Burudani

Kilio cha Ray C chazusha mjadala kama kweli Methadone ni tiba inayomfaa!

Rehema Chalamila aka Ray C aliyesifika kwa sauti tamu ya kuimba na kiuno chake bila mfupa, bado anakabiliwa na vikwazo vingi katika vita yake ya kurejea kwenye hali yake ya kawaida baada ya kuwa mwathirika wa madawa ya kulevya.

11190293_825676127480615_692565520_n

Kwa wengi ukiangalia na mahala alipokuwa amefika kabla ya kuanza kupewa tiba, Ray C alipata ‘second chance’ ya kuyarejesha maisha yake kama zamani. Baada ya kuzunguka kwenye hospitali kibao na vituo kadhaa vya rehab hapa nchini, hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete aliamua kumsaidia.

Baada ya muda, Ray C akaanza kurejea kwenye hali yake. Alianza kupata matibabu ya dawa maarufu ya Methadone, inayowasaidia watumiaji wa madawa ya kulevya kuachana na uraibu na kurejea katika hali ya kawaida.

Baada ya kutumia dawa hiyo, Ray C alianza kurejea kwenye afya yake ya zamani japo alinenepa sana. Kwa wengi tuliamini kuwa muimbaji huyo amepona na tayari kurejea kwenye muziki. Ni kweli aliingia studio na kurekodi nyimbo kadhaa na kutoa mmoja uitwao ‘Mshum Mshum’ ambao hata hivyo haujafanya vyema – pengine mashabiki walishindwa kumpata yule Ray C waliyekuwa wamemzoea!

Lakini ikiwa imepita takriban miaka miwili tangu Ray C aanze kutumia Methadone na huku wote tukiamini kuwa huenda akawa amepona kabisa, muimbaji huyo amekuja kutushtua kwa video zake zinazomuonesha akilia kwa uchungu baada ya kunyimwa dawa hizo kwenye hospitali anayotibiwa.

Video hizo ameziweka kwenye akaunti yake ya Instagram.

https://www.youtube.com/watch?v=iJoIPUvZTuo

Ray C anasema kwenye video hizo kuwa kitendo cha yeye kukosa dawa hizo, hugeuka kuwa adhabu kubwa anayoshindwa kuistahimili.

“Nashindwa kuvumilia,” anasikika Ray C akisema. “Mpaka sasa nipo hapa kitengo cha madawa na sijapewa dawa, kwa sababu nilipost ile post nyingine wamenifanyia makusudi. Sasa mimi nikikosa madawa wanataka nirudi kwenye kuvuta unga,” amehoji muimbaji huyo.

Video hiyo imewahuzunisha wengi na pengine kuwashtua zaidi kuwa pamoja na miaka miwili kupita bado muimbaji huyo anaitegemea dawa hiyo. Na hivyo ni muhimu kuhoji iwapo Methadone ni tiba sahihi kwake!

Ni ngumu sana kujua ni maumivu gani anayopitia, lakini nahisi dawa hiyo ilipaswa iwe imemsaidia kiasi cha kumrejesha kwenye hali yake ya kawaida na kutotogemea dawa aina yoyote ile na aishi kama watu wengine. Bila Methadone aliyoitumia kwa miaka miwili sasa, Ray C anaishi maisha magumu yenye maumivu makali.

Kuna njia nyingine mbadala ya kumsaidia? Je! Ataendelea kutumia Methadone katika maisha yake yote? Dawa hiyo ina madhara gani kwenye afya yake hasa akiitumia kwa muda mrefu? Hayo ni baadhi ya maswali ambayo wengi wanajiuliza.

Lakini Methadone kwa mujibu wa Ray C, ni dawa anayoiheshimu sana.

“Namshukuru Mungu kwamba chozi langu limesikika na jioni hii nimepewa dawa,” aliandika Ray C kwenye video nyingine aliyoiweka kwenye akaunti yake ambayo anaonekana akinywa dawa hiyo.
“Naiheshimu hii dawa kuliko kitu kingine chochote katika dunia hii,” ameongeza.

“Dawa hii imeniokoa kutoka kule nilikotoka,dawa hii imenifanya nirudi katika hali yangu ya kawaida. Nitafanya lolote niwezalo kuipata dawa hii kwani ndio mwokozi wangu. Bila dawa hii leo nisingekuwa hapa nilipo! Dawa hii ni haki yangu. Namuomba Mungu anilindie hii dawa kila ninapoiweka mdomoni isinidhuru. Nawashukuru wote kwa sapoti na upendo mlionionyesha leo.”

Kauli yake inaonesha wazi kuwa ataendelea kuitegemea Methadone kwa muda mrefu. Vipi kama akiendelea kuitegemea katika maisha yake yote?
Dawa hiyo si maji. Ukinywa hali kama ya kizunguzungu, usingizi, kichefuchefu, kutapika au kuvuja jasho kwa wingi humtokea mtumiaji. Hali hizi Ray C hukabiliana nazo kila anywapo dawa hii.

Japo si rahisi kama wengi wanavyodhani, ushauri umetolewa kwa muimbaji huyo kujaribu kutumia njia zingine badala ya kutumia dawa hiyo kwa kipindi kirefu.

“Mbona ni yale yale tu, hiyo dawa inakufanya unakuwa mtumwa u can do shit without it…tofauti ni kwamba it has a positive outcome but ur still a slave to drugs. I will be more happy if u stood on ur own,” ameandika director_fiddz.

Naye Dida Mumu ameshauri: Achana na methadone njoo Kigamboni kwa Pilly Misana kuna suluhisho la kudumu vingine mateso hayatakuisha, pls pls ww mwenyewe uliwahi kuja ukajionea jinsi vijana wanavyopambana kuacha na wanafanikiwa wengi tunao mtaani tunawaona hizo methadone zinakudanganya coz zina side effect kubwa pale unapozikosa.Jaribu kuwa muelewa na baadaye usije kurudia kuvuta unga kwa kisingizio cha kukosa hizo dawa wakati suluhisho la kudumu lipo.”
Je anaweza kuacha kutumia dawa hiyo na kuvumilia maumivu hayo kama nicshawz anavyoshauri: Fanya kukubali maumivu, ndokana na methodone, achana na hii dawa pia. Siku ukikosa kabisa utavuta unga @rayc1982 try to live bila hii dawa, am telling u dis koz kuna mtu namfahamu aliweza kuacha kabisa kwa kuvimilia maumiv then nau hatumii kabisa drugs.”

Lakini Amour Mabrouk ana ushahidi kuwa Methadone haina madhara.

“Hizo methadone zinatumika kwa kipindi fulani hadi mtu anapokuwa mbali na hatari ya kutumia madawa,” ameandika. “Msimislead watu waache professional clinic waende mitaani, hiyo ni dose na ina mwisho.Tafadhali ni jambo lililothibitishwa kitaalamu na haina hizo side effects mnazosema, nimeshuhudia ikimponya mama yangu mdogo.”

Blessing Annettee naye ana mawazo kama hayo.

“Stop misleading her,hiyo dawa imethibitishwa na haina side effect na anatumia kwa muda kipimo kikipungua hadi atakapoweza kuishi bila dawa kabisa. Msiwadanganye watu waache clinic maana hawataweza kuhandle arosto watarudi kwenye dawa,methadone ndo suluhisho let them use it,kama hujui kitu dont mislead wengine.”

Swali ni kama Methadone haina madhara na kwamba inaweza kutumika kwa muda na mgonjwa akaweza kurudi kwenye hali yake ya kawaida, ni muda upi huo mtu huyu ataendelea kuitegemea?

Orega ameyahoji maelezo ya Blessing Annettee na Amour Mabrouk,” tuambieni hii dosage ya methadone inachukuwa muda gani? Ili mtu awe huru (methadone-free) we need to be real here. This is neither joke nor a game of chasing a wild goose. Maelfu ya watu wanaumia huko mitaani. Ikiwezekana mtuhabarishe kwanini nchi nyingi zimeipiga marufuku hii Methadone?”

Mange Kimambi naye anashauri kuwa ni muda wa Ray C kuachana na dawa hiyo. “Ray C bado ni mtumwa wa madawa ya kulevya. She has to be strong sasa aachane na hii methadone,” ameandika.

“Ukiona mtu mzima analia hivi ndo ujue hiyo methadone na yenyewe ni majanga. Na serikali inajua ila ni mambo ya budget. Nimesoma sehemu kuwa inaicost serikali ya UK pound 3,000 kumtibia teja kwa kutumia methadone na inawacost more than pound 10,000 kuwatibia kwa kuweka rehab. So wanaona bora wawape tu hiyo dawa wa save pesa. Kwa nchi maskini kama Tanzania ndo kabisaaaaaa. Hakuna pesa waanze kujenga marehab centre etc si bora wawatulize na hiyo methadone.”

Ni kweli kumekuwepo na mijadala mingi kuhusiana na kama methadone ni dawa sahihi kwa watu wenye uraibu wa madawa ya kulevya. Katika baadhi ya nchi kwa mfano Urusi, methadone ilipigwa marufuku.

Ray C ni mmoja tu ya watu wengi wanaokumbana na mateso haya. Ni muhimu kuwepo mjadala wa kuangalia namna gani nyingine inaweza kuwasaidia waathirika wa madawa ya kulevya kuachana kabisa na kuishi maisha ya kawaida bila kutegemea dawa nyingine. Pia vita dhidi ya madawa ya kulevya inapaswa kuongezewa nguvu zaidi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents