Habari

Furaha amlilia Zuch, awataka vijana kupendana, kusaidiana

MKURUGENZI wa Furaha Media, Furaha Dominick amewataka vijana kupendana, kushirikiana, kusaidiana, kupeana fursa, kuneneana yaliyomema pamoja na kuishi katika mienendo ya kumpendeza Mungu.

Furaha ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa mpiga picha na mwandishi wa habari wa Millardayo na Ayo Tv, Noel Mwingila (Zuch Zuchero) aliyefariki dunia alfajiri ya Aprili 26, 2024 baada ya kupata ajali ya pikipiki maeneo ya Makonde – Mbezi, Dar es salaam.

Amesema ni muhimu vijana wakapendana na kuneneana yaliyomema na kwamba linapotokea jambo lolote linalomgusa kijana mwingine wawe mstari wa mbele na kuungana na kusaidiana.

Amesema Zuch amekuwa kijana wa kuigwa kwa namna alivyoishi na watu vizuri na kusaidia wengine hivyo Taifa limepoteza nguvu kazi na litamkumbuka daima kwa jinsi alivyokuwa kijana shupavu, mpambanaji na asiyebagua watu.

“Ukimwangalia Zuch utagundua kuwa alikuwa mtu wa kujishusha sana, alikuwa na jina kubwa lakini hakuwahi kujikweza hata ukiangalia aliacha gari yake na kupanda bodaboda, hiyo yote ni kuonyesha kujishusha kwake.

“Kifo chake kinasikitisha na kuumiza lakini ni mipango ya Mungu haina makosa tunapaswa kushukuru kwa kila jambo, tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Zuch hapa duniani,” amesema Furaha

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule amesema ni vema kuhakikisha waandishi wa habari wanaandika habari zenye tija sio zile za kuleta mtafaruki na kupoteza amani katika nchi yetu.

“Napongeza vyombo vya habari kwa kutuunganisha watanzania na kuwa kitu kimoja katika kuhabarisha kutoa elimu na kuburudisha haya ndio Noel aliyotuachia katika kuyaenzi,”amesema na kuongeza

“Ni juhudi katika kazi,amani,ucha Mungu na kuwa kitu kimoja katika kusema watu vizuri hayaa tumeyaona hapa yanazungumzwa juu ya Noel,”alisema.

Zuch alikua ni mmoja kati ya wapigapicha mahili kwenye tasnia ya habari na matukio.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents