Habari

Jeneza la ajabu lililokaa chini ya ardhi zaidi ya miaka 2,000  lafunuliwa (+Picha)

Jeneza la ajabu lililokaa chini ya ardhi zaidi ya miaka 2,000  lafunuliwa (+Picha)

Wiki tatu zilizopita, wanaakiolojia nchini Misri waligundua jeneza kubwa lililoundwa kwa mawe magumu ya matale (granite) ya rangi nyeusi katika mji wa Alexandria.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha BBC Jeneza hilo lilikuwa limekaa kwa zaidi ya miaka 2,000 bila kufunuliwa. Uvumi ulianza kueneza upesi, kwamba huenda jeneza hilo lilikuwa na mabaki ya kiongozi maarufu wa Wagiriki, Alexander the Great (Alexander Mkuu), au pengine kitu cha laana kubwa.

Image result for Egyptian Officials Open Black Sarcophagus, Find 3 Skeletons Inside

Kwa mujibu wa wataalamu walipolifungua, jeneza hilo halikuwa na hata kimoja kati ya vitu hivyo viwili. Badala yake, waligundua mifupa ya watu watatu na maji machafu sana ya rangi ya hudhurungi ambayo yalitoa uvundo usioweza kuvumiliwa mkali ajabu.

Waziri wa Vitu vya Kale wa Misri alikuwa ameteua kamati ya wanaakiolojia wa kufungua jeneza hilo ambalo liligunduliwa katika eneo kulikokuwa kunafanyika ujenzi.

Image result for Egyptian Officials Open Black Sarcophagus, Find 3 Skeletons Inside

Kwa mujibu wa kituo cha habari cha El-Watan cha Misri, awali walijaribu kuinua kifuniko cha jeneza hilo hadi sentimeta tano hivi juu (inchi 2), lakini uvundo wa ajabu uliwazuia kuendelea na kulazimika kuondoka eneo hilo.

Baadaye walilifungua, wakiwa wamejiandaa kwa vifaaa, wakisaidiwa na wahandisi kutoka jeshi la Misri.

Image result for Egyptian Officials Open Black Sarcophagus, Find 3 Skeletons Inside

“Tuliipata mifupa ya watu watatu, na inaonekana ni kama walikuwa wa familia moja… Kwa bahati mbaya, miili hiyo haikuhifadhiwa katika hali nzuri na ni mifupa pekee iliyosalia,” amesema Mostafa Waziri, katibu mkuu wa Baraza Kuu la Vitu vya Kale Misri.

Akizungumzia wasiwasi uliokuwa umeenea kwenye vyombo vya habari kwamba kufunguliwa kwa jeneza hilo pengine kungesababisha laana kutoka kwa Mafirauni, Bw Waziri alisema: “Tumelifungua na, namshukuru Mungu, kwamba hakujawa na giza duniani.

“Nilikuwa wa kwanza kutazama ndani ya jeneza hilo … na niko hapa, nimesimama mbele yenu… na niko salama.”

Image result for Egyptian Officials Open Black Sarcophagus, Find 3 Skeletons Inside

Licha ya hayo, eneo lilikopatikana jeneza hilo watu wamehamishwa huku kukiwa na wasiwasi kwamba linaweza kutoa hewa yenye sumu, gazeti la serikali ya Misri la Al-Ahram limeripoti.

Wanasayansi wamefanikiwa kuthibitisha kwamba hakuna “Laana ya Miili ya Kale”, lakini je kuna hatari nyingine katika makaburi na majeneza ya kale?

Lodi Carnarvon, aliyefadhili ufukuaji wa makaburi ya Firauni Tutankhamun alifariki baada ya kuumwa na mbu muda mfupi baada yake kufungua kaburi hilo 1923.

Tangu wakati huo, kumekuwepo na uvumi kwamba kuvu au bakteria zilinusurika ndani ya kaburi hilo na kwamba zilimwambukiza nakusabaisha kifo chake.

Lakini F DeWolfe Miller, profesa wa utaalamu wa viini vinavyosabbaisha magonjwa Chuo Kikuu cha Hawaii ameambia National Geographic kwamba hakuna hatari yoyote.

“Hatujafahamu kuhusu kisa hata kimoja cha mwanaakiolojia au mtalii aliyewahi kuathirika [kutokana na bakteria au kuvu kutoka makaburini],” aliambia jarida hilo.

Wataalamu wanasema watu hao watatu ambao mabaki yao yalipatikana Alexandria huenda alikuwa wanajeshi enzi za Mafirauni.

Fuvu la kichwa la mmoja wao lina nyufa zinazoashiria jeraha la mshale.

Sanamu ndogo ya alabasta ambalo ni jiwe jeupe laini lililofanana na marumaru ambayo imeharibika kiasi cha kutojulikana ilikuwa sanamu ya nini, pia ilipatikana pamoja na jeneza hilo.

Jeneza hilo lina urefu wa karibu mita mbili (futi 6.5) kwenda juu na urefu wa mita tatu, na ndilo kubwa zaidi la aina yake kuwahi kugunduliwa.

Lina uzani wa tani 27 na linaaminika kuwa la enzi za Wagiriki wafahamikao kama Ptolemy ambao ulianza mwaka 323 baada ya kifo cha Alexander the Great.

Wanaakiolojia sasa watachunguza jeneza hilo kwa kina kubaini waliozikwa humo ndani walikuwa wanaishi wakati gani na waliishi vipi.

 

Related Articles

2 Comments

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents