Burudani

Mashabiki msitengeneze bifu isiyo ya lazima kati ya Wizkid na Alikiba

Ushabiki ni mzuri kufurahia, ni mzuri kupongezana, lakini pale unapoingiza matusi, hakika matokeo yake ni mabaya siku zote.

wiz-na-ali

Ama pengine ushabiki kimuziki tulionao Tanzania, ubaki kuwa wa kurushiana matusi tu ndani kwa ndani na usihusishe wasanii wa nje ambao timu zetu hazihusiani nao asilani.

Ninasikitishwa sana na ninachokiona kwenye ukurasa wa Instagram wa Wizkid baada ya kubainika kuwa tuzo ya MTV EMA aliyokuwa ameshinda awali itachukuliwa na atapewa Alikiba – ambaye kwa mujibu wa kura ndiye aliyestahili kushinda. Hiyo imekuwa habari njema kwa mashabiki wa Alikiba. Wanastahili kufurahia – actually, Watanzania wote bila kujali timu zilizopo tunapaswa kufurahia na kumpongeza Kiba kwa hatimaye kututoa kimasomaso.

Lakini kwanini Wizkid ambaye naye alipewa tu tuzo hiyo (si kama aliwawekea MTV EMA mtutu wa bunduki ili wampe) atukanwe? Kwanini mashabiki wanataka kutengeneza uadui si tu kati ya Wizkid na Alikiba, bali ni Nigeria na Tanzania?

Unadhani mashabiki wa Wizkid au Wanaijeria kwa ujumla wanapenda kuona msanii wao anatukanwa bila sababu? Kwanini hatuwezi tu kufurahia ushindi huu bila kumtusi, kumkejeli Wizkid ambaye kwa miaka yote amekuwa akiipenda sana nchi yetu? Isitoshe Alikiba amempongeza Wizkid kwa ushindi wake.

Sasa kwanini mashabiki wanashindwa kutambua kuwa msanii wanayempenda anahitaji kushirikiana na wasanii hawa na sio kutengenezewa tension baina yao isiyokuwa na faida! Nigeria ni sehemu muhimu Afrika kimuziki, si jambo la heri kwa msanii wa Tanzania kukimwagia mchanga kitumbua anachoweza kuhitaji kutoka huko siku za usoni.

Anachofanyiwa Wiz kwenye ukurasa wake ni aibu inayoirudia Tanzania. Watu wachache wanaharibu jina la nchi kwa kuendekeza ushabiki usiokuwa na afya. Na pengine ndio maana Wiz ametweet: Too many dumb people in the world. God help us!

Ombi kwa baadhi ya mashabiki wa Alikiba ama tu wengine ambao wameamua kutumia nafasi hiyo kumharibia siku Wizkid: Tunajidhalilisha kwa tunachokifanya. Hakuna faida ya maneno tunayomwandikia msanii huyu kipenzi cha wengi Afrika na duniani kwa ujumla. Tufurahi kuwa tuzo inakuja Tanzania na tumpongeze Ali kwa ushindi huo, basi!

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents