Afya

Afya: Utafiti kuhusu ugonjwa wa usonji (autism).

Usonji ama “Autism” ni hali ambayo mtu huwa nayo tangu utotoni ambayo hutambulika kwa mhusika kushindwa kuwasiliana vizuri (communicate) na pia kushindwa kujihusisha na watu wengine katika mambo mbalimbali ya kijamii (socialize) katika hali ya kawaida.

Ishara za usonji zinaweza kuonekana mapema, hata katika umri mdogo wa mtoto wa miezi 6 – 18, ingawa mara nyingi huchukua mpaka watoto wakiwa na miaka 2-5. Uchunguzi wa uwepo wa usonji hufanywa na madaktari watalaamu wa tatizo hili, pamoja na wanasaikolojia kwa kutumia vipimo tofauti. tofauti, ikiwa ni pamoja na kuwauliza maswali walezi wa mtoto, kuangalia na kusoma tabia za mtoto.Ni muhimu sana kugundulika mapema ili huduma za kumsaidia zianze mapema.
Tafiti zinaonyesha mchanganyiko wa sababu za kijenetiki na zisizo za kijenetiki, au mazingira zinapelekea mtoto kuwa na uwezekano mkubwa kupata hali ya usonji.

Sababu za kijenetiki:
Tafiti zinaonyesha tatizo la usonji unakuwepo kwenye familia. Mabadiliko ya kijenetiki yanapelekea mtoto kuwa na uwezekano mkubwa kupata hali ya usonji. Kama mzazi ana mabadiliko hayo, anaweza kumpitisha mtoto (hata kama mzazi hana usonji). Wakati mweingine, mabadiko hayo ya kijenetiki yanaweza kutokea ghafla wakati yai na mbegu zikikutana. Lakini, mabadiliko mengi yanayotokea hayapelekei mtoto kuwa na usonji, bali yanaonngeza uwezekano kuwa na hali ya usonji.

Sababu za Mazingira:
Tafiti zinaonyesha kuwepo na sababu za kimazingira zinaoweza kuongeza – ama kupunguza – uwezekano wa mtoto, ambaye tayari ana mabadiliko ya kijenetiki, kuwa na hali ya usonji. Tafiti pia zinaonyesha kwamba ukubwa wa uchangiaji wa sababu za mazingira ni mdogo.

Hali za kimazingira zinazoongeza kuwepo uwezekano wa mtoto kupata usonji ni kama: -Umri mkubwa wa wazazi (mama zaidi ya miaka 35, na baba zaidi ya miaka 40) -Matatizo ya ujauzito au wakati wa kuzaa (mfano: uzito mdogo, mimba pacha na kuendelea, na watoto njiti sana, wanaozaliwa kabla ya wiki ya 26 ya ujauzito), na mimba zinazofuatana kwa karibu sana, chini ya mwaka mmoja.

Aidha, tafiti zimeonyesha kwamba vitamini zenye folic acid zinazoshauriwa kunywewa na wakina mama wakati wa ujauzito zinapunguza uwezekano wa mtoto kupata hali ya usonji.

Utafiti uliofanywa kwa miaka mingi na Dr John Cannell umeonyesha uhusiano wa moja kwa moja wa upungufu/ukosefu wa Vitamin D wakati wa ujauzito wa mtoto mwenye usonji. Utafiti bado unaendelea kuhusiana na hii sababu ya Vitamin D kutathmini kwa uhakika kwamba usonji unahusishwa na upungufu wa Vitamini D kwa mama wakati wa ujauzito.

Mpaka sasa hakuna tiba ya usonji inayojulikana. Hii haimaanishi kwamba hamna kitu ambacho kinaweza kufanyika kumsaidia mtu/mtoto mwenye usonji. Usonji hutokana na changamoto za kibailojia ambazo huathiri ukuaji na utendaji kazi wa ubongo. Kwa wengi hali hii hudumu maisha yao yote ingawa kama hatua za kuwasaidia kuweza kujitegemea zitachukuliwa mapema iwezekanavyo basi wataweza kufanikiwa kuboresha sana uwezo wao wa kujitegemea.

Chanzo Dr Isaac Maro

Na Laila Sued

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents