Michezo

Farid: Siyo kweli kuwa Azam FC ilikuwa inanibania kwenda Hispania

Mchezaji wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid Mussa, ameweka wazi kuwa mabingwa hao hawajambania kwenda nchini Hispania kucheza soka la kulipwa kama ilivyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari.


Farid Mussa wakati akiongea na waandishi wa habari

Kwa kuudhihirishia umma, Mussa amejitokeza hadharani na kupinga madai hayo akidai kuwa muda wowote kuanzia sasa atakwenda nchini humo kujiunga na Club Deportivo Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza baada ya kupata ‘Visa’ maalumu ya kuingia nchini akiwa kama mfanyakazi.

“Kwanza napenda kumshukuru Mungu baada ya kupata visa, haikuwa kazi rahisi namshukuru Meneja Mkuu Abdul (Mohamed) kapigania hadi suala hili limekamilika, cha kwanza nilikuwa ninawaomba Watanzania wajue kuwa Azam haikuwa inanibania ni masuala tu ya visa yalikuwa yakisumbua ubalozini.

“Mara baada ya kupata visa ya kufanya kazi muda wowote ninaweza kuondoka kuanzia Januari,” alisema Farid wakati akizungumza mbele ya waandishi wa habari wakati wa zoezi la kutambulishwa wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo.

Taarifa hizo zilianza kutolewa kwenye vyombo vya habari, kufuatia suala la Farid kwenda Hispania kuwa kimya lakini ukweli wa mambo ni kuwa visa hiyo ndio iliyokuwa ikikwamisha dili hilo.

Naye Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, akitolea ufafanuzi suala hilo alisema kuwa lengo la uongozi huo lilikuwa ni kinda huyo kuondoka mapema kuelekea nchini humo, lakini suala kubwa lilikwamisha ni visa hiyo ya kufanya kazi nchini Hispania.

“Uongozi wa Azam FC ulikuwa sambamba na Tenerife kuhakikisha Farid anaondoka, lakini tunashukuru suala hilo limekamilika kwa asilimia 98, lakini ni kwamba Farid muda wowote kuanzia sasa Mungu akijaalia ndani ya wiki mbili zijazo au wiki moja anaweza kuondoka kutoka Tanzania kuelekea Hispania,” alisema.

Azam FC inaamini ya kuwa kuondoka kwa nyota huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kutafungua milango kwa wachezaji wengine ndani ya timu hiyo na Taifa kwa ujumla kuweza kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents