Habari

Waziri Majaliwa awasilisha fomu za maadili ya viongozi wa umma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema amekwishawasilisha tamko la maadili ya viongozi wa umma kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma tangu Alhamisi hii ya Disemba 28, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari kijijini kwake Namahema ‘A’ wilayani Ruangwa mkoani Lindi,Waziri Mkuu amesema fomu hizo zilipokelewa jana na amekwishapatiwa barua ya kupokea tamko hilo.

“Nimewaita hapa ili kuthibitisha kuwa nimetekeleza takwa hilo la kisheria na tayari Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi ya Umma imekiri kupokea tamko langu kwa barua hii hapa,” alisema Waziri Mkuu huku akionyesha barua hiyo ambayo ilisainiwa na Jaji Harold Nsekela, Desemba 28, 2017.

“Kwa kuzingatia mfano ulioonyesha na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ninawaagiza viongozi wote wanaotakiwa kujaza fomu hizo kwa mujibu wa sheria wafanye hivyo na kuziwasilisha ifikapo tarehe 31 Desemba, 2017 saa 10 jioni,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Alisema anawakumbusha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu wote na viongozi wote walioko kwenye ngazi za uteuzi wahakikishe wanatimiza takwa ambalo liko kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya Mwaka 1995.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwatakia Watanzania wote heri wakati wanaposubiri kumaliza mwaka 2017 na kuwatakia heri na fanaka katika maeneo waliyopo wanapojiandaa kuupokea mwaka 2018.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents