Habari

Mbunge wa Rombo: Nitajiuzulu maji yakitoka

Katika kile kinachoonekana kuwa na uhakika na kauli yake, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) amesema atajiuzulu ubunge wake kama mradi wa maji wa Chigongwe utatoa maji katika siku 21 zijazo.

Nadhiri hiyo imetokana na ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) katika miradi kadha ya Manispaa ya Dodoma ukiwemo wa Chigongwe ambao ulionekana kujawa na madudu kibao.

Selasini amesema, mazingira yaliyopo katika mradi huo yanapingana na kauli ya Kaimu Mhandisi wa Maji wa Manispaa ya Dodoma, Majuto Eliufoo ambaye aliomba kamati hiyo kumpa wiki mbili ili maji yaanze kutoka.

Mbunge huyo pamoja na kusema hayo, pia aliungana na wabunge na Mkurugenzi wa Manispaa ambao wamesema wazi kwamba haiwezekani katika wiki mbili maji yatoke na yeye (Eliufoo) kung`ang`ania kuwa itawezekana.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wakweli kwenye mambo ya msingi, na mimi nataka kuweka ukweli kwenye kumbukumbu kwamba, mradi huu ukianza kufanya kazi ndani ya wiki tatu tangu leo lazima na nisisitize kuwa itakuwa lazima kwa mimi kujiuzulu nafasi yangu ya ubunge,” amesema Selasini.

Mbunge huyo amesema anazo taarifa kuwa mradi huo wa maji katika eneo hilo ulianzishwa kisiasa ndiyo maana wataalamu hawajui chochote.

BY: Emmy Mwaipopo

Chanzo:Habarileo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents