Burudani ya Michezo Live

Exclusive: B’Hits yaeleza upande wake wa ‘story’ ya kuondolewa kwa Gosby, Vanessa na Mabeste nje ya label

Baada ya kuondolewa kwa Gosby, Mabeste na Vanessa Mdee kwenye label ya B’Hits Music Group, kumeendelea kuwepo kwa hali ya sintofahamu kuhusiana na sababu halisi ya tukio zima. Pande hizo mbili zimekuwa zikitupiana lawama na kuwaacha wafuatiliaji wa masuala ya muziki nchini wakiwa njia panda, wasijue nani wa kumuamini.

75903_10201563809284658_2090434671_n
Wasanii wa B’Hits. waliotoka na wale waliosalia

Tumefanya mahojiano marefu na Afisa Muendeshaji Mkuu (COO) wa B’Hits, Amani Joachim ambaye ameeleza kiunagaubaga upande wao wa story. Ameanza kwa kueleza madhara ya wasanii hao kuondoka kwenye label hiyo.

“Kuna athari za aina mbili,” anasema Amani ambaye pia ni mwanasheria wa kampuni hiyo. “Athari kubwa ya kwanza ni kurudi nyumba katika mipango ambayo tulikuwa tumepanga kwanza kwa wasanii ambayo mipango ile ingeweza kufanikiwa kwa hawa wasanii … anapofanikiwa msanii na kampuni na yenyewe inafanikiwa. Tulikuwa tunaplan let’s say two years, three years, sasa hivi sio tena miaka miwili au mitano, imesonga mbele. Lakini kwa upande mwingine, mpaka sasa hivi tunaumia kitaswira. Taswira ya kampuni inaumia na taswira wa CEO wa kampuni sasa hivi personally.

Kutoka kwenye kampuni sasa imeanza kuhamia kwenye mtu binafsi. Hermes Joachim au Hermy B anaumia kwasababu kulikuwa na hizo fikra za nini kilitokea, nini kinatokea na nini kitatokea ambacho kimetokea kuonesha kwamba Hermy B yuko vipi, pamoja na uongozi wa B’Hits upo vipi, kitu ambacho kwangu ni uongo.

Akielezea sababu za Vanessa Mdee, Gosby na Vanessa kuondolewa B’Hits, Amani amesema ni kutokana na utovu wa nidhamu.

“Sababu zipo tofauti sababu hawa wasanii wenyewe pia wameingia kwa time tofauti. Tofauti pia na fikira zao ni kwamba walikuwa na mikataba tofauti. Vanessa na Gosby sababu zao zinafanana kiasi fulani, Mabeste ya kwake ni tofauti. Sababu kubwa ya Vanessa na Gosby ambayo naweza nikaisema ni misbehaviour.

Vanessa na Gosby wameondoka kutokana na kuvunja mkataba mara kwa mara sio kitu cha mara moja. Imefika mwisho tukaona sasa misamaha imekuwa mingi ambazo ukija ukaproject utagundua kuwa nisamehe nisamehe zitaendelea, tukaona this is just enough.”

Hata hivyo Amani amezikanusha tetesi kuwa Gosby na Vanessa waliondolewa kwasababu walitumbuiza kwenye Fiesta, Dar. “Hiyo ni fikra kubwa ambayo watu wanaifikiria,” anasema. “Nimeshaulizwa sana huko nje, lakini ni uongo kwamba hawakuondolewa sababu walienda kufanya tamasha la Fiesta and I have to say Fiesta is very big. We appreciate Fiesta kuwepo na vile vile tunajua ni kitu kikubwa na ni platform imetupatia tena hata wasanii wetu including Mabeste wamekuja kuonekana kwenye matamasha kama ya Fiesta tutakuwa waongo tukisema Fiesta ni kitu cha kawaida.

But what happened kuhusu Vanessa na Gosby ni kwamba walibuku lile onesho bila kutoa taarifa katika uongozi. Fiesta is big ilitakiwa kupanga nini cha kufanya kikubwa utishe kuliko wenzako, B’Hits ionekane ina rock. Ikaenda hatukuambiwa chochote. Hermes wanted to react.”

Amani amesema baada ya kuona hivyo waliamua kutumia formula waliyoianzisha ya kutotoa beat nzima na kutoa yenye urefu wa sekunde 30 tu ambayo madj wanaweza kuitumia kama wakiiunganisha lakini si kwa wasanii.

Hatua hiyo ilichukuliwa kama njia ya kuwabana wasanii wasifanye show kinyemela. Amesema hicho ndicho walichomwambia Gosby ambaye alisema katika uongozi alikotoka hakukuwa na utaratibu kama huo lakini Amani aliendelea kushikilia msimamo wake.

Baadaye Vanessa naye alijaribu kumuomba Hermy B apewe beat ya wimbo Monifere lakini naye aliendelea kushikilia msimamo wake. Baadaye Hermy B na Amani waliwaambia kuwa kama wanataka kupata beat hiyo waende studio kuiunganisha wenyewe lakini si kwa kutumia producer wa nje na Pancho na Hermy wasingefanya kazi hiyo.

“Tulikuwa tunajua kabisa hii si simple statement ya kuwaambia kwamba we are not going to do this, but you cannot imagine what happened,” amesema Amani na kueleza kuwa Vanessa na Gosby walienda studio kutaka wafanye kazi hiyo wao.
Amesema alipokea simu kutoka kwa Vanessa ambaye hawakuwa wameongea kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na kuwa na tofauti lakini hakuipokea hadi pale alipoona simu ya Hermy B ikiita pia.

Hermy B ambaye muda huo alikuwa nje ya nchi alimuambia Amani kuwa Gosby na Vanessa walikuwa wanamlazima Pancho awape beat. “Unapokuja studio wewe sio producer halafu unaambiwa uje kuproduce beat au kubounce na unajua kabisa huwezi,wewe unakuja kufanya nini? Vanessa na Gosby walikuja kufanya nini katika studio ya B’Hits wakitaka beat? Mimi kwangu naiita kuleta fujo na actually walileta fujo. Walimkuta Pancho in a middle of business, alikuwa anafanya kazi ya client wakamwambia azime, afungue Monifere na awape beat. Hapo ndio mambo yetu yalipoishia, hiyo ndo source ya sisi Vanessa na Gosby kuachana.”

Akielezea imani ya watu wengi wanaoamini kuwa mikataba ya wasanii wengi wa B’Hits ni migumu na haiendani na mazingira ya Kitanzania, Amani amesema mikataba yao ni ya kawaida lakini tatizo linakuja kutokana na ukweli kuwa muziki wa Tanzania hauna fedha kiasi hicho.

“Mikataba ya muziki Tanzania is just useless,” amesema.

“Wasanii wengi sana wa Tanzania hawana fedha. Na unapoingia mkataba na mtu ambaye hana fedha just know that unajizika wewe mwenyewe. Niambie wasanii wangapi wa B’Hits waliowahi kuwaumiza B’Hits wana hiyo fedha ya kuwalipa B’Hits,” anahoji.

Amani amesema kuwa tatizo jingine kubwa lililopo Tanzania ni kuwa wasanii wakubwa Tanzania hawalipii nyimbo wanazorekodi. Amesema B’Hits iliacha siku nyingi kufanya nyimbo kwa njia hiyo kwakuwa haina tena muda wa kutafuta jina na sifa.

“Hiyo ndio tofauti ya B’Hits na producer mwingine ambaye sasa hivi mnamsikia ana nyimbo nyingi sana. When B’Hits actually said ‘this is enough’ na ikagundua kwamba muziki hauna fedha nyingi namna hiyo, ikaamua kuengage na masuala mengine ya biashara.”

Amani amefafanua pia kauli ya Hermy B kuhusu kudai kuwa aliwekeza kwa karibu shilingi milioni 30 kwa Mabeste ambayo wengi waliitafsiri vibaya kuwa ni fedha taslimu. “Kazi tuliyoifanya mpaka sasa hivi inaweza kuwa approximately.. we know it’s more kwasababu Mabeste ana albam na nusu.. Ile statement tulikuwa tunaongea ‘intellectual property, tunaongelea wazo la mtu, kitu ambacho leo ukikichukua ukakivalue, ule muziki unaweza ukakulipa kiasi hicho cha fedha.”

Akimuongelea Mabeste, Amani amesema pamoja na rapper huyo kufanya show nyingi za nje na fedha zote walikuwa wakimuachia kwakuwa hakikuwa kiasi kikubwa lakini mwisho, walimwambia inabidi aachane nazo kwakuwa huo ndio ulikuwa ugomvi wao uliofanya aondolewe.

“Tukaja kumwambia achana na hiyo kitu. Mabeste is talented. Tumegongana na Mabeste sasa hivi lakini nakuhakikisha hakuna rapper kama Mabeste. Mpaka nakufa mimi ntakuwa fan wake namba moja, hakuna rapper mkali kama Mabeste hapa Tanzania,” anasisitiza Amani.

Amesema hata baada ya kuondoka B’Hits, wamekuwa wakimuomba kwa muda mrefu arudi na waanze ukurasa mpya lakini amekataa. “Hermy anamuomba Mabeste arudi, ‘tusiende huko bro, tusifikishane mbali, mimi sitaki tufike huko, rudi tuje tufanye kazi yameisha, achana na hiyo mambo’ anakataa.”

Amani amesema hali iliendelea hivyo hadi wakaamua kuachana naye lakini wameshindwa kujua sababu ya yeye kufanya hivyo.

“That’s the only artist ambaye tulikuwa tumekaa naye mambo yakashindikana. Ugomvi wetu sisi na Mabeste ulikuwa ni hayo masuala ya kufanyafanya show nje za hovyo hivyo. It wasn’t really about man lakini ‘kwanini usitoe taarifa ghafla umeanza kuwa dishonest’.

Akizungumzia nyimbo za wasanii hao zilizobaki studio, hadi sasa Amani ambaye ni producer na mwandishi pia wa nyimbo, amesema hawajajua zitafanywaje. “Tuna uwezo wa kuzifungia hizo nyimbo tukawa tunazisikiliza kwa burudani yetu sisi wenyewe. So far mimi personally sijadesign njia ya kuzifanya zile nyimbo, but one thing I am very sure zinaweza kuwa za burudani yetu sisi wenyewe.”

Katika hatua nyingine Amani aliwasihi wasanii hao waliondoka B’Hits kuachana na tabia ya kuichafua ‘B’Hits kwa kupakaza shutuma zisizo na ukweli. “Waache kuongea uzushi na maneno ya uongo.”

Ametolea mfamo uzushi uliopo kuwa wasanii hao hawakulipwa kwenye show ya Azonto kitu ambacho ni uongo.
“Mimi ndio mtu niliyekuwa nadeliver hizo fedha, watu wamelipwa. Sasa atokee ambaye anasema kwamba hajawahi kulipwa show ya Azonto, msanii yeyote au mtu yeyote hadi mtu aliyefagia siku ya mwisho, kila mtu alilipwa,” amesisitiza.
Amani amewataka wasanii hao walioondoka B’Hits kuacha kuipaka matope B’Hits kwakuwa wanachafua jina lake mbele ya umma.

“Mimi nimekuja nimeongea ukweli wangu. Worry yangu ni kuwa tunachafuliwa image. Hermy sasa hivi anaumia na anachafuliwa image yake,vyote ni vya uongo. Njoo hapa mbele Bongo5 useme kwamba ‘hiki na hiki anachosema Amani ni uongo na ukweli ni huu’. But otherwise kama ni uongo jamani tusiumizane. Kila mtu aende kwa amani yake na tuendelea na maisha mengine.”

MSIKILIZE AMANI KWA UREFU:

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW