Basata kuandaa tamasha la sanaa
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linajiandaa kufanya kongamano kubwa la muziki linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni ili kujadili mwenendo mzima wa fani hii ikiwa ni pamoja na kujenga utambulisho wa muziki wa Tanzania.
Ghonche Materego ambaye ni katibu Mtendaji wa BASATA alisema hayo jana kwenye Ukumbi wa BASATA. Shughuli hiyo inaypotarajia kufanyika kila Jumatatu itfafanua masuala mbalimbali yanayojitokeza kwenye Jukwaa la Sanaa na kusema kwamba,kongamano hilo pamoja na mambo mengine litakuja na majibu kadhaa ya changamoto mbalimbali zinazoikabili fani ya muziki nchini sambamba na kujenga heshima ya wasanii wa Tanzania ndani na nje ya nchi.
Awali Ghonche alisema, ‘Tunakusudia kufanya kongamano kubwa ambalo litahusisha maproducer, wadau wa vyombo vya habari, mapromota, wasanii wote wa muziki na wadau mbalimbali wa sekta ya sanaa ili kwa pamoja tujiulize fani yenyewe iendeshwe vipi na tutajengaje utambulisho wa muziki wetu ili tuweze kuuzika kimataifa alisisitiza Materego.
Aliongeza kwamba, muda umefika sasa kwa wasanii wa muziki na wadau wote kukaa chini na kukuna vichwa juu ya mwenendo mzima wa fani hii kwani kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiibuka na kuzua wasiwasi wa fani hii kudidimia na kukosa muelekeo kama jitihada za makusudi hazitafanyika.
Alihoji tabia inayokua kwa kasi ya baadhi ya wasanii wa kitanzania kunakiri vionjo (beats) vya miziki kutoka nje hasa Marekani na kuonyesha wasiwasi wa wasanii wetu kuja kuburuzwa mahakamani na hata kutozwa faini kubwa za fedha kutokana na kitendo hicho kukiuka sheria za kimataifa za hakimiliki na hakishirikishi.