BurudaniHabari

Chitalilo atamba kutesa miaka 20

SIKU kadhaa baada ya Jeshi la Polisi kubainisha kuwa Mbunge wa Buchosa, Samwel Chitalilo, aliwadanganya wapiga kura kuhusu elimu yake, mbunge huyo ameibuka na kutamba kuwa kashfa hiyo haitamharibia.

na Jovin Mihambi, Sengerema

 

SIKU kadhaa baada ya Jeshi la Polisi kubainisha kuwa Mbunge wa Buchosa, Samwel Chitalilo, aliwadanganya wapiga kura kuhusu elimu yake, mbunge huyo ameibuka na kutamba kuwa kashfa hiyo haitamharibia.

 
Akizungumza jimboni humo mbele ya Naibu Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo, ambaye alikuwa wilayani humo kukagua ujenzi wa shule mpya za sekondari, Chitalilo alisema kuwa, anao uhakika wa kukalia kiti hicho cha ubunge kwa muda wa miaka 20 ijayo.

 
Chitalilo alisema kuwa, suala kuwa aliwadanganya wananchi kuwa alisomea Uganda na kuhitimu kidato cha sita, halioani na utendaji wake wa kazi akiwa mbunge wa Jimbo la Buchosa.

 
Aliongeza kuwa, anao uhakika wa kukalia kiti hicho kwa muda huo, kwa madai kwamba wananchi wa Buchosa bado wanauhitaji mchango wake kwa maendeleo yao.

 
Akitumia historia, mbunge huyo aliuelezea ubunge wake kuwa na baraka kutoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

 
Alisema Mwalimu alipofika katika eneo hilo la Buchosa ambalo wakazi walihamishiwa hapo wakitokea Kisiwa cha Ukara, kilichoko katikati ya Ziwa Victoria, alipanda mti nyumbani kwao, kwa mzee Chitalilo.

 
Huku akiomuonyesha naibu waziri mti huo, Chitalilo alisema kitendo hicho cha Mwalimu kilikuwa ni ishara tosha ya kuibariki familia ya mzee Chitalilo.

 
Alisema mti huo ulikuwa ni kielelezo kuwa, katika familia hiyo atazaliwa kiongozi atakayekubalika, ambaye atawaongoza wananchi wa Buchosa.

 
Mbunge huyo ambaye amekuwa kimya kabisa tangu aanze kuandikwa na vyombo mbalimbali vya habari kuhusu sakata lake la elimu, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye ni mbunge wake, kinafahamu vyema utendaji kazi wake.

 
Alisema mbali ya chama chake, Bunge nalo linatambua utendaji wake na ndiyo maana limempanga katika baadhi ya kamati nyeti za Bunge hilo, ikiwamo Kamati ya Fedha.

 
Mbunge huyo alieleza kufurahishwa na hatua ya Jeshi la Polisi kushindwa kumchukulia hatua yoyote dhidi ya madai ya kughushi vyeti.

 
Alisema anatambua pia kwamba, CCM haiwezi kusitisha ubunge wake kutokana na masuala ya vyeti, na kuongeza kuwa, ubunge na vyeti ni vitu viwili tofauti.

 
“Ubunge si makaratasi, ila ni uongozi ulio imara kwa wananchi na wao wakukubali kuwa ni kiongozi wao ambaye uko karibu kusaidia maendeleo yao,” alisema Chitalilo.
Hata hivyo, mbunge huyo alishindwa kukubali au kukataa madai yanayomhusisha yeye na kuwadanganya wapiga kura wakati wa kampeni kuwa alikuwa amewahi kusoma katika chuo kimoja nchini Uganda.

 
Katika mkutano huo wa hadhara, Chitalilo alichangia shule za sekondari za Nyakasungwa na Kafunzo kiasi cha sh 700,000 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi unaoendelea.

 
Kauli hiyo ya Chitalilo inakuja siku mbili tu baada ya gazeti la Tanzania Daima Jumapili, katika toleo lake la juzi kumkariri, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Manumba akisema jeshi hilo lilikuwa limethibitisha pasipo shaka kuwa mbunge huyo aliwadanganya wapiga kura wakati wa kampeni.

 
Hata hivyo, jeshi hilo lilisema, lilikuwa haliwezi kumchukulia hatua yoyote, zaidi ya kulirejesha suala la mbunge huyo katika chama chake (CCM) na kuliwasilisha kwa Spika wa Bunge.

 
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents