Habari

Wabakaji watisha Z’ bar

KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni juhudi za kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ubakaji, Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar, limeunda kamati maalumu ya kupambana na watu wanaofanya vitendo hivyo.

na na Mwandishi Wa Tanzania Daima

 

KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni juhudi za kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ubakaji, Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar, limeunda kamati maalumu ya kupambana na watu wanaofanya vitendo hivyo.

 
Katika hali inayowashangaza watu wengi visiwani humu, kumekuwa na ongezeko la matukio ya ubakaji, walengwa wakubwa wakiwa ni wasichana vigoli, wakiwamo wanafunzi.

 
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mussa Ali Mussa, alisema kwamba vitendo vya ubakaji vinaongezeka kwa kasi ya kutisha na kujenga wasi wasi miongoni mwa wazazi pamoja na wanafunzi.

 
Alisema kwamba takwimu zinaonyesha vitendo hivyo vimeongezeka kwa asilimia 50, na visipodhibitiwa vinaweza kuwa chanzo kikuu cha kasi ya maambukizi ya maradhi ya UKIMWI.

 
Alisema kwamba mwaka 2005 matukio ya ubakaji yaliyoripotiwa yalikuwa 16, lakini mwaka jana kulikuwa na kesi 34, hali inayoonyesha kasi kubwa ya ongezeko la vitendo hivyo.

 
“Tumeamua kuunda Kamati Maalumu kwani vitendo vya ubakaji vinaongezeka kwa kasi kubwa na vinaathiri watu wazima pamoja na watoto,” alisema Kamanda huyo.

 
Aliwataja wajumbe wa kamati hiyo, ambayo itakuwa chini ya uenyekiti wake, kuwa watatoka katika ofisi ya mkoa na wilaya pamoja na maofisa kutoka Idara ya Ustawi wa Jamii.

 
Kamanda Mussa alisema kwamba wasichana, wakiwemo wanafunzi, wamekuwa wakinyemelewa na wanaume na baadaye wengine kubakwa wakiwa katika shughuli zao za kijamii au matembezi ya kawaida.

 
Juhudi hizo za polisi zinafuatia kubaini kuwa ushahidi wa kesi nyingi za ubakaji umekuwa ukivurugwa na familia kutokana na ufahamu mdogo wa sheria kuhusiana na makosa ya aina hiyo.

 
Alisema mara nyingi, wanafamilia wamekuwa wakiwalazimisha wasichana wanaokabwa kufua nguo za ndani na kuosha sehemu za siri, na hivyo kuharibu vielelezo muhimu.

 
Kamanda Mussa alisema kwamba kila serikali ya mtaa itapewa mafunzo ya wiki moja juu ya njia madhubuti ya kuhifadhi ushahidi na pia kuwafikisha waathirika wa matukio hayo katika vituo vya Polisi na baadaye hospitali kwa muda muafaka.

 
Licha ya ongezeko la matukio hayo, kamanda huyo alisema Polisi wameshindwa kupeleka kesi nyingi za ubakaji mahakamani, kutokana na kukosekana kwa ushahidi.
Alieleza kwamba hali hiyo inasababisha wasichana hasa wanafunzi kupatwa na wasi wasi mkubwa wanapokuwa katika shughuli zao, ikiwemo wakati wa kwenda na kurudi masomoni.

 
Katika kilele cha maamdhimisho ya Siku ya Wanawake mapema mwezi huu, Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Asha Abdallah Juma, alisema vitendo vya unyanyasaji wanawake vinaongezeka na kuchangia kuenea kwa maambukizi ya UKIMWI.

 
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents