Habari

Dereva, mke wa Tundu Lissu wanena mazito ‘Watanzania wote wanajua’

Mke wa Mbunge wa Singida Masharaiki, Mhe Tundu Lissu, Bi. Alicia Magabe amefunguka juu ya tukio la mumewe kupigwa risasi kwa kudokeza kwamba tukio hilo haliwezi kuwa limetokana na sababu nyingine isipokuwa kazi ambazo amekuwa akizifanya.

Mke wa Mhe Lissu, Bi Alicia Magabe wa kwanza kulia.

Bi Alicia amezungumzia pia kuhusu afya yake na kueleza kuwa bado sio nzuri na kuwaomba Watanzania waendelee kumuombea.

Watanzania wote wanajua Lissu maisha yake yote amekuwa ni mtetezi wa wanyonge na tukio hili amelipata kutokana na kazi zake hizo hivyo nawaomba tumuombee tu,“amesema Bi Alicia huku akiwaomba watanzania wasichoke kumuombea Mhe. Lissu “Ninachoweza kusema hali ya mheshimiwa Lissu sio nzuri ingawa ni tofauti na tulivyomleta hapa, hivyo naomba Watanzania kuendelea kumuombea.

Kuhusu kauli ya Serikali kwamba ipo tayari kugharamia matibabu ya Lissu popote ikiwa itaombwa na familia hiyo, Alicia ambaye pia ni wakili amesema kwa sasa hana maoni yoyote.

“Katika hili no comment (sina maoni) ndio tumesikia jana amezungumza na kwa kuwa jambo hili siyo la uamuzi wa mtu mmoja, mimi sina cha kusema,” amesema Alicia.

Hata hivyo, Bi Alicia amewashukuru Watanzania kwa michango na maombi yao kwa Mhe. Lissu akisema hiyo inaonyesha ni jinsi gani wanathamini mchango wake kwa jamii.

Kwa upande mwingine, mbali na Alicia dereva wa Tundu Lissu ambaye ndiye mtu pekee waliyekuwa wote siku ya tukio hilo, Simon Bakari amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu tukio hilo na kudokeza kwamba amevurugwa na hana kumbukumbu sahihi.

“Kwa sasa siwezi kuzungumza vizuri tukio hili kwani nadhani sina kumbukumbu vizuri.”amesema Simon Bakari ambaye yupo nchini Kenya kwa matibabu ya kisaikolojia.

Alipoulizwa kuhusu wito wa polisi wa kwenda kutoa maelezo, amesema atafanya hivyo pindi atakaporejea nchini baada ya matibabu,“Nilisikia polisi wamenitaka nikatoe maelezo lakini sijisikii vizuri na bado napata matibabu. Nitakwenda.”

Chanzo:Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents