Habari

Vigogo wabwagwa Dar

UCHAGUZI wa Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa wa Dar es Salaam ulifanyika jana huku Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk. Makongoro Mahanga na Mbunge wa Ubungo, Charles Keenja, waliokuwa wanagombea ujumbe wa kamati hiyo wakiwa miongoni mwa ambao majina yao yalikatwa na Sekretarieti ya Mkoa kwa kutotimiza vigezo kadhaa.

Shadrack Sagati


UCHAGUZI wa Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa wa Dar es Salaam ulifanyika jana huku Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk. Makongoro Mahanga na Mbunge wa Ubungo, Charles Keenja, waliokuwa wanagombea ujumbe wa kamati hiyo wakiwa miongoni mwa ambao majina yao yalikatwa na Sekretarieti ya Mkoa kwa kutotimiza vigezo kadhaa.


Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, majina manne kati ya19 ya walioomba kugombea ujumbe wa kamati hiyo yalikatwa na sekretarieti ya mkoa kwa kutotimiza vigezo mbalimbali na yaliyobaki ndiyo yaliyowasilishwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa kilichofanyika jana.


Kamati ya siasa ya mkoa ni chombo chenye madaraka ya kutoa uamuzi na maelekezo muhimu ya chama hicho kwa ngazi ya mkoa. Kwa hadhi, madaraka yake ni sawa na ya Kamati Kuu ya Taifa ya chama hicho.


Guninita hakutaja majina hayo, lakini vyanzo vyetu vya habari vilithibitisha kuwa majina ya Mahanga na wenzake yalikatwa pamoja na wabunge wengine wawili ambao ni Mbunge wa Viti Maalumu, Janeth Masaburi na mwingine ambaye hatukufanikiwa kupata jina lake.


Akizungumza baada ya uchaguzi huo ambao ulifanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Temeke, Guninita alisema wakati wa kuchuja majina waliamua kukata majina manne; lakini akasisitiza kufanya hivyo siyo kumbagua mtu ila walitaka kupata uwiano wa wagombea kutoka kila wilaya.


“Walikuwa 19 na tukarudisha majina 15, inawezekana wengine hawakufurahia utaratibu tuliotumia, lakini tumeufanya kwa kuzingatia misingi na taratibu za Katiba yetu,” alisema Guninita wakati akifunga mkutano huo.


Alisema wana-CCM ni lazima wakubali utaratibu wa kuachiana vijiti, hivyo akawataka wale ambao wameshindwa na wale ambao majina yao hayakurudi wasinune badala yake wajione kama waliochaguliwa ni watendaji wao.


Guninita alisema kamati hiyo ya siasa itawajibika kutoa taarifa kwa NEC Mkoa na akawataka wajumbe wa halmashauri hiyo ya mkoa ambao hawakushinda kuhakikisha wanaikosoa na kuihoji, kwani inaenda kutumika kwa ajili yao.


“Kwa hiyo nyinyi ambao hamkuchaguliwa au kupendekezwa mkione chombo hiki kama ni chenu,” alisema Guninita ambaye tofauti na utaratibu wa miaka yote wa kutoa majina mapema, safari hii alienda mbele ya wajumbe asubuhi na kusoma majina yaliyopitishwa na sekretarieti.


Guinita alisema utaratibu huo ni mzuri kwani wameufanya kwa kuzingatia jinsia na uwezo wa mgombea wa kushiriki vizuri. Alisema walipitisha majina hayo asubuhi na yakachapwa tayari kusomwa ukumbini mbele ya wajumbe. “Ni kweli tumepitisha majina haya asubuhi hii, tulikuwa na lengo letu.”


Alisisitiza katika kufanya hivyo, hawakubagua mgombea na akaongeza wametenda hivyo kwa kufuata haki na Katiba ya chama.


“Nawashukuru kwamba tulirudisha majina ya wanaume tisa na wanawake sita, lakini nyinyi wajumbe mmetuchagulia wanawake watatu na wanaume wawili, kwa kweli nawashukuru,” alisema Guninita.
Katika uchaguzi wa jana, walioshinda ni Sophia Simba kutoka Ilala, Ritha Mlaki (Kinondoni) na Said Kizega (Temeke). Wajumbe wengine wawili ambao walichaguliwa baadaye baada ya kupata washindi kutoka kila wilaya ni Rita Kabali na Jerome Mwanaussi.
Sophia alishinda kutoka katika wilaya ya Ilala na alipambana na Fatuma Sakali (9), Heri Kessy (1) na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Selemani Karanji aliyepata kura tatu.
Ritha alishinda kwa kura 17 kutoka katika wilaya ya Kinondoni ambako alipambana na Shy-Rose Bhanji (10), George Manyama (8), Zena Mgembe (2) na mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Aron Mwaikambo aliyeambulia kura nane.


Kutoka katika wilaya ya Temeke, Kizenga alishinda kwa kupata kura 17 na aliwashinda Ayubu Chamshama (5), Jerome Bwanaussi (9), Mustapha Yakub (14), na Salim Chicago ambaye hakupata kura.


Katika awamu ya kupata wajumbe wawili wa kuingia kwenye kamati hiyo, Rita Kabati alipata kura 31 na Jerome Bwanaussi alipata kura 28, hivyo wakachaguliwa kuwa wajumbe wa kamati hiyo. Katika kundi hilo walimshinda Yakubu aliyepata kura 21.


Awali wajumbe hao watatu walifungana kura 16 katika awamu ya pili ya uchaguzi ambao uliwashirikisha pia Shyrose Banji aliyepata kura 7, Fatuma (10), Mwaikambo (11), na Manyama kura 6, ndipo waliporudia uchaguzi huo kwa wagombea watatu na kupatikana washindi wawili.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents