Bongo5 ExclusivesBurudani

Breaking: Jose Chameleone aandamana Ubalozi wa Tanzania kudai Passport yake kwa Eric Shigongo!

Msanii Jose Chameleone leo asubuhi aliamua kuwachukua vijana wake wa Leone Island Crew na kuandamana nao mpaka Ubalozi wa Tanzania jijini Kampala ambapo aliweka kambi ya kudai Passport yake nje ya Ubalozi huo baada ya kuchoshwa na hatua dhaifu zilizochukuliwa baada ya yeye kwenda kulalamikkia kitendo cha Passport yake kuwa inashikiliwa na mkurugenzi wa Global Publishers Eric Shigongo baada ya kufanya shoo uwanja mkuu wa taifa jijini Dar-Es-Salaam siku ya tarehe 7 katika tamasha la Matumaini.

Kwa mujibu wa Chameleone mwenyewe kama unavyoona kwenye picha hizi anasema aliamua kuchukua uamuzi huo wa kuandamana mpaka ubalozini baada ya kuona kwamba hakuna msaada wa maana anaoupata kutoka kwa viongozi wa Ubalozi huo ambao yeye anasema walikuwa hawalipi kipaumbele cha kutosha suala lake huku Passport yake ikiwa inashikiliwa na bwana Shigongo.

Sakata hili ni mwendelezo wa habari ambayo tuliitoa tarehe 9 July mwaka huu baada ya Chameleone kulizungumzia suala hili siku ya tarehe 8 usiku kabla ya kuondoka na kurudi kwao kwa kutumia hati ya dharura na kurudi tena wiki moja baadae lakini wakati huo ilikuwa Zanzibar ambapo alialikwa kupiga shoo katika tamasha la Ziff.

Kama tulivyoandika mwanzo kwa mujibu wa Chameleone yeye anasema Eric Shigongo alichukua Passport yake pamoja na wenzake wawili aliokuwa ameambatana nao kwa kutumia mfanyakazi wake katika hoteli ya Atriums ambako alikuwa amefikia.

Tunamnukuu “ Wakati nina check out mimi na wenzangu dada mmoja ambaye ni mfanyakazi katika hoteli tuliyofikia ya Atriums alitufuata na kutuambia anaomba Passport zetu ili azitoe kopi mimi sikuwa na wasiwasi kwani alisema hii ni kwa ajili ya kama kuna mtu atatusumbua uwanja wa ndege, eeh, kumbe mambo yalikuwa tofauti baada ya hapo ujumbe uliofuata ni kwamba Eric shigongo anasema hatupi Passport zetu mpaka hapo tutakapompatia dola 3500 alizotapeliwa na mtu aliyejifanya meneja wangu”. alisema Chameleone.

Sakata hilo halikuishia hapo kwani Chameleone anasema yeye alienda kwanza polisi kuripoti alafu akaenda Ubalozi wa Uganda nchini Tanzania na kuwapa taarifa ya tukio hilo la kuzuiliwa kwa Pasi yake na za wenzake wawili.

Anasema alipewa hati ya dharura ya kusafiria na kuambiwa akifika aanze kufuatilia kupitia polisi wa kimataifa Interpol na ubalozi wa Tanzania nchini Uganda. Kwa maelezo yake anasema ilibidi aingie mtaani kumsaka huyo tapeli anayejifanya ni meneja wake na kufanikiwa kumtia mbaroni kijana tapeli anayeitwa George na kumfikisha kituo cha kati cha Kampala lakini kwa mshangao tapeli huyo alipewa dhamana na kuachiwa kitu kilichomfanya apagawe zaidi kwani bila pasi yake hawezi kupiga shoo ambazo anazo Uingereza, Belgium, Norway, Sweden, south Africa, Malawi na Canada.

Anasema hasira hizo ndizo zilizomsukuma kuamua kwenda ubalozi wa Tanzania jijini Kampala ili kupata msaada wa haraka ambapo nako akaona mambo yanakwenda Valu Valu kwani maafisa katika ubalozi huo hawakumpa ushirikiano wa kutosha hivyo kuamua leo iwe siku maalumu ya kwenda kukesha ubalozini mapaka kieleweke.

Mpaka tunapoandika habari hii Chameleone na vijana wa kundi lake la Leone Island Crew walikuwa wamepelekwa kwa mkuu wa Polisi Uganda Meja jenerali Kale Kaihura na kufanya nae maongezi ambayo anasema yamesaidia kutatua mgogogro uliopo kati yake na Eric Shigongo na kwamba habari ambayo imeingia hivi punde ni kwamba Passport ya Chameleone na wenzake iko njiani kuelekea kampala na imepelekwa na mmoja wa maofisa wa Ubalozi wa Uganda.

Kwa sasa Chameleone anasubiri kukabiziwa pasi yake na anatarajiwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari ili kutoa tathmini ya tukio hilo.

Kabla ya tukio hili Bongo5 ilikutana na Jose Chameleone Zanzibar na aliacha ujumbe mzito kwa Eric Shigongo lakini tulipojaribu kuongea nao walisema tusubiri kauli kutoka kwao ambayo nafikiri ni busara wakaitoa.

Bongo5 itakuletea habari kadri tutakavyozipata

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents