Afya

UTAFITI: Uzalishaji mbegu za kiume waporomoka duniani

Utafiti mpya uliofanywa na Chuo Kikuu cha Hebrew-Hadassah Braun cha Jerusalem umebaini kuwa kiwango cha mbegu za kiume kwa wanaume duniani kimepungua kwa zaidi ya asilimia 50.

Utafiti huo umeeleza kuwa kiwango na ubora wa mbegu za kiume kimeshuka katika kipindi cha chini ya miaka 40 na hakuna ushahidi kuwa kiwango hicho kitaongezeka.

Hata hivyo utafiti huo umesisitiza kuwa kiwango na idadi ya mbegu za kiume kimeshuka zaidi kwa wanaume wa nchi za Magharibi.

Pia imeelezwa kuwa kushuka kwa ubora na idadi ni tishio kwa uwepo wa watu duniani.

“Utafiti huu unawapa wasomi kazi kubwa zaidi hasa kwani idadi ya mbegu za kiume na afya ya binadamu ni muhimu zaidi. Wasomi sasa wanatakiwa kuchunguza chanzo cha kushuka huko kwa idadi ya mbegu za kiume na namna ya kutatua tatizo hilo,” amesema Dk Hagai Levine.

Profesa Hagai ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mazingira na Afya wa Chuo cha Hebrew, amefanya utafiti huo kwa kushirikiana na Profesa Hannah Swan wa Chuo Kikuu cha New York kitengo cha Afya ya Jamii.

Madaktari wengine waliohusika katika utafiti huo ni wa Brazil, Denmark, Israel, Hispania na Marekani. Utafiti huo umefafanua zaidi kuwa kiwango na idadi ya mbegu za kiume ni kipimo sahihi cha uwezo wa kuzalisha wa mwanaume.

Na Emmy Mwaipopo

Chanzo: Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents