Siasa

Majambazi ‘wamwambia’ JK kuwa bado wanatesa

ZAIDI ya watu watano wanaodaiwa kuwa majambazi, baadhi yao wakiwa na sare za askari wa Polisi Usalama Barabarani, wameteka magari ya mizigo na kupora kiasi kikubwa cha fedha.

Na Glory Mhiliwa, Arusha

 

ZAIDI ya watu watano wanaodaiwa kuwa majambazi, baadhi yao wakiwa na sare za askari wa Polisi Usalama Barabarani, wameteka magari ya mizigo na kupora kiasi kikubwa cha fedha.

 

Tukio hilo lilitokea juzi saa tatu usiku katika eneo la Makuyuni ambapo majambazi hayo waliweka vizuizi barabarani kana kwamba ni askari wa usalama barabarani wanaoangalia usalama barabarani.

 

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Bw. Evarist Mangala, akizingumza kwa njia ya simu, alikiri kutokea kwa tukio hilo, ambapo alisema kwa sasa Jeshi lake linaendesha msako mkali dhidi ya kukamata majambazi hao.

 

Alisema magari hayo ya mizigo ambayo yalitekwa ni matano yaliyokuwa yamebeba kiasi kikubwa cha mizigo iliyokuwa inasafirishwa ambayo ni namba T 523 AJK aina ya Toyota, T 688 ALC Land Rover Defender, T 591 AJN Nissan Patrol na malori mawili namba T 521 AMG na T 800 AJF.

 

Alieleza kwamba majambazi hao waliteka magari hayo kutokana na mengi ya mizigo kusafiri usiku, ili kuondokana na adha ya msongamano wa magari barabarani.

 

Alisema kiasi cha fedha zilizoibwa na baadhi ya vitu kwenye magari hayo ya mizigo hakijafamika, ingawa alisema ni kikubwa.

 

Aliongeza kuwa mbinu walizotumia kuteka magari ni sawa na zinazotumiwa na askari wa usalama kuweka vizuizi barabarani ili kuangalia mienendo ya magari na usalama.

 

Kamanda Mangala alisema majambazi hao walikuwa wamevalia nguo nyeupe zenye vizibao vinavyong’aa ambavyo hutumiwa na watu wengi hata wasiokuwa askari, ingawa walioshuhuduia walidai kuwa walikuwa na sare za Polisi.

 

Hata hivyo, ingawa Jeshi la Polisi mkoani hapa lilikataa kutoa ufafanuzi wa madai ya majambazi hao kuwa na silaha walipokuwa wanateka magari hayo, lakini baadhi ya vyanzo vya habari vilikiri majambazi hao kutumia silaha.

 

Utekaji wa magari hayo umetokea wakati Rais Jakaya Kikwete akiendelea na ziara yake mkoani hapa kukagua miradi ya maendeleo ya wananchi.

 

Wakati huo huo, watalii watano na kiongozi wao wapo kwenye hali mbaya baada ya kuvamiwa na kushambuliwa na genge la majambazi wenye silaha.

 

Tukio hilo lilitokea jana saa tano asubuhi eneo la Tengeru karibu na hoteli ya kitalii ya Mountain Village, ambapo watalii hao walikuwa wakitembea kwa miguu kutoka hotelini hapo kwenda mji mdogo wa Tengeru umbali wa kilometa mbili.

 

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Bw. Ervarist Mangala, alikiri kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema majambazi hao walikuwa wawili na silaha.

 

Aliendelea kusema kuwa watalii hao ambao wanne ni raia wa Marekani na mmoja wa Uingereza wapo kwenye hali mbaya baada ya kupigwa risasi kadhaa.

 

Aidha, alisema kiongozi wa watalii hao ambaye ni Mtanzania wa kampuni ya utalii ya Green Foot Print Adventure, Bw. Charles Safari (28) alijeruhiwa kwenye paji la uso.

 

Hata hivyo watalii hao ambao wawili walifahamika kuwa ni Wamarekani Jacquie Lutz (36) na Raymond Mollica (39) na wenzao, hali zao ni mbaya sana.

 

Kamanda Mangala alisema kutokana na hali hiyo, watalii hao walikimbizwa hospitalini Nairobi Kenya huku kiongozi wao akiwahishwa kwenye hospitali ya rufaa ya KCMC, Kilimanjaro.

 

Baada ya Rais Kikwete aliyeko ziarani mkoani hapa kupata taarifa za tukio hilo, alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Bw. Basilio Matei, kusitisha ziara na kuwasaka majambazi hayo.

 

Agizo hilo alilitoa akiwa wilayani Ngorongoro ambako alitaka kupewa taarifa za kukamatwa kwa majambazi hao haraka iwezekanavyo.

 

“Nataka kusikia kwamba watuhumiwa wamekamatwa ili kurudisha hali ya usalama na amani Arusha ambapo ndio kwenye kitovu cha hifadhi za kitalii,” aliagiza Rais Kikwete.

 

Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kiongozi wa Watalii hao alifariki dunia hospitalini KCMC.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents