Bongo5 Makala

Makala: Professor Jay, Sugu wapo ‘bize’ sana

Muziki wa Bongo Fleva unazidi kubadilika na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo na mapinduzi yanazidi kufanyika katika muziki huu.

Mabadiliko katika sekta/tasnia yoyote hayawezi kuepukika, endapo utajitenga na hilo kupata mafanikio ni vigumu, kwani mafanikio huambatana na mabadiliko.

Tumeshuhudia mabadiliko na mapinduzi makubwa katika Bongo Fleva, wanamuziki wameweza kuvunja kuta na mipaka katika mambo makubwa ambayo miaka 10 nyuma ilikuwa ni vigumu kubashiri hilo. Weka nuka hapo.

Kwanini Professor Jay na Sugu

Joseph Haule ‘Professor Jay’ na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, haya ni majina mawili ambavyo yamechukua nafasi kubwa katika kitabu cha kumbukumbu ya Bongo Flava. Kwa sasa wote ni Wabunge kitu ambacho kinawatofautisha na wasanii wengine na kuwapa sifa ya ziada.

Kwa mara ya kwanza mwaka 2010 Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alipata nafasi ya kuingia bungeni kupitia kura za wananchi wa Mbeya Mjini, pia mwaka 2015 akatetea tena nafasi yake. Wakati Sugu anafanikiwa kutetea nafasi yake, Joseph Haule ‘Professor Jay’ anaipa tena heshima Bongo Flava kupitia wananchi wa Mikumi ambao walimchagua awe Mbunge wao.

Kutokana na kupewa nafasi hizo za uongozi imekuwa ni nadra sana kuwasikia vilivyo kwenye Bongo Flava kama ilivyokuwa mwanzo.

Karibu Mr Blue, Sholo Mwamba na Azma

Hawa ni wasani watatu tofauti kabisa, Mr Blue na Azma wakifanya muziki wa rap, huku Sholo Mwamba akiibuka hivi karibuni kupita muziki wa singeli.

Kama kumbukumbu zangu zipo sawa, tangu kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hawa watatu ndio wasanii pekee waliopata nafasi ya kufanya kolabo na hawa wabunge.

Sugu ametoa wimbo uitwao Freedom uliofanyika MJ Records chini ya prodyuza Daxo Chali, mwanzoni kulikuwa na madai kuwa wimbo huu ulikuwa wa Mr Blue, kitu kilichokuja kuleta mgogoro hasa pale video ya wimbo huo ulipotoka halafu hayupo (Mr Blue) kitu kilichomfanya kulalamika kuwa ameporwa wimbo wake.

Hata hivyo hayo yote walikuja kuzungumzwa na yakaisha na maisha mengine yakaendelea.

Tangu hapo Sugu hajatoa tena ngoma nyingine zaidi ya kushirikishwa na Azma katika ngoma ya Garagasha. Kolabo hii ilikutanisha wasanii wanne ambao ni Azma, Sugu, Izzo Bizness na Abela (The Amazing).

Azma alieleza Bongo5 kuwa lengo la kufanya ngoma hiyo ni kuwakutanisha wasanii kutoka mkoani Mbeya.

Tuje kwa Professor Jay, baada ya kupata ubunge watu wengi walikuwa na shahuku ya kujua kama ataendelea kufanya aina yake muziki kwa kuachia nyimbo kama Ndio Mzee, kikao cha Zarura, Nang’atuka n.k.

Kinyume na matarajio ya weingi Prof Jay akaja na muziki wa singeli. Licha ya kuwepo wasanii wengi wanaofanya vizuri kwenye singeli, ila jicho lake lilidondoka kwa Sholo Mwamba.

Ndipo wakatoa wimbo uitwao Kazi Kazi, Professor Jay mwenyewe akiita hip hop singeli, hata hivyo wapo waliokubali na wapo ambao hawakuridhika.

Watu wengi walieleza hisia zao, huku wengine wakisema Professor Jay ameusaliti muziki wa hip hop uliompatia umaarufu mkubwa. Twende pole pole.

Rapper Roma alisema aina zote za muziki zimeshafanyika kinachotakiwa ni msanii aje na ubunifu mpya ili kuwateka mashabiki, kwa hiyo muunganiko kati ya singeli na hiop hip ni kutambulisha kitu kipya.

Roma aliongeza kuwa hata ukichukua akapela ya wimbo huu (kazi kazi) ukaivisha kwenye mdundo wa wimbo wa Zali la Menteli bado itakuwa vile vile, yaani rap.

Pia Fid Q alisema iwe itakavyokuwa ila mwisho wa siku muziki unabakia kuwa ni sanaa, na sanaa haina mwisho, mtu anaruhusiwa kufanya ambavyo anaona ni sahihi kwake.

“Inatengemea na yeye alivyoona ni sahihi, na alichofanya yeye (Professor Jay) ni rap, lakini anasalia kuwa mwana hip hop,” alisema Fid Q.

Pia mwaka huu Professor Jay ametoa wimbo uitwao Kibabe chini ya prodyuza Mr T Touch. Katika ngoma hii anaelezea namna anavyoitumia nafasi aliyopewa na wananchi, harakati zake kutoka mwanzo hadi kufikia mafanikio hayo, marafiki aliowaongeza kupitia siasa, muziki wake n.k.

Kweli wapo ‘bize’

Wakati muda huu tukishuhudia utitiri wa ngoma mpya katika Bongo Flava ambazo wasanii wamekuwa wakizitoa kila siku, kwa Prpfessor Jay na Sugu hali ni tofauti kidogo.

Kama nilivyoeleza hapo awali tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wote wawili wamekuwa si wakutoa ngoma kila mara au kuwasikia katika kolabo. Tangu kipindi hicho wote wawili wamesikika katika ngoma mbili tu. Hapo kwa tafsiri yangu wapo ‘bize’ katika kutumikia wananchi wao.

By Peter Akaro

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents