Bongo5 Makala

Kenya ni STL, Uganda ni Keko, Tanzania nani?

June 3, ilikuwa ni birthday ya Keko rapper wa kike kutoka Uganda. Mvua ya salamu za pongezi kutoka kwa watu wa kila aina ilionesha jinsi gani rapper huyo anakubalika si tu Uganda kwao bali Afrika nzima.

Tukitaja jina lake na kuongeza la Stella Mwangi aka STL wa Kenya kuna swali litakujia.Ni rapper gani wa kike Tanzania kwa sasa ambaye tunaweza kumfananisha na kinadada hao wawili?

Uwezo wa rapper hao wawili umewapeleka mbali kiasi cha kushare stage na wasanii wakubwa duniani achilia mbali nyimbo zao kutamba kwenye vituo vya radio na runinga vya kimataifa.

Keko ambaye jina lake halisi ni Jocelyn Tracy Keko (Keko likimaanisha asubuhi na mapema) msomi wa shahada ya biashara katika chuo kikuu cha Makerere,ni fahari ya Uganda kwakuwa ni msanii pekee wa kike anayeiwakilisha nchi hiyo na kufanikiwa zaidi katika muziki wa Hip hop.

Mwaka jana alijinyakulia tuzo katika Channel O music video awards, na remix ya wimbo This is how we do aliowashirikisha jamaa wa kundi la Goodlyf, Radio na Weasel katika kipengele cha “Most Gifted African East video” na kuwashinda P-Unit’s “kare”, “Kigeugeu” ya Jaguar, AY ft Ms Trinity’s “Good Luck” na “Action” ya Cpwaa.

Tofauti na Keko, Stella Nyambura Mwangi aka STL mzaliwa wa Nairobi, ni nusu mNorway na nusu Kenya lakini anaiwakilisha vyema Kenya. Familia yake ilihamia Norway mwaka 1991 na kukumbana na ubaguzi wa rangi mkali nchini humo.
Kazi zake zimetumika kwenye filamu maarufu kama American Pie Presents: The Naked Mile na Save the Last Dance 2 pia kwenye TV-series kama CSI: NY na Scrubs.

Ana tuzo kibao ikiwemo ya Kisima Awards, Clops Awards na Jeermaan Awards. Ni mwanamuziki maarufu sana nchini Norway baada ya kushinda shindano la Melodi Grand Prix 2011.

Mwaka jana aliiwakilisha Norway kwenye shindano la Eurovision kwa kuimba wimbo wake Haba na Haba.

Wasifu wa rappers hao wa kike inatupa mzigo wa swali! Kwanini Tanzania hatuna rapper wa kike anayekaribia mafanikio kama hayo?

Kuna wakati tulikuwa na Female MC’s wakali wakiwemo Rah P, Sista P, Dataz, Zay B na wengine lakini ukiuliza walipo na wanafanya nini utapata jibu litakalokukatisha tamaa. Wameacha!

Ni kama vile rap ya kike imekufa kabisa Tanzania. Hatujamsahau Chiku Keto ambaye walau amejaribu na anaendelea kupiga mzigo wa Hp Hop lakini, bado..
Hatutaki kuamini kama hakuna akinadada wenye uwezo wa kufanya hip hop na kuiwakilisha Tanzania kama wanavyofanya Keko na STL kwa Uganda na Kenya.

Rap ya kike ina utamu na raha yake. Tunakosa mambo mengi kwa kutokuwa na mc wa kike anayefanya hip hop ‘kike’ na sio ‘kiume.’

Wanachokosea baadhi ya wasichana wanaojaribu kufanya Hip hop ni kutaka kuonesha muonekano wa kigumu uliotawaliwa na mambo ya kiume. Rapper wa kike atafanikiwa zaidi kama ataendelea kuwa na swagga za kike tena kama akiwa mrembo.

Watazame akina Nicki Minaj, Lora Monroe, Iggy Azalia na wengine wanaowakilisha kizazi cha sasa cha hip hop Marekani. Rap yao imekaa kike na hivyo kuifanya kuwa na ladha nzuri na tofauti kwenye masikio ya kila jinsia.

Mashabiki wa hip hop nchini wanamiss sauti za kike kwenye playlist ya vituo vya radio. Kwakuwa si kweli kwamba hakuna wasichana wenye uwezo huo, jambo la kwanza linalotakiwa kufanywa ni kuondoa ile imani kuwa msichana akifanya rap ataonekana malaya.

Inawezekana Tanzania kuwa na rappers wa kike wakali kama STL na Keko watakaofanikiwa kibiashara pia.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents