Habari

Kombora la Israel laipiga Iran

Kombora la Israel limeipiga Iran, maafisa wa Marekani wamekiambia kituo mshirika wa BBC CBS News.

Milipuko ilisikika katika jimbo la kati la Isfahan na safari za ndege zimesitishwa katika miji kadhaa, vyombo vya habari vya Iran vinasema.

Iran iko katika hali ya tahadhari baada ya Israel kusema kuwa itajibu shambulizi la Iran dhidi yake Jumamosi usiku.

Iran ilirusha zaidi ya ndege zisizo na rubani 300 na makombora katika shambulio lake la kwanza kabisa la moja kwa moja dhidi ya Israel.

Takriban yote yalinaswa na ulinzi wa anga wa Israel kwa msaada kutoka Marekani, Uingereza na washirika wengine.

Shambulio hilo la Iran lilikuwa la kulipiza kisasi shambulio la Israel lililoua makamanda wakuu wa Iran nchini Syria tarehe 1 Aprili.

Mkoa wa Isfahan ni nyumbani kwa kituo kikubwa cha anga, eneo kubwa la uzalishaji wa makombora na maeneo kadhaa ya nyuklia.

Shirika la habari la Iran la Fars linasema milipuko imesikika karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Isfahan na kambi ya jeshi katika mji wa Isfahan, na kuamsha mifumo ya ulinzi wa anga ya ndani.

Video kutoka kwa Isfahan iliyochapishwa kwenye akaunti ya Instagram ya BBC Persian inaonyesha mwanga wa rangi ya chungwa angani usiku na sauti ya kile kinachoonekana kama milipuko ya moto wa kutungua ndege.

Katika siku za hivi karibuni, viongozi wa Iran walikuwa wameonya kwamba shambulio lolote la Israeli dhidi ya Irani lingesababisha majibu ya haraka. Kumekuwa na majaribio kati ya jumuiya ya kimataifa ili kupunguza mzozo huo, kwa wito wa kujizuia.

Siku ya Alhamisi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema kumekuwa na “kuongezeka kwa hatari” kati ya Israel na Iran.

” Kosa moja, linaweza kusababisha jambo lisilofikirika – mzozo kamili wa kikanda ambao ungekuwa mbaya kwa wote wanaohusika,” aliambia Baraza la Usalama.

Haya yanajiri siku sita baada ya Iran kufanya shambulizi ambalo halijawahi kushuhudiwa kulipiza kisasi shambulio la anga la Israel kwenye jengo la ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria tarehe 1 Aprili, ambalo liliua majenerali wawili wakuu.

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Zahedi ndiye aliyekuwa mkuu wa operesheni za kijeshi za Iran nchini Syria na Lebanon ambapo vikosi vinavyoiunga mkono Iran vimeanzisha mashambulizi dhidi ya Israel.

Takriban ndege zisizo na rubani za Iran na makombora ya baharini na ya balistiki yalinaswa na ulinzi wa anga wa Israel kwa msaada wa Marekani, Uingereza na washirika wengine, jeshi la Israel lilisema.

Makombora kadhaa ya balistiki yalipiga kambi ya anga katika jangwa la Negev. Msichana mdogo wa Bedouin, ambaye aliumia sana kwa kuangukiwa na makombora, ndiye pekee aliyeripotiwa kuumia.

Credit: BBC Swahili.

Imeandikwa na Mbanga B.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents