Illuminata amrithi Odemba

Illuminata amrithi Odemba
Mlimbwende Illuminata James kutoka mkoani Mwanza, juzi usiku alitwaa
taji la Miss Universe Tanzania kwa mwaka huu na kujikatia tiketi ya
kuliwakilisha taifa katika michuano ya dunia itakayofanyika baadaye
mwaka huu katika visiwa vya Bahamas. Illuminata ambaye anapokea taji
hilo kutoka kwa mwanadada nyota katika fani ya mitindo nchini, Miriam
Odemba, alitwaa taji hilo baada ya kuwashinda walimbwende wenzake 19

Shindano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City Dar es
Salaam, mbali ya mashabiki wa masuala ya ulimbwende kupata burudani ya
kuonyeshwa mavazi na miondoko ya ‘catwalk’ kutoka kwa washiriki 20, pia
walikongwa nyoyo zao na burudani safi ya muziki kutoka kwa msanii nyota
wa Bongofleva, Ambwene Yesaya ‘Mzee wa Commercial’ na mwanadada Wahu
kutoka Kenya anayetamba na wimbo wa ‘Sweet Love’. Burudani nyingine
ilitoka kwa bendi ya Diamond Musica chini ya Allaine Mulumba walioingia
na wimbo wao maarufu wa ‘Mapenzi kitu gani’ na kufuatiwa na sebene la
uhakika. Ngoma za utamaduni kutoka kikundi cha Albino Revolution
Cultural Troupe kilihitimisha burudani.

Mbali na Illuminata, washindi wengine katika fainali hizo za Miss
Universe Tanzania zilizohusisha warembo kutoka mikoa mitano ya Arusha,
Mwanza, Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam, walikuwa ni Evelyne Almasi
aliyeshika nafasi ya pili na hivyo kujipatia nafasi ya kushiriki
shindano la Miss Earth. Hidaya Maeda aliyeshika nafasi ya tatu
ataliwakilisha taifa katika shindano la Miss International baadaye
mwaka huu, na nafasi ya nne ilikwenda kwa Zainab Kianda na Gisela
Tarimo alikuwa wa tano.

Miss Universe Tanzania 2009 mbali ya kujipatia tiketi ya kushiriki
shindano la dunia, pia alizawadiwa Sh milioni tatu, nafasi ya kusoma
kozi ya lugha ya Kifaransa kwa mwaka mmoja katika kituo cha Alliance
Francaise pamoja na kupatiwa vipodozi vyenye thamani ya Sh 500,000
kutoka duka la Shear Illusion. Majaji wa shindano hilo walikuwa ni
Mbunge wa Viti Maalumu, Al Shaymaa Kwegyir (CCM), wanamuziki John
Kitime, msanii Masoud Kipanya, Mbunifu wa mavazi Ally Rhemtullah, Maria
Sarungi Tsehai, Amit Patel kutoka kwa wadhamini wa shindano hilo
Kampuni ya Samsung na Jaji Mkuu alikuwa Rosie Motene kutoka Afrika
Kusini. Motene ni mwigizaji nyota na mtangazaji wa Kituo cha Studio 53.

Shindano hilo lilianza kwa washiriki wote 20 kupita jukwaani katika
mavazi mbalimbali yakiwamo ya ubunifu na jioni yaliyotengenezwa na
wabunifu mbalimbali wa nchini na baadaye kufuatiwa na kutangazwa
washiriki bora 10 ambao nao walichujwa na kubakia watano bora.
Washiriki waliofuzu hatua ya tano bora walikuwa ni Gisela Tarimo,
Evelyne Almasi, Zainab Kianda, Illuminata James na Hidaya Maeda ambao
waliingia kwenye hatua ya maswali na majibu wakijibu maswali kutoka kwa
majaji wa shindano hilo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents