Watu 10 wafariki Zanzibar

Watu 10 wafariki Zanzibar
Kikosi cha wazamiaji wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kimeopoa maiti tatu na
kuziona nyingine nne zikiwa zinaelea na hivyo kufanya idadi ya miili ya
watu waliofariki katika ajali ya boti ya Mv. Fatih inayomilikiwa na
kampuni ya Seagul, kufikia kumi.

Kikosi hicho kiliwasili jana kutoka jijini Dar es Salaam kwa lengo la
kuongeza nguvu kwa kushirikiana na wazamiaji 30 kutoka Kikosi Maalum
cha Kuzuia Magendo (KMKM) katika kuokoa watu kwenye ajali hiyo
iliyotokea Ijumaa majira ya saa 3:30 usiku.

Awali kulikuwa na maiti tatu zilizoopolewa na habari zinasema maiti tatu zilizoopolewa jana zilipatikana ndani ya boti.

Maiti zilizopatikana jana ni za Ashura Suleiman Mtege na watoto wawili Ali Haroub Mohammed, 3, na Mukrim Mohammed, 6.

Maiti ya mama iliyopatikana jana ilikutwa ikiwa na mtoto aliyemfunga
mbeleko. Mtoto huyo anakisiwa kuwa na umri wa miaka mitatu. Watu
waliokuwepo kwenye Bandari ya Malindi kushuhudia uokoaji, walionekana
kuongezeka majonzi baada ya kushushwa kwa maiti ya mama huyo na mtoto
wake.

Maiti hizo tatu zilipelekwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kuhifadhiwa.

Wataalamu wa bandarini wanasema huenda kukawa na maiti zaidi ndani ya
boti hiyo. Habari zilizopatikana jana jioni zinasema kuwa kuna maiti
nne zaidi zimeonekana, lakini bado hazijatolewa kutokana na kazi ya
uokoaji kufanyika katika mazingira magumu.

Awali viongozi mbalimbali, akiwemo naibu waziri kiongozi wa Zanzibar,
Ali Juma Shamhuna walifanya ziara kwenye Bandari ya Malindi na kupata
maelezo halisi juu ya tukio hilo kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika la
Bandari Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma aliwaambia
waandishi wa habari kwamba, matukio ya wizi yaliyotokea baada ya ajali
hiyo. Alisema polisi wamefanikiwa kuyadhibiti na hivi sasa
watahakikisha mali inayotolewa katika meli hiyo haingii katika mikono
ya wahalifu na ulinzi mkali umewekwa bandarini.

Alisema kulikuwa na wizi mkubwa baada ya ajali hiyo kwa kuwa baadhi ya
watu waliojifanya kutoa msaada, walitumia fursa hiyo kufanya uhalifu na
kuondoka na vitu mbalimbali vilivyokuwa vimepatikana katika boti hiyo
vilivyokuwa vikielea majini.

Juma alisema polisi imefanikiwa kuwakamata baadhi ya watu ingawa hakutaja idadi.

Miongoni mwa vitu ambavyo vimekuwa vikiibwa ni magunia ya bidhaa kama
vitunguu, viazi, nyaya, juisi na magodoro na baadhi ya watu walioiba
walibambwa na polisi maeneo ya Kizingo na Mji Mkongwe.

Baadhi ya bidhaa hizo zilikuwa zikiuzwa kwa bei poa katika mitaa mbalimbali.

Aidha Waziri Juma alisema katika kuchukua hatua zaidi za kutafuta
chanzo cha ajali hiyo baada ya kuwapo maelezo yanayotatanisha katika
vyombo vya habari, wameitaka kamati ya ulinzi na usalama kulifanyia
uchunguzi suala hilo.

Kauli ya waziri huyo inakuja baada ya kuwapo kwa madai kuwa chanzo cha
ajali hiyo huenda kikawa ni kutoelewana kati ya viongozi wa Shirika la
Bandari na nahodha wa meli hiyo baada ya kutoa taarifa ya kutaka
kushusha abiria maeneo yasiyo rasmi.

Taarifa za awali zinasema uzembe wa Shirika la Bandari la Zanzibar ndio
uliosababisha ajali hiyo kwa kuwa nahodha, Ussi Ali alipiga simu na
kuwaeleza udhaifu wa meli hiyo wakati ikiwa njiani na kutaka kusimama
eneo la Chumbe, lakini uongozi wa Bandari ulikataa na kumtaka nahodha
huyo kwenda hadi Bandari ya Malindi.

Waziri Hamza alifahamisha kuwa hadi sasa serikali bado inafanya
uchunguzi na vikosi vya ulinzi na usalama vimetakiwa kuzifanyia
uchunguzi taarifa hizo ili kupata ukweli na baadaye serikali itatoa
kauli yake.

Waziri huyo alifahamisha kuwa madai ya ubovu wa chombo hicho, ambayo
pia yalitolewa na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ni
miongoni mwa mambo ambayo yanafanyiwa uchunguzi na kamati hiyo kwa vile
mmiliki wa meli hiyo alieleza kuwa ni mpya.

Alisema wataliangalia hilo kwani hawafahamu kama kulikuwa na mazingira ya rushwa katika usajili wa chombo hicho.

"Mazingira ya ruswa ni vigumu kuyatambua sasa kama kulikuwa na hilo
katika usajili sisi tutaliangalia kwani huyu mmiliki alisema boti yao
ni mpya," alisema waziri huyo.

Hadi tunakwenda mitamboni bado maombi ya tangi Kutoka Shirika la
Bandari la Dar es Salaam ambayo ilionekana kuwa itaweza kusaidia kazi
ya uokoaji huo haijaweza kufika katika Bandari ya Malindi Zanzibar.

Mkurugenzi wa kitengo cha maafa nchini, Bakari Shaaban alisema Serikali
ya Muungano itaangalia namna ya kushiriki katika kusaidia ajali hiyo
kwa kuwa taarifa za tukio hilo ziliwasilishwa kwa viongozi wakuu wa
nchi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents