Habari

Viwanja vya ndege 11 nchini kufanyiwa ukarabati

Serikali imeanza majadiliano na Benki ya Dunia ili kupata mkopo wa kugharamia ukarabati na upanuzi wa Viwanja vya Ndege 11 kwa kuzingatia mapendekezo ya ripoti ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao ulizingatia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukuaji wa shughuli za kiuchumi, utalii na mahitaji ya usafiri wa anga.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Ndikiye Mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Tanga Mhe. Mussa Mbarouk lililohusu Ujenzi wa Uwanja wa Ndege mkubwa na wa kisasa katika jiji la Tanga.

Mhandisi Ndikiye amesema kuwa kiwanja cha ndege cha Tanga ni miongoni mwa viwanja hivyo 11 vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kugharamiwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa Transport Sector Support Project (TSSP).

“Katika upembuzi huo kiwanja cha ndege cha Tanga ni miongoni mwa viwanja vilivyopewa kipaumbele kwa mahitaji ya ukaribu hivyo katika majadiliano ya awali Benki ya Dunia imeonesha nia ya kugharamia ukarabati wake.”

“Kwa sasa majadiliano kati ya Serikali na Benki ya Dunia yanaendelea yakiwemo mapitio ya awali ya ripoti za miradi iliyopendekezwa pamoja na maandalizi ya taarifa mbalimbali zinazohitajika kabla ya mkataba wa mkopo kusainiwa na baadaye kutangaza zabuni,” amefafanua Mhandisi Ndikiye.

Hata hivyo, Mhandisi Ndikiye alivitaja viwanja vingine vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu ikiwemo Lake Manyara, Musoma, Iringa, Songea, Kilwa Masoko, Lindi, Moshi, Njombe, Simiyu na Singida ambapo usanifu huo ulimalizika mwezi June 2017 kwa kuhusisha usanifu wa miundombinu ya viwanja hivyo kwa ajili ya upanuzi na ukarabati ili kukidhi mahitaji ya sasa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents