Mali: Mwanajeshi mmoja atiwa mbaroni baada ya uzinduzi wa Kitabu
Mwanajeshi mmoja mwenye Cheo cha Kanali katika jeshi la Mali ametiwa mbaroni kutokana na kitabu chake kilichozinduliwa hivi karibuni, ambacho kilikuwa na madai kuwa jeshi limefanya ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia.
Katika kitabu hicho chenye kurasa 400 chenye Kichwa cha Mali: ‘Changamoto ya Ugaidi katika Afrika’, Kanali Alpha Yaya Sangare, akinukuu mashirika ya haki za binadamu aliandika. “Tangu 2016, FDS (Vikosi vya Ulinzi na Usalama) vimejihusisha na unyanyasaji dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuwa sehemu ya makundi ya kigaidi”.
Aliongeza kuwa Wanajeshi walifanya unyanyasaji huo kwa Ushirikiano na Uongozi wa Kijeshi.
Bw. Sangare alikamatwa Jumamosi jioni, lakini kukamatwa kwake kulithibitishwa na Familia yake Jioni ya siku ya Jumapili.
Waziri wa Ulinzi wa Mali Ijumaa iliyopita ilishutumu madai hayo yaliyochapishwa katika kitabu hicho, na kuyataja kuwa ya “Uongo”.
Mashirika kadhaa ya Kimataifa ya Kutetea Haki za Binadamu yameshutumu Wanajeshi wa Mali kwa Kuwadhulumu na kuwanyonga Raia katika mapambano yao dhidi ya Waasi wa Kiislamu.
Chanzo: Voa Swahili
Imeandikwa na Mbanga B.