Siasa

ATC waanza kutafuta mchawi

BODI ya Shirika la Ndege Tanzania (ATC) jana imefanya kikao cha dharura kujadili sakata la mchakato wa safari ya mahujaji kwenda Makka, Saudia na jinsi watakavyorudi bila usumbufu.

Na Ramadhan Semtawa


BODI ya Shirika la Ndege Tanzania (ATC) jana imefanya kikao cha dharura kujadili sakata la mchakato wa safari ya mahujaji kwenda Makka, Saudia na jinsi watakavyorudi bila usumbufu.


Agenda ya msingi katika kikao cha bodi hiyo ni jinsi mchakato huo ulivyofanyika na mahujaji watakavyorudi, hivyo baadaye kuweza kuandaa taarifa kwenda kwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge.


Meneja Uhusiano wa ATC, Godfrey Muganyizi, alipoulizwa ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, alithibitisha kufanyika kwa kikao hicho cha bodi, lakini akasema hafamu agenda zilikuwa zinajadiliwa.


Tayari serikali kupitia waziri Chenge, imetoa msimamo wa kuitaka bodi itoe maelezo baada ya kumalizika kwa safari za mahujaji hao ambayo itakuwa ni baada ya kurejea nchini.


Serikali imeitaka bodi hiyo iandae taarifa kueleza mchakato mzima kuanzia kumpata wakala huyo na vigezo vilivyotumika.


Msimamo huo wa serikali ndiyo ambao umekuwa ukiumiza vichwa vya wajumbe wa bodi hiyo wanaoongozwa na Mwenyekiti wake, Balozi Mustapher Nyang’anyi.


Hata hivyo, Muganyizi alipoulizwa ni vipi mchakato huo ulivurugika na hadi ATC kuingizwa mkenge, alijibu: ” Mambo unayouliza siwezi kuyajibu, hayo yameshapita katika ngazi yangu yapo kwenye bodi “.


“Bodi itatakaa na kujadili kisha itampa waziri taarifa, tayari na waziri ameshatoa tamko la serikali sina cha kuzungumza kuhusu mchakato huo,” alisisitiza Muganyizi.


Muganyizi alipoulizwa tena kiasi halisi cha fedha ambacho ATC ililipa wakala Kampuni ya Al Wasam ya Saudia na hatua zitakazochukuliwa na shirika alijibu: “Hayo yote yapo chini ya mamlaka ya bodi”.


Pamoja na maelezo ya Muganyizi, taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza zaidi kamba wajumbe wote wa bodi walikuwepo.


Kwa mujibu wa taarifa hizo, kikao hicho awali kilikuwa kifanyike mjini Bagamoyo mwishoni wa wiki iliyopita, lakini haikuwezekana.


Hata hivyo, taarifa ya bodi kwenda serikalini huenda ikatolewa wakati wowote lakini ni hadi ATC ihakikishe mahujaji wamerejea nchini baada ya kutimiza nguzo ya dini yao wiki ijayo.


Sakata la kukwama kwa mahujaji hao limeitikisa serikali hadi kuamua kiingilia kati ili kuokoa jahazi kwa kukodi ndege ya Kampuni ya Global Aviation ya Afrika Kusini.


Uamuzi huo ulitokana na wakala Kampuni hiyo ya Al wasam kushindwa kupata ndege na kibali cha kutua na kuegesha ndege (Ground Handling)nchini Saudia, licha ya kupewa kazi hiyo karibu mwezi mmoja uliopita.


Mahujaji hao ambao hatimaye waliondoka kwa mafungu kwa kuchelewa, walikwamba katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa siku 12.


Hali hiyo iliwalazimu Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuingilia kati ambapo Rais alilazimika kuchelewa safari yake ya kwenda Marekani na Lowassa kuahirisha ziara yake ya mkoa wa Kagera.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents