Siasa

Lipumba amvaa JK

SAKATA la kashfa ya ufisadi inayoihusu kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, limechukua sura mpya baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kumhusisha Rais Jakaya Kikwete, kwamba naye anapaswa kuwajibika kwa hasara iliyotokana na kashfa hiyo

na Kulwa Karedia

SAKATA la kashfa ya ufisadi inayoihusu kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, limechukua sura mpya baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kumhusisha Rais Jakaya Kikwete, kwamba naye anapaswa kuwajibika kwa hasara iliyotokana na kashfa hiyo.

Chama hicho kimemhusisha Rais Kikwete katika kashfa hiyo kwa madai kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambalo liliidhinisha uamuzi wa Wizara ya Nishati na Madini kuipa kandarasi Richmond.

Kauli hiyo nzito, ilitolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, wakati akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Taifa la chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam.

“Rais Kikwete anastahili kuwajibika kutokana na kashfa ya Richmond kwa vile yeye ndiye alikuwa mhusika mkuu wa kutoa maamuzi kwenye Baraza la Mawaziri…tunataka kuona akichukua hatua za kuwajibika,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa hakustahili kuwajibika peke yake kutokana na ukweli kuwa hakuchukua uamuzi pekee bila kupata ruhusa kutoka kwa mkubwa wake, yaani Rais Kikwete.

“Tunakubali wote kwamba haya yametokea, lakini si Lowassa pekee aliyetakiwa kuwajibika hapa, Rais Kikwete anahusika kwa namna moja au nyingine kwa vile ndiye kiongozi wa mwisho kutoa uamuzi,” alisisitiza Profesa Lipumba.

Akihitimisha mjadala wa hotuba ya wizara yake, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema hatma ya waliohusika kwenye ufisadi wa Richmond iko tayari baada ya kamati aliyoiunda kuwasilisha mapendekezo yake, ambayo yatakabidhiwa kwa wabunge wakati wowote kuanzia sasa.

Mbali ya kumshutumu Rais Kikwete, Profesa Lipumba alisema chama chake kimejipanga vya kutosha ili kuhakikisha kuwa mwaka 2010 kinaingia Ikulu na kuua mtandao wa ufisadi unaoonekana kuota mizizi nchini kila uchao.

“Baada ya kushuhudia taifa likiwa katika mtikisiko mkubwa wa kashfa ya ufisadi, CUF tunasema mwisho wa mtandao wa mafisadi ni mwaka 2010, tusipoangalia nchi inaweza kusambaratika… lazima tuuondoe utawala huu,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesababisha hali ya uongozi wa kitaifa kuwa shakani kutokana na kuendeleza vitendo vya kulinda tuhuma mbalimbali zinazowakabili baadhi ya viongozi wake.

“Kielelezo tosha ni pale CCM ilipoamua kukutana kijijini Butiama, Musoma kwa ajili ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu, huku wakijua wazi wamejaa madhambi…tunashangaa kuona walishindwa kufikia malengo waliyokusudia mojawapo ikiwa la kuundwa kwa serikali ya mseto Zanzibar,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema hatua ya CCM kugoma kuunda serikali ya mseto kisiwani Zanzibar, imetokana na hatua ya kupuuzwa kwa ushauri wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere alioutoa mwaka 1995.

“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliishauri CCM kuwa, ili kumaliza mgogoro wa Zanzibar, lazima iundwe serikali ya mseto, lakini wenzetu wameamua kukataa katakata, tena aliyepinga hadharani ushauri huu ni rais wa wakati huo, Dk. Salmin Amour,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali ya Zanzibar chini ya Rais Aman Abeid Karume, imevunja katiba yake na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumzia kashfa ya wizi wa sh bilioni 133 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), Profesa Lipumba alisema ili kurejesha imani kwa wananchi, serikali inapaswa kutaja majina ya wahusika na hatua za kisheria dhidi yao zichukuliwe haraka.

“Suala hili bado limeonekana kuwa zito, sasa tunasema tunataka kuona majina ya wahusika wote yanatajwa ili kurejesha imani kwa wananchi,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema katika madeni hayo, serikali ilihusika kuwapatia fedha baadhi ya watu waliodaiwa kuwa wafanyabiashara kutoka nchini Yugoslavia kinyume cha sheria.

Pia alidai kuwa fedha hizo zilitumiwa na CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kwa kutengeneza kofia, fulana, mabango na vipeperushi na kuvisambaza nchi nzima.

Kuhusu aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, Profesa Lipumba alisema hivi sasa alistahili kuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi wakati suala lake likiendelea kufanyiwa uchunguzi.

“Tunashangaa kuona Chenge yuko mitaani…huyu alitakiwa kuwa chini ya ulinzi wa polisi akiwasaidia katika maswala mbalimbali yanayohusu matatizo yake, na inaonyesha wazi kabisa kwamba hakumuonyesha rais fomu zake za kumiliki mali,” alisema Profesa Lipumba.

Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisema chama chake kinaunga mkono hatua ya kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai kujitoa katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

“CUF tunalaani kwa kauli moja mambo yote yanayofanywa na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, tunataka serikali ya umoja wa kitaifa ambayo haitamshirikisha Mugabe kamwe… tunaendelea kumuunga mkono Tsvangirai,” alisema Profesa Lipumba.

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents