Siasa

‘Chenji’ ya rada Tanzania kuambulia patupu

TAMKO la Rais Jakaya Kikwete kuwa Serikali yake italazimika kuidai kampuni ya BAE Systems ya Uingereza sehemu ya fedha zilizozidi (chenji)

Hassan Abbas na Grace Michael

 

TAMKO la Rais Jakaya Kikwete kuwa Serikali yake italazimika kuidai kampuni ya BAE Systems ya Uingereza sehemu ya fedha zilizozidi (chenji), iwapo mkataba wa ununuzi wa rada utabainika kuwa uliongezwa thamani ili kuwanufaisha watu wachache, imeelezwa kuwa inaweza kugonga ukuta na kubaki ya kisiasa kutokana na sababu nzito za kisheria.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Majira kwa wiki kadhaa kwa kuangalia sheria na rejea ya kesi mbalimbali za Uingereza na za Tanzania katika masuala ya mikataba, kauli hiyo ya Rais Kikwete, aliyoitoa hivi karibuni alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari, imebainika, inaweza kuishia kuwa ya kisiasa.

Katika utafiti huo sheria za Kiingereza na hata zile za Tanzania, imebainika, zinakubaliana katika msingi mmoja, ambao ndio kikwazo cha kwanza kwa azma ya Rais Kikwete kwamba mkataba wowote unaposainiwa, kwa pande mbili husika kukubaliana, suala la thamani ya mkataba kama imepunguzwa au imepandishwa halina msingi.

Katika dhana hiyo, wasomi wa taaluma ya sheria wanasema masharti ya msingi ya kusainiwa mkataba yakifikiwa, kama vile wahusika kukubaliana bali shuruti wala ulaghai, na ikabainika kuwa waliohusika wote wananguvu au mamlaka kisheria kuingia kwenye mkataba, inatosha kuufanya mkataba huo kuwa halali.

Msimamo huo unaonekana kuikwaza azma ya Tanzania kudai kile tunachoweza kukiita ‘chenji’ hata kama itabainika kuwa mkataba wa ununuzi wa rada, uliongezwa thamani katika mazingira ya rushwa.

 

Katika utafiti huo, Majira limebaini kuwa kudai chenji katika mkataba wa rada iwapo maofisa wa Tanzania walijua kwa dhati suala la bei na aina ya mtambo wanaoununua una thamani na teknolojia ya kiwango gani, ni jambo litakalokosa mantiki kisheria labda ziwepo sababu ambazo wataalam wanaziona zitasaidia.

Katika kufafanua hoja inayofanana na sakata hilo, Mahakama ya Rufani ya Uingereza tayari imeweka bayana mawazo yake kupitia shauri mashuhuri la Chappell & Co. LTD VS Nestle Co. LTD (1959) 2 All ER, 701, ambapo iliamuliwa kuwa hata kama mhusika katika mkataba aliamua mwenyewe kuuza gari lake kwa pauni moja, kisheria mkataba huo utakuwa halali.

Katika uchunguzi huo, Majira limebaini zaidi kuwa ushahidi uliopo mpaka sasa kwenye ripoti rasmi (Hansard) za Bunge la Mamwinyi (House of Lords) la Uingereza unaibana zaidi azma hiyo ya Rais.

Katika ‘Hansard’ hizo, maafisa kadhaa wa Tanzania wamenukuliwa humo, wakitetea kuwa rada iliyonunuliwa ndiyo ambayo Tanzania ilikuwa ikiihitaji na iliridhika nayo kwa mujibu wa mahitaji yake.

Kauli hiyo na msimamo wa sheria za Uingereza kama ulivyooneshwa katika shauri la Chappell, ni kikwazo ambacho kinaweza kuizima azma ya Tanzania na hata kama Serikali itafungua kesi, yanaweza kujirudia yale ya IPTL, wanashauri baadhi ya wataalam hao.

Baada ya kuangalia msimamo wa sheria za Kiingereza, imebainika kuwa hata sheria za Tanzania hazitofautina sana ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Mikataba (The Law of Contract Ordinance [LCO]), thamani iliyokubaliwa na pande mbili zinazoingia mkataba ndicho kitu cha muhimu.

Hata hivyo wataalam mbalimbali wa sheria wanasema, upo mwanya mdogo kwa Serikali ya Tanzania kuweza kufanikiwa katika azma hiyo ambapo itailazimu Serikali kuupitia mchakato mzima wa mkataba wa ununuzi wa rada na waliohusika wahojiwe ili yapatikane masuala matatu ya msingi ambayo yanaweza kuisaidia Tanzania.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, mawakili mbalimbali mashuhuri wa Dar es Salaam, wameyataja mambo hayo kuwa ni Serikali kutakiwa kuthibitisha kwamba wakati wa kusainiwa mkataba kulikuwa na mazingira ya ulaghai, kutokuelewana au upande mmoja kulazimishwa (hata kwa kishawishi cha rushwa) kuingia mkataba huo, ndipo suala la kudai chenji linaweza kueleweka kisheria.

Akizungumza na Majira, Wakili wa kujitegemea Bw. Gaudiosus Ishengoma, alisema kuwa kuhusiana na sheria ya mkataba huwezi ukadai kitu chochote endapo mnunuzi wa kitu hicho aliingia mkataba na muuzaji kisheria bila ya kuwa na msukumo wowote au kulazimishwa kufanya hivyo ili kulinda maslahi fulani ambayo ni kwa faida yao.

” Unaweza ukadai endapo mkataba huo utangundulika ulifanyika kwa njia za ulaghai, kuwepo kutokuelewana au kuwepo msukumo kutoka nje ambao unaweza ukafanywa na watu wengine ili kushinikiza mkataba huo. Hapo ndio sheria inaweza ikachukua mkondo wake na si vinginevyo,” alisema Bw. Ishengoma.

Akizungumzia suala la ununuzi wa rada Bw. Ishengoma alisema kuwa Tanzania itaweza kudai fedha hizo endapo tu mkataba huo ulikuwa na makosa hayo.

Naye Wakili Bw. Charles Semgalawe alipohojiwa kuhusiana na masuala ya mikataba kisheria, alisema kuwa inawezekana kudai endapo kulikuwa na chembechembe za udanganyifu, hilo lisipokuwepo inakuwa ni ngumu kudai malipo yoyote.

Kutokana na mazingira hayo kuwa magumu kuyathibitisha kisheria, wengi kati ya wataalam waliozungumza na Majira, waliitahadharisha Serikali isije ikiwaingiza tena Watanzania kwenye hasara kama ya IPTL, ambapo kesi iliongeza gharama za uendeshaji na uzalishaji wa umeme nchini.

Suala la Serikali ya Tanzania kujaribu kupambana na ufisadi katika masuala ya mikataba mingi inayoonekana kusainiwa katika mazingira tete limekuwa tata.

Miaka kadhaa iliyopita Serikali kupitia TANESCO ilijaribu kuuvunja mkataba wake na kampuni ya IPTL kwa kupeleka shauri hilo kwenye Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Uwezekaji la London, ambapo kimsingi Serikali ilishindwa na kutakiwa kulipa mabilioni zaidi kwa kampuni hiyo na kusababisha gharama za uzalishaji na hata bei za umeme kupanda.

 

Kwa sasa suala la sakata la rada linaendelea kuchunguzwa na Taasisi za Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKURU) na ile ya Uingereza , SFO.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents