Habari

Zoezi la kuwaokoa watu wanane walionasa kwenye kebo linaendelea

Uokoaji unaendelea kwa watu wanane, wakiwemo watoto sita, waliokwama kwenye gari la kutumia nyaya (Cable car) kwenye bonde kaskazini-magharibi mwa Pakistan.

Kundi hilo lilikuwa likielekea shuleni wakati moja ya nyaya hizo ilipokatika, na kuiacha ikining’inia mita 274 (futi 900) juu ya ardhi, maafisa walisema.

Kaimu Waziri Mkuu wa Pakistan amewaamuru waokoaji kufika kwenye tukio la “kuogofya” huko Battagram.

Helikopta za jeshi zimefika kwenye gari lakini hali ya uokoaji haijulikani. Abiria hao wanane walinaswa kwa takribani saa nne kabla ya helikopta ya kwanza kufika, chombo cha habari cha Dawn.com kiliripoti.

Tukio hilo lilitokea yapata saa 07:00 kwa saa za huko (02:00 GMT) siku ya Jumanne katika eneo la mbali, la milimani ambapo magari ya nyaya ni viunganishi vya kawaida kwa wakazi.

“Mungu tusaidie,” Gulfraz, mwanaume aliyekwama kwenye gari hilo, alikiambia kituo cha televisheni cha Pakistani cha Geo News kwa njia ya simu.

Alithibitisha watu wanane walikuwa ndani ya chombo hicho. Mmoja wa wanafunzi hao alikuwa amepoteza fahamu katika muda wa saa tatu zilizopita, alisema na kuongeza kuwa wanafunzi walikuwa na umri wa kati ya miaka 10 na 15.

“Watu katika eneo letu wamesimama hapa na kulia,” Gulfaraz alisema, akizitaka mamlaka kutuma msaada wa haraka.

Kulingana na picha mtandaoni, gari hilo la kebo limekwama katikati ya bonde lenye kina kirefu katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa.

Uokoaji unaonekana kuwa mgumu kutokana na upepo mkali na wasiwasi kwamba rota za helikopta zinaweza kuharibu zoezi afisa wa uokoaji katika eneo hilo aliiambia Reuters.

Helikopta moja tayari imerejea kutoka kwa safari ya uchunguzi huku nyingine ikitumwa hivi karibuni, aliongeza. Mwalimu wa eneo hilo aliiambia Dawn.com kwamba takriban watu 150 husafiri kwa gari la kebo kwenda shule kila siku kwa sababu ya ukosefu wa njia za usafiri katika eneo hilo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents