Moto Hauzimwi
Shinda na SIM Account

Askofu aanika wala rushwa wakuu

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dkt. Odernberg Mdegella, ametaja idara na taasisi zinazotakiwa kujisafisha kwa rushwa.

Na Francis Godwin, Iringa


ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dkt. Odernberg Mdegella, ametaja idara na taasisi zinazotakiwa kujisafisha kwa rushwa.


Askofu huyo hata hivyo ametaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa ya kwanza kufanya hivyo, na kuwataka viongozi wa dini kutokuwa waoga katika kukemea rushwa.


Aliyasema hayo wakati akichangia mada juu mbinu inayotakiwa kutumika ili kupunguza rushwa au kuepusha rushwa katika taasisi za Serikali, dini, vyama vya siasa, mashirika na watu binafsi.


Mada hiyo ilijadiliwa katika kipindi cha Jukwaa la Siasa kinachoendeshwa na kituo cha Televisheni ya Manispaa ya Iringa (IMVT) kwa kushirikisha viongozi wa vyama vya siasa, dini, waandishi wa habari na wananchi wa kawaida.


Alisema rushwa ilianza tangu mwaka 1995 wakati Serikali ya Rais Benjamin Mkapa ilipoingia madarakani na kuwa Rais Jakaya Kikwete aliikuta na amekuwa akifanya jitihada kubwa kuikomesha ila baadhi ya watu wamekuwa wakikwamisha jitihada hizo, kwa kubuni mbinu mpya kila kukicha.


Hata hivyo alisema anaposema TAKUKURU hana maana ya Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt. Hosea, ila anaitaka TAKUKURU kama taasisi kwa ujumla wake kuwa ya kwanza kujiosha.


Hivyo alisema vita dhidi ya rushwa ni ngumu iwapo viongozi wataendelea kuisema bila kutekeleza kwa vitendo mapambano yake.


Alisema baadhi ya wagombea wamekuwa wakilazimika kutoa rushwa baada ya kuona uwezo wa kushindana kwa hoja na wapinzani wao unakuwa mdogo na baadhi yao wakiomba mikopo kutoka vyama vya ushirika au benki huku mdhamini kwenye kampeni za uchaguzi.


“Hivyo Serikali pia imekuwa ikishiriki kutoa rushwa kutokana na kudhamini baadhi ya wanasiasa kuchukua fedha za kampeni kwa madai ya kuanzisha miradi…mimi nafikiri nitaje orodha kama waandishi wa magazeti mkiandika nitashukuru tu.”


Dkt. Mdegella alisema rushwa haitamalizika au kupungua kama wanasiasa wataendelea kutumia fedha kuomba nafasi mbali mbali za uongozi, hivyo alisema kwa upande wake ameona ni vyema kuwataja hadharani wale wote wanaopaswa kuanza kujisafisha.


“Kweli nasema kuwa wa kwanza kujisafisha awe TAKUKURU kwani wao ndio wapokeaji wa rushwa wakubwa. TAKUKURU wakisema nithibitishe nitawaonesha vitu tena watatia aibu, heri wasiniulize,” alionya.


Hata hivyo katika orodha hiyo, alisema nafasi ya pili ya watu wanaotakiwa kujisafisha ni viongozi wa vyama vyote za siasa, wakati kundi la tatu alilitaja kuwa ni Ikulu na kusisitiza kuwa hana maana ya Rais.


Dkt. Mdegella alitaja kundi la nne kuwa ni mawaziri ambao aliwataka wakutane na kuweka mkakati wa kutotoa rushwa katika uchaguzi wowote ujao.


“Mawaziri wetu waanze kumsaidia Rais Kikwete katika mapambano dhidi ya rushwa, kwa kuweka kikao cha pamoja na kusema kuwa uchaguzi ujao uendeshwe bila rushwa.


“Kweli wakae na kujisafisha, kwani rushwa inayotolewa kwa wapiga kura ni ya aibu; yaani unapikiwa wali halafu nawe unasema ni rushwa hiyo…mwenzako anakwenda kukaa miaka mitano wewe unakula wali siku moja au kitenge na mpira,” alisema.


Alisema kundi la tano ni Polisi, la sita Mahakama na kundi la saba ni watoa vibali mbali mbali katika halmashauri na kundi lingine ni sifa za wagombea wa nafasi mbali mbali.


Katika hilo alisema kwa upande wake hawezi kukubali mtu ambaye hajafika kidato cha sita, kwenda kugombea ubunge na kuwa iwapo inatokea hivyo katika mkoa wa Iringa, yeye akiwa Askofu atasimama kupiga kampeni ili mtu huyo asishinde.


Hata hivyo, alisema rushwa haina dini wala chama, hivyo ili kuisaidia Serikali katika mapambano ya rushwa, ni vyema kujitokeza kuikemea.


Alisifu ujasiri wa Mchungaji Christopher Mtikila katika kupambana na masuala mbali mbali na kumtaja kuwa mmoja wa viongozi wa dini, ambaye amekuwa akikubali kufungwa jela na anapotoka anaendeleza mapambano zaidi.


Source: Majira

Leave a comment

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW