Msaidizi wa Chenge atoa kali

Naibu Waziri wa Miundombinu Dokta Makongoro Mahanga ametoa kali Bungeni baada ya kusema anajibu swali kwa niaba ya Waziri katika wizara hiyo ambaye ameshaachia ngazi

Na Sharon Sauwa, Dodoma

 
 

Naibu Waziri wa Miundombinu Dokta Makongoro Mahanga ametoa kali Bungeni baada ya kusema anajibu swali kwa niaba ya Waziri katika wizara hiyo ambaye ameshaachia ngazi.

Wizara hiyo hadi juzi ilikuwa chini ya Bw. Andrew Chenge lakini akabwaga manyanga baada ya kuhusishwa na kashfa ya ununuzi wa rada.

Kwa kawaida Naibu Waziri anapotaka kujibu swali anapaswa kuanza kwa kusema, “kwa niaba ya Waziri wa (anataja Wizara husika) napenda kujibu swali la mbunge wa (anataja jina la mbunge aliyeuliza swali)“ ndipo anatoa majibu.

Kutokana na utaratibu huo, Dk. Makongoro alipotwangwa swali na Mheshimiwa Estherina Kilasa bungeni jana, alifuata staili hiyo na kujikuta akisema kuwa anajibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Miundombinu, bila kukumbuka kuwa waziri huyo ameshajiuzulu.

Baada ya kujibu swali hilo, Mbunge wa Dimani, CCM, Hafidh Ali Tahir alisimama na kuomba mwongozo kwa Spika, kisha akahoji ikiwa Waziri hayupo, wakati wa majibu, Naibu Waziri anapaswa kusemaje.

Spika Samuel Sitta alisema Dk. Makongoro ana nidhamu na kwamba amejibu hivyo baada ya kughafirika.

Akijibu hoja hiyo, Dk. Mahanga alisema ingawa Waziri husika hayupo lakini ofisi ya Waziri wa Miundombinu ipo na hivyo majibu yake yalilenga kuiwakilisha ofisi hiyo.

Hata hivyo baadaye katika muendelezo wa maswali alijibu moja kwa moja bila ya kusema kwa niaba ya Waziri wa Miundombinu.

Katika tukio lingine, Bw. Sitta amekataa kutoa ufafanuzi wa hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Koani, CCM, Mh. Haroub Said Masoud, aliyetaka mwongozo wa Spika juu ya uundwaji wa kamati za kushughulikia mambo maalum kama kamati ya ukimwi, na ya kushughulikia ufisadi.

Spika Sitta alisema mheshimiwa Masoud ameleta hoja hiyo wakati ambao haustahili na kwamba na kwa maana hiyo akasema anaiweka pembeni hadi muda wake utakapofika.

“Waheshimiwa wabunge tuache maswala ya kukurupuka kila jambo linawakati wake…. suala hili limeletwa wakati ambao si wa kwake,“ akasema.

 

 

Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents