Bongo5 Makala

Makala: Professor Jay umesoma vema kitabu cha Eto’o na Messi

“We ndio wangu wife material, uzuri na tabia zinafuta changu kilio, ado ado mambo bado wape kisago mtoto upo kamili gado”. Hii mistari inayopatikana katika wimbo wa Professor Jay ‘Kamili Gado’ uliotoka mwaka 2012.

Professor Jay ambaye weekend iliyopita alifunga pingu za maisha na mchumba wake wa siku nyingi, alikuwa anataka kufikisha ujumbe kwa mwanamke ambaye alikuwa anaamini kwake ni wife material. Bila shaka mwanamke huyo ni Grace Mgonjo ambaye kwa pamoja walikubali kula kiapo cha kuishi pamoja hadi pale kifo kitakapo watenganisha.

Professor amebainisha kuwa wamedumu katika uchumba kwa kipindi cha zaidi ya miaka 13. Kipindi hiki kirefu cha zaidi ya siku 4,745 ni sawa idadi ya kurasa za kitabu cha Professor kwa sasa ambacho kimebeba ujumbe nzuri kwa vijana wakike na wakiume ambao bado hawajaingia katika ndoa.

Kitabu hiki kinaeleza licha ya hatua hiyo aliyofikia kuna changamoto lukuki alizopitia, ilifika hata wakati wakatengana na mchumba wake lakini baadae wakaja kukaa na kumaliza tofauti zao, huenda kila mmoja alipata picha halisi wapi watakuwa siku ya leo.

Ukurasa wa mwanzo ni kabla hata ya Professor Jay hajapata umaarufu mkubwa alionao kwa sasa, ni kabla hata hajatoa albamu ya J. O. S. E. P. H (2006) na  Aluta Continua (2008), ni kabla ya kushinda tuzo kadhaa za Kill Music, BBC, Radio One Awards (2006), na kubwa zaidi ni kabla ya kushinda kiti cha ubunge (2015). Lakini Bi. Grace aliamua kupambana na kitabu hiki kuanzia ukurasa wa mwanzo hadi sasa akiwa ukurasa wa 4,745 na zaidi, pongezi kwake.

Katika hili kunahitaji uvumilivu mkubwa wa pande zote, kwa yule anayeandika na yule msomaji. Wakati tunasoma kitabu hiki alichoandika Professor Jay na kujifunza mambo mengi, huenda na yeye alisoma katika vitabu vya wachezaji wenye historia kubwa duniani, Samuel Eto’o na Lionel Messi ambao nao tuna mengi ya kujifunza katika maisha yao ya utafutaji, kazi, umaarufu na hadi ndoa.

Karibu Eto’o na Messi

 Moja ya maneno yenye busara yaliyonukuliwa kutoka kwa Elbert Hubbard yanasema, “mara nyingi maisha huja kupitia upendo wa kipekee”. Hii ina maana palipo na mapenzi ya kweli ndipo maisha yalipo, na kama utayakosa basi umekosa maisha, kanuni ambayo aliiamini Leo Buscaglia.

Eto’o na mkewe walipohudhuria harusi ya Messi

Mwaka 1997 Samuel Eto’o raia wa Cameroon akiwa na umri mdogo wa chini ya miaka 18 alifunga safari hadi nchini Hispania kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klab ya Real Madrid.

Baada ya kupitia msoto mkali katika klab za Real Madrid B alipoanzia, Leganes, Espanyol, Real Mallorca ambayo ndio timu ya kwanza kumsajili rasmi kwa kwa pauni milioni 4.4, mwaka 2004 Barcelona walimsaji kwa dau la euro milioni 24, hapo ndipo alipong’aa na ulimwengu mzima kumjua.

Eto’o alipata mafanikio makubwa ndani ya Barcelona na kuweka rekodi nyingi Ulaya na Afrika. Baada ya kuondoka Barcelona na kwenda Anzhi Makhachkala ya Urusi alikuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa kuliko wote dunia akiwazidi hata Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Katika mafanikio hayo makubwa ya Eto’o kuna mwanamke aliyekuwa nyuma yake toka mwanzo kabisa, ambaye alijitolea kupigana kwa kila hali hadi pale kitabu chenye kubeba historia ya mafanikio ya Eto’o kikamilike kuandikwa, pia jina lake liwepo.

Georgette na Eto’o siku ya harusi yao

Georgette Tra Lou ambaye ni mke wa Eto’o kwa sasa alikuwa nae tangu akiwa mchezaji chipukizi wakati akicheza soka la mtaani nchini Ufaransa. Eto’o alieleza kuwa wakati huo alikuwa hana kitu chochote na mpenzi wake ndiye alikuwa akigharamia kila kitu kwa fedha ambazo alikuwa akizipata katika saloon aliyokuwa akiimiliki.

“Georgette alinivumilia kwa mambo mengi na kunipa moyo wa kujituma zaidi, leo hii ni mke wa mchezaji tajiri Afrika, kwa pamoja tuna zaidi ya euro milioni 100 katika akaunti zetu Bank, nina furaha kumuoa mwanamke mvumilivu” alieleza Eto’o.

Baada kipindi kirefu cha uchumba mwaka jana walifunga ndoa nchini Italy na kuhudhuriwa na wachezaji kadhaa wa zamani wa Barcelona.

Tumsome Messi kidogo

Wiki kadhaa zilizopita mchezaji huyu raia wa Argentina wenye historia kubwa alimuoa mpenzi wake ambaye wamekuwa wote tangu utotoni. Harusi hiyo kati ya Messi mwenye umri wa miaka 30 na Antonela Rocuzzo mwenye umri wa miaka 29, inatajwa kuwa harusi ya karne.

Messi na Rocuzzo walikutana wakiwa watoto wa miaka 13 kabla ya yeye kuelekea kuchaza soka nchini Uhispania, licha kupata mafanikio makubwa na umaarufu bado moyo wake ulitulia kwa Rocuzzo. Pegine Rocuzzo alishawishika kuwa mtu mwingine lakini aliamini katika penzi lake na kutanguliza uvumilivu mbele.

Wamekuwa pamoja kwa kipindi cha miaka 17, Rocuzzo aliamua kuwa kipofu asimuone mwanaume mwingine zaidi ya Messi, leo hii anafurahia maisha ya ndoa wakati mumewe akilipwa kati ya £500,000/€565,000 kwa wiki, kiasi ambacho wachezaji wawili tu ndio hupokea £500,000 kwa wiki, ambao ni Carlos Tevez and Ezequiel Lavezzi wanaocheza Chinese Super League.

Bila uvumilivu na kuamini katika penzi lake yote haya yangekuwa kama simulizi zenye kusisimua masikioni mwa Rocuzzo.

Turudi kwa Professor Jay

Tumesoma kwa makini stori mbili za Eto’o na Messi, ukilinganisha na ile ya Professor Jay kuna vitu vinashabiana kwa kiasi kikubwa isipokuwa mazingira. Messi, Eto’o na Professor Jay walipambana kwa kila hali kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri ya kiuchumi pindi wanapoingia katika maisha ya ndoa.

Wakati huo Rocuzzo, Georgette na Grance waliwavumilia wapenzi wao na kuwatia moyo katika kile walichokuwa wakikipigania. Hiki ni kitu cha msingi na jambo lilokuu zaidi.

Siku zilizopita kitambo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) lilifanya mahojiano na baadhi ya wazazi nchini Somalia. Wazazi hao walieleza jinsi vijana wao wengi wanapokimbilia barani Ulaya kutafuta maisha, kikubwa kilichotajwa ni kwamba vijana wengi wanaenda kutafuta fedha kwa ajili ya kuoa.

Inaelezwa kuwa kwenye baadhi ya jamii nchini Somalia suala la kuoa limefanywa kuwa kitu ghali zaidi kiasi kwamba vijana wasio na fedha husindwa kuoa. Mantiki ya simulizi hii ni kwamba hadi unapoona watu wanafikia hatua ya kufunga ndoa kuna jitihada zinazopaswa kuheshimiwa na uaminifu wa kusujudiwa. Tumsimame hapo.

Muziki wake ni mahaba tosha

Nimekuwa mfuatiliaji wa muziki wa Professor kwa kipindi kirefu sasa, licha ya kuandika mashairi mazuri katika upande wa siasa, pia katika mapenzi ni mtunzi mzuri na vile anavyoimba vipo katika maisha yake.

Nikisikiliza wimbo wake ‘Niamini’ aliomshirikisha Lady Jadee kuna ujumbe wa kusisimua unaopatikana ndani yake, ujumbe utakao kusafirisha kihisia na kukupeleka katika ulimwengu wa kusadikika.

Professor Jay anasema, “ona wanasangaa kuona penzi halichuji, ndio maana wanatunga uongo kwa makusudi”, kisha sauti nzuri Binti Komando ‘Jide’ inamliwaza kwa kumueleza kuwa, “wengi walifurahi pindi tulipogombana, weka masikio pamba ili tusiwape mwanya,”.

Bado Professor Jay anaendelea kutoa ya moyoni kwa kusema, “kila nikikosea nafsi yangu inanisuta, kweli nakiri kwako siwezi kufurukuta”, Jide naye anajibu, “ni mapenzi gani yasiyo na mikwaruzo, upendo na nidhamu ya kweli hiyo kwetu ni nguzo”. Nikisiliza hii mistari ni sawa na kusikiliza hit songs kadhaa za Whitney Houston kama My Love Is Your Love, I Will Always Love You na Saving All My Love For You

Lady Jaydee akitoa burudani katika harusi ya Professor Jay

Asante Professor Jay kwa kukisoma vema kitabu cha Eto’o na Messi, kisha kuandika chako ambacho tunakisoma kwa sasa. Unazidi kujenga nguvu ya ushawishi kwa vijana, wasanii wenzako na wanasiasa pia, kweli kitabu kipo KAMILI GADO.

By Peter Akaro

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents