Burudani

TCRA wafanya ukaguzi wa mwisho na kuiruhusu Radio5 kurudi hewani Disemba 16

Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania TCRA, leo December 14 imefanya ukaguzi wa mwisho, kujiridhisha na kuruhusu kituo cha utangazaji cha Radio5 Arusha kurudisha matangazo yake hewani ifikapo Disemba 16 mwaka huu 2016.

Akiongea na viongozi na baadhi ya wafanyakazi wa Radio5 baada ya kukamilisha ukaguzi wao, Mkurugenzi wa Utangazaji wa TCRA Fredrick Ntobi amesema wao kama Mamlaka waliamua kuja kufanya ukaguzi wao kwa ajili ya kujiridhisha kurudisha matangazo ya kituo hicho hewani December 16 ambapo ndiyo tarehe rasmi ya kuisha kwa Adhabu waliyokuwa wamewapa Kituo hicho.

Mamlaka hiyo ilifanya ukaguzi wa studio ya kurusha matangazo (On air Studio), studio ya kuzalisha vipindi (Production Studio), chumba cha Habari (News room), control Room, ofisi zote za kituo pamoja na mnara wa kurushia matangazo ambapo kote wamekuta kila kitu kiko sawa kwa kazi kama mamlaka inavyotaka.

Hata hivyo Fredrick Ntobi akiwa ameongozana na viongozi wa mamlaka ya mawasiliano Tanzania TCRA kanda ya Kaskazini, amewakumbusha watangazaji na waandishi kufuata maadili ya uandishi wa habari ili kulinda Vvituo vyao na kulinda taaluma zao kwa ajili ya kuendelea kuhabarisha na kuelimisha Jamii nzima ya Watanzania.

“Mimi niwasisitize tu kuendelea kufuata maadili ya taaluma yenu ya uandishi wa habari, kufuata sheria na kanuni za uandishi wa habari ambao mmesomea, tumieni lugha Sanifu ambayo inakubalika kwa jamii na tasnia yenu na niwatakie maandalizi mema ya kurudi hewani pamoja na Sikukuu zinazokuja,” alisema Ntobi.

Naye Mkurugenzi wa Tan Communication Media inayomiliki kituo cha Radio5, Robert Francis, amewataka Wasikilizaji wa Radio5 kukaa mkao wa kuhabarika, kupata burudani na kuelimika zaidi kupitia Radio5 kwani wamejipanga vyakutosha kurudi hewani kwa kishindo.

“Mimi niwaombe tu wasikilizaji wetu ambao najua wametumiss sana, wakae tayari kuhabarika, kuelimika na kuburudika zaidi sababu mimi na wafanyakazi wangu tumejipanga vya kutosha haswa ukizingatia kwamba mwaka mpya ndo huu unakuja,” amesema.

“Kingine niwape pole tu wasikilizaji wetu wote kwa kutotusikia hewani kwa kipindi cha miezi mitatu, pamoja na wadau ambao tumekuwa tukishirikiana kwa pamoja katika mambo mbali mbali niwaambie tu tunarudi rasmi Ijumaa ya tarehe 16 December 2016, aliongeza.

Kituo cha Radio5 kilisimamishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA kurusha matangazo yake tarehe 16 Septemba 2016.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents