Lifahamu Elani: Kundi la Kenya linalotikisa kwa nyimbo zenye utunzi wa Kiswahili fasaha
Pamoja na kuanzishwa miaka kadhaa iliyopita, nimelifahamu kundi la Elani la Kenya kupitia wimbo wake uitwao Milele.
Utunzi, uandishi na sauti za wimbo huo, vilinifanya niusikilize mara nyingi na kwa makini zaidi kwakuwa nilisikia kitu kipya kutoka Kenya ambacho kwa muda mrefu sijawahi kusikia.
Nilivutiwa na namna ambavyo utunzi wao umetumia Kiswahili fasaha kuliko nyimbo nyingi za Kenya ninazozifahamu. Kwa sifa hizo kwa sasa Elani kwangu ndio kundi bora zaidi Afrika Mashariki.
Siwezi kuacha kuusifia urembo wa wasichana wawili wanaounda kundi hilo, Wambui Ngugi na Maureen Kunga.
Elani linaundwa na vijana watatu. Pamoja na Wambui na Maureen, yupo pia Bryan Chweya. Watatu hawa walikutana Alliance Française mwaka 2008 na haraka wakawa marafiki.
Haikuwa muda mrefu hadi walipogundua kuwa wote walikuwa wanapenda kufanya muziki na ndipo kundi la Elani likaanzishwa.
Elani ni neno la Giriama linalomaanisha mwanga. Wanasema wanataka kuwa mwanga wa dunia kupitia muziki wao.
Pamoja na muziki, Muthoni alisomea sheria kwenye chuo kikuu cha Nairobi, Wambui alisomea Actuarial Science kwenye chuo hicho pia na Bryan alisomea sheria.
December 6 kundi hilo liliachia album yake ya kwanza iitwayo “Barua ya Dunia” ikiwa na nyimbo kama Milele, Jana Usiku, Kuku, Barua, Zuzu, Peperuka na zingine.