Nahreel akioongoza. Alikiba anaingia kwenye verse ya pili kwa sauti tamu na kuifanya ngoma iakisi ladha yake muhimu yenye Bongo Flava. Kiba kwenye verse yake anathibitisha uwezo wake alionao wa kubadilika kama kinyonga na kuzalisha ladha ya aina yake ya R&B.

Lini ni wimbo ambao tayari umekuwa gumzo nchini huku redio zikiwa zimeshaanza kuucheza. Ni wimbo utakaofanya vizuri hasa ukizingatia fanbase kubwa iliyopo nyuma ya Kiba -TeamKiba. Kinachosubiriwa sasa ni video ya wimbo huu ambayo hapo awali zimewahi kufanyika jitihada za kuifanya, lakini zilizogonga mwamba kutokana na ratiba zao kupishana.

2. BHENGA

Bhenga kama jina lake ni wimbo wa kuchezeka zaidi. Baada ya sauti fupi ya Nahreel, ni Aika ndiye anayefungua na sauti yake kusindikizwa na visauti vya watoto na chakacha zinazosikika kwenye masikio mawili kama ukisikiliza kwenye earphones. Nahreel anaingia mbele kidogo na bridge inayosindikizwa na vinanda vya kuvutia na synth zilizocharazwa vyema. Nahreel anaingia kwenye verse ya pili yenye Kiswahili na Patois.

Verse ya tatu wanapokezana wote na Nahreel anaumalizia wimbo kwa kurudia mara kibao neno Bhenga.

3. BAJAJ F/ PATORANKING

Bajaj ni moja ya nyimbo kubwa na kali zaidi kwenye AIM. Of course licha ya kuundwa vizuri, uwepo wa Patoranking kwenye ngoma hii, unaifanya uwe mzito tayari. Bajaj ni wimbo chatara ya Dancehall na R&B. Wimbo unaanza kwa piano iliyochezwa kwa kuvutia na Nahreel ndiye anauyefungua wimbo kwa kishindo na kuelezea umuhimu wa kumfanya girlfriend wako ajisikie kuwa anapendwa na kwamba yupo mwenyewe. Na ana shauri ili mpenzi wako aweze kujisikia hivi, unapaswa kumpeleka kula dinner ama kumfungulia mlango wa gari mnaposhuka. Chorus inaimbwa na Nahreel, ‘mwanamke sio bajai ukipanda ukishuka unasahau, sio bajaj wala pikipiki.’

Pato anaingia kwenye verse ya pili na sauti yake kali ya dancehall na patois yake utadhani amezaliwa Jamaica. Kwenye verse yake Patoranking anaeleza kuwa usipomjali mpenzi wako, atakuambia goodbye ama mwanaume mwingine atakunyang’anya na kumpeleka Dubai.
Amenifurahisha zaidi kwenye mstari huu, ‘better take her for vacation, before she puts on probation.’ Aika anamsaidia Patoranking kwa kuyarudia maneno yake ya mwisho kwa kuchomeka Kiswahili.

Kwenye verse yake, Aika anaeleza jinsi yeye alivyopata mwanaume wa pekee (Nahreel) asiyependa makubwa. Verse yake inachagizwa vizuri na base iliyopigwa vyema kwa mkono huku rolling za ngoma zikipokezana kwa ustadi.

4. FEEL GOOD

Feel Good ni wimbo wa kwanza kutoka kwenye album hii na ndio wenye video rasmi hadi sasa. Licha ya kuwa ni wimbo mzuri, kwangu mimi, Feel Good ndio wimbo dhaifu baada ya Bhenga. Hii ni kwasababu AIM imejaza hits tu na hivyo katika kutengeneza chati yake yenyewe, kuna nyimbo nzuri zinazoweza kuonekana za kawaida miongoni mwa nyenzake.

Hata hivyo, Feel Good umekuwa na mafanikio yanayoweza kuipa nafasi zaidi AIM kutusua nje ya mipaka ya Tanzania. Ni kwasababu huu ni wimbo unaodaiwa kufanya vizuri sana nchini Israel na katika nchi za Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.

Hiyo ilipelekea DJ na producer maarufu wa Israel, Moshe Buskila awaombe atengeneze official remix yake ambayo nayo imejumuishwa kwenye album. Moshe hakuishia hapo, alitengeneza pia wimbo wa mwisho kwenye album hii, Young.

5. DONE F/ MR EAZI

Done ni wimbo wa kuachana – break up song. Wamemshirikisha msanii mwenye asili ya Nigeria lakini mwenye makazi yake nchini Ghana, Mr Eazi. Done ni moja ya nyimbo ninazozipenda sana kwenye album hii. Kasoro kwangu binafsi niliyoiona kwenye wimbo huu ni katika mixing ya sauti ya Eazi katika verse yake. Naamini mtayarishaji wa wimbo aliamua kuiweka hivyo makusudi lakini inatia ukakasi kama unauisikiliza kwenye earphones na kuisikia sauti ya Eazi ikiwa imeelemea kwenye sikio moja.

6. MORNING

Kwa ujumla, Morning ndio wimbo ninaupenda zaidi kwenye AIM. Si tu kwasababu ya ujumbe wake mzuri wa kimapenzi, bali pia ni wimbo ambao Nahreel ameimba kwa hisia zaidi pengine kuliko nyimbo zote za album hii. Bila shaka wakati anaingiza sauti alikuwa ameshikilia picha ya mpenzi wake Aika kumpa hisia za ukweli – ha ha ha! Na pia kwenye wimbo huu Nahreel amethibitisha uwezo wake mkubwa katika kutengeneza melody za kuvutia na kuibadilisha apendavyo kwenda katika milindimo ya dancehall na pia kwenye R&B.

Chorus yake ni tamu sana na usiposikiliza vizuri unaweza usiijue ni ipi hadi pale Aika atakapomaliza verse yake na inasikika tena. Hisia alizokuwa nazo Nahreel zinahamia pia kwa Aika anapoingia na verse yake na awamu hii sauti yake inakuwa nyembaba zaidi. Ni verse tamu na inadhihirisha pia ujuzi alionao katika kuyavuka mawimbi mbalimbali ya sauti. Huu ni wimbo mzuri kinoma kumdedicate umpendaye.

7. FEEL GOOD (REMIX)

Kama ulidhani kuwa Feel Good ni club banger, hebu sikiliza remix yake iliyotayarishwa na DJ Moshe Buskila wa Israel. Imechangamka zaidi sasa hivi na bila shaka itakuwa kipenzi cha MaDj wengi kwenye viota vya starehe duniani. Pia Moshe amefanikiwa kuichanganya vizuri katika mahadhi ya EDM na dancehall iliyochangamka kweli kweli.

8. LINI (PART 2)

Kama umeliona cover la nyuma la AIM huenda ukawa umehisi kuwa LINI PART 2 an LINI waliyomshirikisha Alikiba vinaweza kufanana kiasi . Hapana, Part 2 iko tofauti sana – tuseme ni wimbo unaojitegemea na walikuwa na uwezo wa kuupa jina tofauti na usishtukie kitu. Lini Part 2 ni wimbo wa R&B iliyochangamka na vinanda vyake vinaweza kukufanya uhisi unasikiliza wimbo wa R&B wa Marekani ambao huukumbuki ni wa nani.

9. BLESS UP F/ ROSA REE

Bless Up ni certified club banger na moja ya ngoma ninazozipenda sana kwenye AIM. Unachezeka kichizi na kama wakifiria kuja kufanya video yake wimbo huu utakuja kuwa hit dunia nzima hasa katika nchi za Ulaya na Carribean. Bless Up naufananisha na baadhi ya nyimbo za zamani za Sean Kingston. Na kama bado ulikuwa na hofu kuwa Nahreel ni msanii namba moja wa dancehall kwa sasa, nina uhakika humu huwezi kubisha.
Mchango wa msanii wa label yao (The Industry), Rose Ree ni wa muhimu kwenye ngoma hii. Humu ameonesha uwezo wake wa kuchanganya rap na dancehall pamoja na uimbaji mtamu wa R&B.

10. NIPENDELEE F/ R2BEES

Nipendelee ni wimbo mwingine wa mapenzi, mzuri wenye bonge la beat na chorus ya Kiswahili. Katika chorus iliyoimbwa na Nahreel chini inasikika sauti ya G-Nako. Nahreel ndiye anayeanza kwa verse ya Kiswahili, kali mno kabla ya mbele kuchomeka patois. Member wa kundi la R2Bees la Ghana, yule anayeimba, anaingia kwenye verse ya pili vizuri kabisa. Aika naye anaingia kwenye verse ya pili na kuongeza bridge tamu ‘treat me like a real woman, you got me feel more human.’ Member wa kundi la R2Bees anayerap hasikiki kwenye wimbo huu – labda kama naye aliimba.

11. YOUNG

Young ni wimbo uliotayarishwa na DJ Moshe Buskila. What do you expect? Ni bonge moja la EDM linaloifunga album hii kwa kishindo.
Ninaipa nyota ngapi hii kati ya 5? Hii naipa zote 5. Nenda kachukue nakala yako sasa.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW