Akizungumza na vyombo vya habari, Mwanasheria Mkuu wa Marekani Merrick Garland amemtaja mshukiwa huyo kuwa ni Jack Teixeira, mfanyakazi katika jeshi la anga la walinzi wa taifa na kiongozi wa kundi la mtandaoni ambako hati hizo zilivujishwa kwa mara ya kwanza.
Kukamatwa kwake kulikotangazwa moja kwa moja na Televisheni, kunafuatia kukamilika kwa uchunguzi wa wiki nzima uliochochewa na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani katika mojawapo ya uvujaji mbaya zaidi wa taarifa za siri tangu sakata la Edward Snowden mwaka 2013.
Ofisi ya jeshi la anga la walinzi wa taifa la Marekani imesema kuwa Teixeira alijiunga mwaka 2019 na alikuwa ni mtaalamu wa Tehama ambaye alikuwa amefikia kiwango cha wafanyakazi wa daraja la kwanza.
Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon ilikuwa imesema kuwa kuvuja kwa taarifa hizo kunatoa “hatari kubwa” kwa usalama wa taifa wa nchi hiyo.
Tukio hilo la aibu la kuvuja kwa nyaraka nyeti za kiusalama zinazohusisha wasiwasi wa Marekani juu ya uwezekano wa uvamizi wa vikosi vya Kyiv dhidi ya wanajeshi wa Urusi, ulinzi wa anga wa Ukraine lakini pia inahusisha Marekani kuwachunguza washirika wake ikiwemo Israeli na Korea Kusini.
Nyaraka zingine ni pamoja na tathmini kwamba Ufaransa inawezekana ikashindwa kufikia malengo ya kiusalama katika kanda ya Afrika Magharibi na kati.