Siasa

AU sasa kumjadili Mugabe Misri

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, ameondoka nchini jana kwenda Misri, kuhudhuria kikao cha 11 cha wakuu wa nchi za Afrika, ambako, pamoja na mambo mengine, kitazungumzia hali ya kisiasa nchini Zimbabwe

MWENYEKITI wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, akitua nchini Misri
na Mwandishi Wa Tanzania Daima

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, ameondoka nchini jana kwenda Misri, kuhudhuria kikao cha 11 cha wakuu wa nchi za Afrika, kitakachofanyika mjini Sharm El Sheikh, ambako, pamoja na mambo mengine, kitazungumzia hali ya kisiasa nchini Zimbabwe.

 

Rais Kikwete anatarajiwa kuwa mwenyekiti wa kikao hicho kilichotanguliwa na kikao cha siku mbili cha 16 cha kawaida cha Baraza la Utendaji la AU, kilichoanza June 27, mwaka huu, chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Tanzania, Bernard Membe.

 

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imeeleza kwamba mada kuu katika kikao cha wakuu wa AU ni maji na usafi wake, chini ya mada ya jumla ya juhudi za Afrika kutekeleza maazimio ya milenia.

 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kikao kitapokea na kujadili ripoti ya Kamati ya Wakuu 12 wa AU kuhusu kuanzishwa kwa serikali ya Umoja wa Afrika, ambapo mjadala kuhusu suala hilo unaendelea tangu Libya ilipotoa pendekezo la kuanzishwa kwa serikali hiyo mwaka 2005.

 

“Ripoti itawasilishwa na Rais Kikwete, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, iliyokutana katika kikao chake, Arusha, Mei 22 na 23, mwaka huu, “Mbali na Tanzania, nchi nyingine yenye wajumbe katika kamati ya wakuu 12 ni Ghana, Senegal, Libya, Misri, Botswana, Afrika Kusini, Ethiopia, Uganda, Gabon na Cameroun ambazo zote zilihudhulia mkutanao wa Arusha,” ilieleza taarifa.

 

Ilifanunua kuwa kikao cha Sharm El Sheikh kitajadili na kufikia uamuzi kuhusu pendekezo la kuunganishwa kwa mahakama ya Afrika kuhusu haki za binadamu na Waafrika pamoja na mahakama ya AU.

 

Kikao hicho pia kitateua majaji wanne wa mahakama hiyo kati ya majaji saba wanaowania nafasi hiyo.

 

Pamoja na hayo, kikao kitapokea na kujadili ripoti ya shughuli za Baraza la Amani na Usalama la AU. Mjadala huo utagusia hali ilivyo katika nchi za Comoro, Burundi, Ivory Coast, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Somalia, Darfur na Zimbabwe.

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents