Siasa

JK apasua ukweli kuhusu Richmond

RAIS Jakaya Kikwete, ameanika ukweli na kisa cha kuipa zabuni kampuni ya Richmond Development Corporation (RDC), kuzalisha umeme wakati wa mgao nchini mwaka jana.

Titus Kaguo, Brussels

 

RAIS Jakaya Kikwete, ameanika ukweli na kisa cha kuipa zabuni kampuni ya Richmond Development Corporation (RDC), kuzalisha umeme wakati wa mgao nchini mwaka jana.

 

Amesema kampuni hiyo ilichukuliwa kwa kigezo cha unafuu wa huduma zake ambazo zingetolewa ilipolinganishwa na kampuni nyingine zilizojitokeza ingawa baadaye serikali iligundua uwezo wake ulikuwa ni mdogo.

 

Rais akizungumza na Watanzania waishio Ubelgiji, jijini Brussels alisema gharama za Richmond katika zabuni ilikuwa ni senti 4.99 za Marekani kwa unit tofauti na kampuni nyingine hatua aliyosema ilifanya Kampuni ya Aggreco kuteremsha gharama zake ili kulingana na Richmond. Alikuwa akijibu swali la Abubakari Hoza aliyemwomba rais afafanue mazingira yaliyofanya serikali kuipa mkataba kampuni hiyo na ikashindwa kuzalisha umeme kama ilivyotarajiwa. Pia alitaka kujua kwa nini Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) liliongeza gharama zake na kuenda kinyume cha kutaka kila Mtanzania kuwa na maisha bora.

 

Katika swali lake hilo, Hoza pia alitaka kupata majibu kwa nini Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ipewe mwekezaji mpya wa kuiongoza wakati hata muda haujapita tangu serikali ionyeshe kutoridhishwa na menejiment ya mwekezaji wa Net Group Solutions ndani ya Tanesco.

 

Katika majibu yake rais alisema pamoja na Richmond kuonyesha uwezo mdogo na kuuzwa kwa Kampuni nyingine ya Dawns, hatua hiyo haijakiuka au kuvunja masharti ya uwekezaji kwa kuwa katika dunia ya utandawazi uuzwaji wa kampuni umekuwa ni kitu cha kawaida.

 

“Katika taratibu za kibepari si tatizo kuuziana kampuni kwani hata kampuni kubwa duniani zinauzwa baada ya kushindwa ndiyo maana kampuni za ndege kama za Sabena na Swiss nazo zilinunuliwa baada ya kuyumba,” alisema.

 

Akizungumzia suala la Net- Group Solutions na mwekezaji mpya ndani ya TTCL, Kampuni ya
Saskatel kutoka Canada, Kikwete alisema tatizo ambalo mashirika ya umma yanakumbwa nalo ni menejimenti mbovu.

 

“Tunazo taasisi ambazo haziendeshwi vizuri, haiwezi kufikia serikali inatoa fedha tu zijiendeshe, fedha ambazo zingetumika kuendeleza shughuli za maendeleo kwa Watanzania.
“Tanesco katika kipindi fulani ilikuwa ni kampuni bora katika nchi zinazoendelea lakini kutokana na matatizo ya menejimenti ilifikia mahali tukasema tujaribu wawekezaji waiendeshe na hilo ndilo linalotokea TTCL,” alisema.

 

Alisema wakati fulani serikali ilitaka kujaribu kuigawanya Tanesco katika idara tatu za uzalishaji, usambazaji na ugavi, hatua ambayo imeshindikana kufikiwa kutokana na ukweli kwamba huwezi kuweka vitengo hivyo vitatu vijitegemee wakati uzalishaji wa umeme ni mdogo ambao hauzidi migawati 500.

 

Hata hivyo serikali imejaribu kupunguza makali kwani Tanesco iliomba kupandisha kwa asilimia 25 kiwango ambacho kingewaumiza Watanzania, alisema.

 

Tanesco imepandisha gharama zake kwa asilimia sita. Akizungumzia uwekezaji ndani ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), Rais alisema Kampuni inayokodishwa ya Rites kutoka India ina uzoefu mkubwa hivyo Watanzania hawatakiwi kuwa na hofu. Rites ni kampuni inayojulikana kwa masuala ya usafiri wa reli duniani na imekwisha kuwekeza Columbia, Cameroon na Msumbiji na inafanya kazi nzuri, alisema na kuomba ipewe nafasi ionyeshe uwezo wake.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents