Burudani

Mjue Rais wa Masharobaro

mr_choc

Kwa Tanzania ni wasanii wachache sana waliobahatika kuwa na vipaji vya uimbaji na utayarishaji wa muziki kama ilivyo kwa wenzetu katika nchi zilizoendelea, tayari tumeshuhudia kazi za kina Benjamin wa Mambo Jambo, Said Comorien, Akili the Brain, Bryton, Juma Nature, Jose Mtambo, Mr. Abel na wengine wengi.

 

Bob Junior ama Mr. Chocolate a.k.a Rais wa Masharobaro, ni mmoja wa watu waliopo katika kundi hilo, akiwa ni mtayarishaji katika studio za Sharobaro – ambaye baada ya kuwatoa wasanii kadhaa, sasa hivi ameamua kutoka mwenyewe.

Jina lake si geni masikioni mwa wadau wa burudani, kwani ndiye yewe aliyetayarisha kazi za wasanii kama walioibuka kwa kasi kama Diamond, Tox Star, Top C, Ude Ude. Hao ni baadhi ya wasanii waliopata kutoa kazi nzuri ambazo zimeweza kuwapandisha chati kwa haraka, zikitiwa mkono na Mr. Chocolate.

Umaarufu wao haukuishia katika kutoa kazi nzuri tu, bali pia kulipaisha jina la ‘Sharobaro’ ambalo awali hapa nchini lilikuwa likitafsiriwa kwamba ni wasanii wanaoimba kwa mtindo wa kubana pua, lakini kumbe maana halisi ya neno hilo ni watu walio nadhifu/maridadi.

Sasa baada ya kuwapaisha wakali hao, sasa Mr. Chocolate naye ameingia katika chati ya kumi bora za vituo vya televisheni, redio na magazeti mbalimbali nchini kupitia kibao chake kinachokamata ile mbaya kwa sasa – ‘Oyoyo’.

Rais huyo wa Sharobaro anasema kuwa kuingia kwake katika kuimba hakumaanishi kama anaipa kisogo fani yake ya utayarishaji muziki, bali anataka kuonyesha kipaji chake kingine.

“Unajua ma-sharobaro tumejaaliwa na vipaji lukuki, haiishii katika uimbaji tu, bali kuna watu wenye vipaji vya kila namna,” anasema.

Hata hivyo mtayarishaji huyo anasema ‘Oyoyo’ si wimbo wake wa kwanza kwani mwaka 2007/2008 aliwahi kutoa singo inayokwenda kwa jina la ‘Nafsi’ akimshirikisha Ali Kiba, lakini haikufanya vema – singo hiyo aliitayarisha mwenyewe.

Ndipo mwaka 2008/2009 kwa vipindi tofauti alikwenda kuongeza ujuzi katika tasnia ya utayarishaji wa muziki katika nchi za India na Finland.

“Baada ya kurudi ndipo nilipoafanya kazi ya Diamond kuanzia ‘Kamwambie’ hadi kukamilisha albamu yake nzima, pia nikaendelea kufanya kazi za wasanii wengine,” anasema.

Baada ya ‘Oyoyo’ kwa sasa anakuja na singo yake nyingine inayokwenda kwa jina la ‘Ng’ombe’ aliyomshirikisha mwanadada Lady Jaydee na tayari wimbo huo anaotarajia kuuachia hewani wakati wowote, ameshautambulisha katika ukumbi wa Club Bilicanas usiku wa Desemba 26.

Kama hiyo haitoshi, msanii huyo yupo katika matayarisho ya mwisho ya kukamilisha albamu yake ya kwanza ambayo ndani yake anatarajia kuwashirikisha wasanii kama Mr. Blue, Weasal & Radio kutoka Uganda, Ali Kiba na wengineo.

KUIMBA NA KUTAYARISHA AMEJIPANGA VIPI?

Mwenyewe anasema kwake vitu hivyo ni sawa, lakini anapenda zaidi kazi ya utayarishaji muziki kwani amepania kuwainua wasanii wengi chipukizi.

Anasema kutokana na urasimu ulipo katika studio nyingi yeye amekuwa akiwasaidia wasanii wengi kwa namna moja ama nyingine ili kuhakikisha wanatoa kazi ambazo zinakuja kuwa moto wa kuotea mbali.

“Kwanza mimi siwezi kuchukua hela ya msanii na kumuingiza studio moja kwa moja, ni lazima ajinoe kwanza mpaka aive,” anasema.

Anasema mpaka alipofikia hapo anamshukuru Mungu kwani ni jitihada na ubunifu wake mkubwa uliomuwezesha kutengeneza kazi ambazo zinakubalika.

Akizungumzia kuhusiana na kundi la Sharobaro, rais huyo anasema linaundwa na wasanii mbalimbali kama Top C, Showdad, Ali Kiba, Diamond, Q-Chillah, Tox Star, Ude Ude, Jacqline Wolper na wengineo.

Anasema pamoja na kuwa na wanachama, lakini pia anafanya utayarishaji wa kazi za wasanii wengine walio nje ya kundi lao.

“Tumejiwekea mikakati ya kila mmoja kutoka kwa zamu, ndiyo maana utaona mtu akishatambulisha singo kadhaa anatulia na kumpisha mwingine kabla ya kutoa albamu, na mwakani tunataka kutoa watu wawili hadi watatu,” anasema.

Kuhusiana na ushindani uliopo katika utayarishaji baada ya uwepo wa studio nyingi, anasema hilo si tatizo.

“Kama unafanya kazi nzuri utapata kazi nyingi,” anaongeza.

“Kikubwa ni kwa watayarishaji kuwa wabunifu na kuandaa kazi bora ndipo wataweza kuliteka soko, kinyume na hapo itakuwa ni kufanya kazi ya kubahatisha.”

Akiwa na matarajio ya kufanya makubwa zaidi katika medani hiyo, msanii huyo anasema kutokana na kuwa yeye ndiyo mpishi, atahakikisha anawafunika wasanii wake.

Anawashauri wasanii wenzake kujituma kuandaa kazi ambazo hazitakuwa kama pipi, yaani inasikika kwa muda mfupi na kisha kupotea.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents