Habari

Wanafamilia wauawa kwa sumu

WATU watano wa familia moja wakazi wa Kijiji cha Kasongati, Tarafa ya Kakonko wilayani Kibondo wamekufa kwa kula chakula kinachosadikiwa kuwekewa sumu na jamaa yao.

Fadhili Abdallah, Kigoma


WATU watano wa familia moja wakazi wa Kijiji cha Kasongati, Tarafa ya Kakonko wilayani Kibondo wamekufa kwa kula chakula kinachosadikiwa kuwekewa sumu na jamaa yao.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Patrick Byatao, alisema jana kwamba watu hao walipatwa na mkasa huo mwanzoni mwa wiki na kufa mmoja baada ya mwingine hadi kufikia Jumatano.


Akieleza chanzo cha mkasa huo, alisema Jumatano wanafamilia ya Marko Ndeyecha walikula chakula cha mchana na ilipofika saa 11 jioni Makrina Marko alianza kulalamika kuumwa tumbo na kichwa na ilipofika saa nne usiku alifariki.


Baada ya mtu huyo kufariki, kamanda Byatao alisema kuwa watu wengine wa familia hiyo walianza kulalamika kuzidiwa na maumivu na ilipofika saa sita usiku Jenitha Marko mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kasongati aliaga dunia.


Alisema kuwa Novemba 27 katika vipindi tofauti watu wawili wa familia hiyo Reuben Marko (13) mwanafunzi katika Shule ya Msingi Kasongati na Saba Marko (3) walifariki dunia.


Wakati wanafamilia wakiwa katika majonzi ya kuondokewa na watu wanne Jumatano Erick Marko (5) alifariki na kufanya idadi ya wanandugu hao waliokufa kufikia watano.


Kutokana na vifo hivyo vya mfululizo ndugu waliobaki walikimbilia kituo cha Afya Kakonko kwa ajili ya matibabu ambako Christina Marko (18) na Elimana Marko (11) walilazwa. Hali zao kwa sasa zinaendelea vizuri.


Inaelezwa kuwa chanzo cha mkasa huo ni kutokuelewana kati ya Ndeyecha na ndugu yake mmoja aishiye Burundi ambaye alifika nyumbani hapo kudai ng’ombe wawili lakini aliambulia ng’ombe mmoja na ndama.


Kamanda Byatao alisema baada ya ndugu huyo kukosa ng’ombe alirudi Burundi ambako aliacha ujumbe unaosema “wataona kitakachotokea.”


Alisema kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo.


Sampuli ya mabaki ya chakula na viungo mbalimbali vya marehemu hao vimechukuliwa kwa ajili ya kuvipeleka kwenye Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kanda ya Ziwa.


David Azaria anaripoti kutoka Geita kwamba, mkazi wa Kijiji cha Bujulamuyenze amemuua mkewe baada ya kumchinja kwa kisu shingoni na kisha kujinyonga kwa kamba kwa kile kinachodaiwa kuwa wivu wa mapenzi.


Tukio hilo lilitokea juzi asubuhi katika kijiji hicho baada ya kinachodaiwa ni kumkuta mkewe nyumbani kwake akifanya mapenzi na mwanamume mkazi wa kijiji jirani.


Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza, Zelothe Steven, alipoombwa kuzungumzia tukio hilo alisema hajapata taarifa.


Waliokufa katika tukio hilo ni Martine Ngalu (35) na mkewe Gaudencia Anthony (30). Kwa mujibu wa wanakijiji, kabla ya mwanamume kujiua, aliandika barua na kuelezea chanzo cha kufanya mauaji dhidi ya mkewe.


Naye Gurian Adolph anaripoti kutoka Sumbawanga kwamba Modest Nkondo (60) ameuawa kwa kuchinjwa na watu wasiofahamika Jumatano usiku katika Kijiji cha Tululu ingawa inaaminika kwamba chanzo ni ugomvi uliosababishwa na ndama wa aliyeuawa kula mahindi kwenye shamba la Khatib Chakari (25) siku ya tukio.


Polisi inamshikilia Chakari kwa uchunguzi.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents