Habari

Achapwa Viboko kwa kuhudhuria Ibada Kanisani

Watu saba wa familia moja ya Kiislamu mashariki mwa Uganda wamekamatwa na mamlaka kwa madai ya kumpiga msichana wa miaka 18 ambaye alihudhuria ibada ya kanisa, polisi wamenukuliwa wakisema.

Msichana huyo anadaiwa kuchapwa viboko 100 na mjombake huku wajomba zake wengine watano wakimshikilia chini, tovuti ya habari ya Nile Post iliripoti.

Picha zilizoonekana kuonyesha msichana huyo akipigwa zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, na kuzua hisia kali miongoni mwa Waganda.

Familia bado haijatoa kauli yoyote kuhusiana na tukio hilo. Wajomba wa msichana huyo walikamatwa pamoja na shangazi yake, ambaye ni mlezi wake mkuu, polisi walisema.

Wataendelea kuzuiliwa wakisubiri uchunguzi, Samuel Semewo, kaimu msemaji wa polisi wa mkoa, alinukuliwa akisema na tovuti ya habari ya Daily Express.

Bado haijabainika watashtakiwa kwa makosa gani, lakini Bw Semewo aliambia gazeti la Nile Post kwamba vitendo hivyo ni sawa na kushambulia au mateso.

Pia aliliambia gazeti la Daily Monitor wanafamilia hao “walimpiga” msichana huyo “kwa viboko” na kwamba “alikuwa akiendelea kupata nafuu huku akisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu”.

Mwakilishi wa eneo hilo wa baraza la kitaifa la Waislamu alisema shambulio hilo linalodaiwa kuwa la kinyama na haliungwi mkono na kanuni za dini, gazeti la Daily Monitor liliripoti.

Chanzo:BBC Swahili

Imeandikwa na Mbanga B.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents