Siasa

Mafisadi BoT hayakamatiki

TIMU ya Rais kuchunguza watuhumiwa wa ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu Tanzania (BoT), imekiri kuwa kazi ya kuyakamata mafisadi ni ngumu kwani hadi sasa imefanikiwa kuyajua makampuni yaliyohusika tu.

Na Ramadhan Semtawa

 

 

 

TIMU ya Rais kuchunguza watuhumiwa wa ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu Tanzania (BoT), imekiri kuwa kazi ya kuyakamata mafisadi ni ngumu kwani hadi sasa imefanikiwa kuyajua makampuni yaliyohusika tu.

 

 

 

Badala yake, timu hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika imejitetea kwamba, hadi sasa uchunguzi wao umebaini wahusika wakuu ni makampuni ambayo ni tofauti na watu. Wajumbe wengine wa timu hiyo ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema.

 

 

 

Hata hivyo, kauli hiyo mpya ya Mwanyika imeshindwa kujibu hoja ya msingi ya wanaharakati ambayo imezingatia kauli ya Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkullo, ambaye alisema serikali imeshapokea Sh50 bilioni za EPA lakini akasita kutaja majina ya watuhumiwa.

 

 

 

“Kumekuwa na malalamiko ya kutokamatwa kwa waliohusika.

 

“Tunapenda kuueleza umma kwamba, uchunguzi wetu hadi hivi sasa unaonyesha kwamba wahusika wakuu ni makampuni. Kisheria, makampuni hayo ni mtu yaani Legal Person,” alisema Mwanyika na kuongeza: “Hata hivyo, makampuni hayo ni tofauti na mtu wa kawaida. Kampuni katika maana hii, inajitegemea yenyewe. Kwa msingi huo, ikiwa kampuni imefanya kosa, kuna utaratibu wa kisheria wa kufuata. Kazi inayofanyika hivi sasa, ni uchunguzi wa kina kuhusu maafisa wa makampuni hayo ili kufahamu ni kitu gani kilichosababisha hali hiyo kutokea.”

 

 

 

Mwanyika alisema uchunguzi huo unaendelea na ndiyo utakaowezesha kujua hatua za kisheria zitakazochukuliwa, alisisitiza katika taarifa yake ya pili ya jana jioni baada ya kikao cha dharura kuhusu mchakato huo.

 

 

 

Katika taarifa yake ya awali aliyotoa asubuhi, alitetea usiri wa mchakato huo na kutaka wananchi wavute subira akisema ulilenga kulinda taratibu za uchunguzi zisivurugike.

 

 

 

Tofauti na hoja iliyotolewa na wadau mbalimbali wakiwamo wanaharakati, timu hiyo katika taarifa zake mbili imeshindwa kujibu hoja ya vipi watuhumiwa hawakamatwi.

 

 

 

Kukamatwa watuhumiwa hao na kufikishwa katika vyombo vya sheria ni moja ya agizo la Rais Jakaya Kikwete, ambalo alilitoa kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo mapema Januari, mwaka huu, wakati akitangaza matokeo ya ufisadi wa fedha za umma zaidi ya Sh133 bilioni katika EPA.

 

 

 

Hata hivyo, kinyume na agizo hilo na sheria za nchi, watuhumiwa hao katika makampuni 22 yaliyochota fedha hizo, wamekuwa wakizirejesha na kuachiwa huru huku mchakato mzima ukitawaliwa na usiri.

 

 

 

Wakati joto hilo la mchakato huo likiwa juu, Mwanyika , katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, alisema kwa sasa timu hiyo imejikita katika kufanya uchunguzi wa kina na kitaalamu.

 

 

 

Mwanyika katika taarifa hiyo ambayo amelazimika kutumia msemo wa Wahenga katika kutetea usiri huo, alitaka umma wakiwamo waandishi wa habari, wawe wenye subira na kwamba kamati inatoa taarifa ambazo hazitaathiri uchunguzi.

 

 

 

” Timu inapenda kuufahamisha umma kuwa pamoja na majukumu mengi iliyopewa, kwa sasa imejikita katika kufanya uchunguzi wa kitaalamu na wa kina,” alisema Mwanyika na kuongeza:

 

 

 

” Kwa msingi huo, pamoja na fedha zinazorudishwa, ni vema umma na wanahabari wakafahamu kuwa, kazi ya uchunguzi haijafikia mwisho na kwa sasa timu inaona ni vema kutotoa taarifa ambazo zitaathiri kazi ya uchunguzi inayoendelea, tunapenda kuusihi umma na wanahabari kuwa na subira wakati kazi hii inaendelea,” alisema.

 

 

 

Hata hivyo alifafanua kuwa, timu yake imekuwa ikipata ushirikiano mzuri kutoka kwa kampuni na wamiliki wanaohusika na upotevu wa fedha hizo za EPA.

 

 

 

Mwanyika aliongeza kuwa, timu hiyo imepewa miezi sita kufanya kazi, kisha kuwasilisha ripoti kwa Rais Kikwete.

 

 

 

“Vile vile tunapenda kuukumbusha umma na wanahabari kuwa timu imepewa miezi sita kufanya kazi na hatimaye kuwasilisha ripoti kwa Rais,” alisema na kuongeza:

 

 

 

” Huu ni mwezi wa pili tangu timu ianze kazi yake, kwa msingi huo, timu inawasihi umma na wanahabari kuwa na subira.”

 

 

 

“Wahenga walisema Subira yavuta Heri, tunawahakikishia kuwa kazi inaendelea vizuri na heri yaja kwani tulichonacho hadi sasa katika uchunguzi si haba.”

 

 

 

Mjadala kuhusu mchakato wa uchunguzi kuhusu ufisadi wa EPA, uliibuka zaidi wiki moja iliyopita baada ya Mwanyika na Mkullo, kutoa taarifa ambazo zilionyesha kuwachefua Watanzania.

 

 

 

Kwa nyakati tofauti, Mwanyika na Mkullo walitoa taarifa za kurejeshwa Sh50 bilioni zilizochotwa EPA, lakini watuhumiwa wakaachiwa huru na kukataa kuwataja majina yao na kampuni zao.

 

 

 

Hali hiyo, imeibua mjadala kutoka kwa wanaharakati ambao wameanza kupaza sauti, wakihoji serikali kutowakamata watuhumiwa hao.

 

 

 

Miongoni mwa wanaharakati ambao wameinyoshea kidole tume hiyo, ni kutoka Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC).

 

 

 

Tamko hilo la LHRC limekifananisha kitendo cha Serikali kutaja kiwango cha fedha zinazorudishwa katika EPA, bila kuwataja waliohusika kuwa ni kuwatukana Watanzania na kuwafanya wajinga.

 

 

 

Pia Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrsaia na Mandeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa, amehoji uhalali wa serikali kuwapa muda watuhumiwa kurejesha fedha hizo.

 

 

 

Serikali ilipaswa kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa hao, kwa mujibu wa kifungu cha 265 cha Sheria ya kanuni ya adhabu Sura ya 16, ambacho kinaeleza mtu anayechukua kitu kwa njia ya wizi anatenda kosa la jinai.

 

 

 

Sheria hiyo kifungu cha 20, kinasema mtu aliyefanya udanganyifu na kuweza kuondoa imani kwa umma, anakuwa anatenda kosa la jinai.

 

 

 

Kwa mantiki hiyo, pamoja na kurudisha pesa hizo watuhumiwa hao, wanatakiwa kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

 

 

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents