Michezo

Nitaisaidia Azam FC- Shaaban Idd

Mshambuliaji wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shaaban Idd, anaimani kubwa ya kufanya vizuri atakaporejea tena dimbani ataisaidia timu hiyo huku akimwomba Mwenyezi Mungu amjaalie aweze kurejea vema.

Idd ambaye anasumbuliwa na maumivu ya nyonga yake ya kulia aliyotibiwa kwa kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini, na tayari ameshaanza mazoezi madogo madogo ya ‘gym’ tokea hapo jana tayari kabisa kuanza safari ya kurejea dimbani hivi karibuni.

Mshambuliaji huyo ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kwa kipindi chote alichokuwa akiuguza majeraha amefanikiwa kupata sapoti kubwa kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa Azam FC na wachezaji wa timu hiyo.

“Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya yangu hivi sasa imekaa vizuri, pili napenda kuishukuru timu yangu ya Azam FC viongozi wake wote, wachezaji wote kwa kufanikisha suala langu limekwenda vizuri, nimeanza mazoezi mepesi mepesi sijaanza kuingia uwanjani ila baada ya siku 10 natarajia kuanza kukimbia, ila hivi sasa nipo gym na physio (daktari wa viungo).” Amesema Idd.

Shaaban Idd  ameongeza “Baada ya siku 10 nitaanza kukimbia kidogo kidogo uwanjani ila mpaka mwezi wa 12 nitakuwa nimeshaanza kucheza Inshaallah.”

Nyota huyo ambaye hadi anaumia alikuwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, alisema

kitu kikubwa anachokikosa kwa muda huu aliokuwa nje ya dimba ni kucheza mpira, akidai kuwa mpira ndio kazi yake na ndio kitu anakipenda sana.

Akizungumzia namna alivyojipanga kurejea vema mara baada ya kupona asilimia 100, Idd amesema matumaini yake ni makubwa sana kwa sababu msimu uliopita alifanya vizuri na kufunga takribani mabao 13 msimu mzima katika mechi za Ligi Kuu, Kombe la Mapinduzi na Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

“Natarajia nikikaa vizuri Mungu akijaalia, naomba tu anijalie niweze kurudi katika hali yangu ambayo nilikuwa nayo siku zote, nitafanya vizuri na kusaidia timu yangu na kama sasa hivi timu yangu iko na dalili ya kuwania kuchukua ubingwa kwa hiyo tutafanikisha hili suala, Mungu tu ajaalie afya nzuri,” alisema mshambuliaji huyo aliyekulia kwenye kituo cha kukuza vipaji cha Azam Academy

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents