Bob Marley atimiza miaka 40 tangu afariki Dunia
Ni miaka 40 tangu mwimbaji mashuhuri wa rege Bob Marley alipokufa na saratani huko Miami, akiwa na umri wa miaka 36, mnamo 11 Mei 1981.
Mwanamuziki huyo ni mmoja wa wasanii mashuhuri na wanaotambulika katika historia ya muziki, na vibao vikiwemo No Woman No Cry, One Love, na Redemption Song.
Kibao chake cha Buffalo Soldier kilikuwa kikubwa zaidi nchini Uingereza, na kufikia nambari nne mnamo Mei 1983.
Albamu ya 1977 Exodus iliitwa Albamu ya Karne na Jarida la Time.
Utotoni mwake kulikuwa na umasikini na hakuwa akiwasiliana na baba yake, afisa wa jeshi la majini ambaye alifanya kazi katika serikali ya Uingereza.
Aliondoka nyumbani akiwa na umri wa miaka 14 na kuendelea na kazi ya muziki huko Kingston.
Mnamo 1972, Marley aliwasili Uingereza na bendi yake ya The Wailers kufanya ziara na Johnny Nash kwa matumaini ya kuzindua taaluma yake ya kimataifa.
Mwaka uliofuata, Wailers walitoa albamu yao ya Catch a Fire na wakaanza kucheza kwenye televisheni ,BBC.
Uonekano huo ulileta athari kubwa na ukawapa hadhira pana nje ya msingi wa mashabiki wao wa jadi.
Baada ya ziara nyingine mnamo 1975, rekodi ya No Woman No Cry ya moja kwa moja huko The Lyceum, London, ilitolewa kama wimbo mmoja na ikampa Marley kibao chake cha kwanza Uingereza.
Mwimbaji huyo aalijikita katika muziki na akawa jina la kutambulika
Marley alikuwa anajulikana kwa imani yake ya Rastafarian, pamoja na mkewe, Rita, na dini hiyo ilionekana katika muziki wake.
Mwimbaji huyo pia alikuwa akipenda sana mpira wa miguu na alijulikana kwa kukaragaza ngozi kati ya vikao vya studio au kabla ya kupanda jukwaani.
“Ninapenda muziki kabla ya kupenda mpira wa miguu,” alisema kwenye mahojiano mnamo 1980.
“Kucheza mpira wa miguu na kuimba ni hatari kwa sababu mpira una vurugu sana. Ninaimba juu ya amani, upendo na vitu vyote hivyo, na kitu kinaweza kutokea.
“Mtu akikukabili kwa mabavu huleta hisia za vita.”
Onyesho la mwisho la moja kwa moja la Marley nchini Uingereza lilikuwa mnamo 13 Julai 1980 huko New Bingley Hall, Stafford.
Marley alikufa mwaka uliofuata kwa sababu ya ugonjwa wa melanoma ya acral lentiginous, baada ya kugunduliwa kuwa nao mnamo 1977. Alizikwa mahali pake pa kuzaliwa Jamaica katika kijiji cha Nine Mile.