Habari

Wasanii waiomba serikali kuumalizia ukumbi wa BASATA

Wasanii nchini wameiomba Serikali kumalizia ujenzi wa ukumbi wa Sanaa za maonesho unaojengwa kwa zaidi ya miaka minane sasa makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) eneo la Ilala sharif Shamba jijini Dar es Salaam.

2
Msanii na mzalishaji filamu nchini William Mtitu (Kulia) akiongea na wadau wa Sanaa (hawako pichani) wakati akiwasilisha mada iliyohusu ‘Ubora katika filamu na changamoto zake’ kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii. Kushoto ni Katibu wa chama cha waandishi wa habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) Hassan Bumbuli

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa ya Baraza hilo mapema wiki hii, wasanii hao walieleza kwamba kwa sasa kuna ufinyu wa kumbi za za maonesho hali ambayo imekuwa ikiwafanya wasanii hao kukosa maeneo ya kufanya sanaa zao hivyo kumalizika kwa ukumbi huo itakuwa ni ahueni kubwa kwao.

1
Rais na mwanzilishi wa asasi ya Mabalozi wa Utamaduni wa Mwafrika (African Culltural Embassy Association) Colpas Numfor kutoka nchini Cameroon (Katikati) akionesha nyaraka mbalimbali za usajili wa asasi yake wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye programu ya BASATA ya Jukwaa la Sanaa. Kushoto kwake ni Katibu wa chama cha waandishi wa habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) Hassan Bumbuli na Kaimu Mkurugenzi wa asasi hiyo nchini Tanzania Maganiko Charles

“Ukumbi huu ni muhimu sana kwetu, wengi tuliutazama kama mwanzo wa ufufuaji wa Sanaa za majukwaani lakini sasa ni muda mrefu hauoneshi dalili za kumalizika. Kuna kila sababu ya ukumbi huu kukamilika ili kutusaidia katika maonesho yetu” alisema Msanii Khalid Kambau.

Kwa upande wake msanii wa Sanaa za maigizo Christian Kauzeni ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha wasanii waigizaji mkoani Dar es Salaam alisema kwamba kutokana na ukumbi huo kutazamwa kama mkombozi wa wasanii kuna kila sababu ya kuangalia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha unakamilika mapema iwezekanavyo.

Awali akiwasilisha mada kwenye Jukwaa hilo la Sanaa iliyohusu ‘Ubora wa Filamu na Changamoto zake’ msanii na mzalishaji filamu maarufu nchini William Mtitu alisema kwamba tasnia ya filamu chini imepata umaarufu na kukua ingawa bado changamoto za uharamia, elimu na masoko zimeendelea kuiathiri.

“Kwa sasa filamu zinazozalishwa zimekuwa na ubora kuliko huko nyuma. Tatizo liko kwenye elimu kwa wasanii, uharamia na masoko. Kulikuwa na maduka zaidi ya sabini na tano yanayouza kazi za wasanii wa filamu lakini kwa sasa yamebaki sita tu. Wengi wameamua kuuza kazi za nje mbazo ni nafuu. Hii ni hatari,” alisisitiza Mtitu.

Aliongeza kwamba pamoja na Serikali kuirasimisha sekta ya filamu bado kuna changamoto ya kazi zinazotoka nje kutokuwekewa stempu za mamlaka ya mapato huku kukiwa na uharamia unaotishia bei za filamu halali zenye stempu hizo.

Jukwaa la BASATA limekuwa likifanyika kwa mwezi mara mbili siku za Jumatatu na wiki hii kulikuwa pia na utambulisho wa asasi ya ubalozi wa Utamaduni wa Mwafrika ambayo imeasisiwa nchini Cameroon, Afrika Magharibi mwaka 2014.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents