Bongo5 Makala

Makala: Rayvanny itanichukua muda kukuelewa

Nimefungua kitabu na kukutana na maneno ya Zig Ziglar yasemayo, ‘mafanikio ni kiwango cha juu kabisa cha uwezo ulionao”. Mwandishi huyo wa vitabu na mhamasishaji anataka kutuaminisha kuwa mtu kufanikiwa katika kiwango cha kawaida au cha juu kabisa hapo ndipo kilele cha uwezo alionao.

Maneno ya Zig Zilah yanaishi katika maisha ya msanii wa Bongo Flava kutoka label ya WCB, Rayvanny aliyeshinda tuzo ya BET 2017 katika kipengele cha International Viewers Choice na kuwa msanii wa kwanza kutoka Tanzania kushinda tuzo hiyo, pongezi za kutosha kwake.

Uzito wa jina lake umeongezeka maradufu tangu aliposhuka kwenye ndege katika uwanja wa kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere akiwa ameshikilia mkononi tuzo yake ya BET. Binafsi nimejiuliza mbona mapema sana na kuniacha katika mshangao wa mambo haya manne ambayo yatanichukua muda kuja kumuelewa Rayvanny.

  1. Ushindi bila kolabo na msanii mkubwa wa nje

Wakati Diamond Platnumz anachuguliwa kwa mara ya kwanza kuwania BET mwaka 2014 katika kipengele cha Best International Act Africa, alikuwa anafanya vizuri na ngoma yake ‘My Number’. Ukubwa wa ngoma hiyo ulitokana na kolabo aliyofanya na Davido ikiwa ni remix.

Hata alipochaguliwa kuwania tuzo hizo kubwa duniani kwa mara ya pili mwaka 2016 katika kipengele hicho hicho, bado haikuwezesha mikono ya Diamond Platnumz kuchukua tuzo ya BET pamoja na ukubwa wa kolabo nyingine aliyofanya na Mr Flavour ‘Nana’.

Kwa Rayvanny mambo ni tofauti, ni tofauti tena sana, hatujamsikia katika ngoma na msanii mkubwa wa nje. Mwaka huu ndio nimemsikia katika kolabo na msanii kutoka Kenya, Bahati ambaye amemshirikisha Rayvanny katika wimbo wake ‘Nikumbushe’. Nachelewa kuamini uzito wa kolabo hii kama una ushawishi wowote katika ushindi wa Rayvanny BET ingawa naheshimu kazi hiyo.

Rayvanny na ngoma zake zisizozidi tano (official release), yaani Kwetu, Natafuta Kiki na Zezeta lakini ameweza kutusua.

Naweza kusema muda umekuwa rafiki kwake kwani ametoka rasmi kimuziki mwaka jana na kuweza kutambulika na sasa anafikia mafanikio hayo makubwa zaidi, muda haujamtupa mkono. Muda amemkatili vikali Diamond lakini umetenda haki katika jitihada zake.

Ndiyo umetenda haki kwake. Uwekezaji alioufanya katika label yake ya WCB ndio inamfuta machozi na machungu ya kuudhuria BET mara mbili na kurudi mikono mitupu. Ushindi wa Rayvanny ni ushindi wa Diamond na Watanzania wote.

Najaribu kuwaza iwapo Rayvanny angeshinda tuzo hii akiwa nje ya WCB na hana ushirikiano wa Diamond. Napata picha kuwa zile team za mitandao zingeongezeka, leo hii tungekuwa na team Rayvanny pamoja na team Diamond.

Kwa nini team?,. team kwa sababu Diamond ndiye aliyekuwa msanii wa mwisho kutoka Tanzania kuwania BET kabla ya Rayvanny, hivyo watu wangetaka kuwashindanisha lakini hilo halipo kutokana Rayvanny anasimamiwa na Diamond.

Hapo ndipo tunaona faida ya kuwashika wengine mikono katika kufikia ndoto zao. Hili linanikumbusha maneno ya mwandishi Og Mandino  yasemayo, “Wakati wote fanya kilicho bora na kile ulichopanga kwa sasa, baadae utakuja kuvuna”.

  1. Muziki bila kiki

Kama muziki bila kiki lingekuwa somo katika Bongo Fleva na mimi nikawa mwalimu, bila shaka katika somo hili Rayvanny ningempa alama  A au B+ ya kumfanya kutobweteka.

Nimekuwa nikivutiwa zaidi na life style yake, sikumbuki siku niliyosoma jina lake katika magazeti ya udaka lakini kila siku watu wanaruka majoka kama sio madebe kupitia ngoma zake. Kwake muziki mzuri unaongea hahitaji kiki au aina fulani za video kudhihirisha ukali wake, tuachane na hilo lakini ebu tazama hili.

Video zake nyingi zimekuwa zikifanyika hapa nchini na sio nje. Video yake ‘Kwetu’ iliyotoka April 14 mwaka jana ilifanyika hapa Bongo ikiongozwa na Godfather, video yake ya pili ‘Natafuta Kiki’ pia ilifanyika Bongo chini ya Kwetu Studio.

Nyimbo hizi mbili ndizo zimempa Ray umaarufu mkubwa na uwezo wake kujulikana lakini hakukwea pipa hadi Afrika Kusini kutafuta kichupa kikali kama wasanii wengi wanavyoamini kufanya hivyo ni njia ya kutusua kimataifa.

Jambo hili la pili linamuongezea alama katika mada husika ya mwanzo, pia linaongeza muda kwangu wa kutomuelewa.

  1. Kutoka rap hadi kuimba

Mwanzoni Rayvanny alikuwa akifanya muziki wa rap kabla ya kuanza kuimba, wakati huo alijulikana kama Raymond. Alikuwa akitafuta namna ya kutusua kupitia muziki huo huku akiamini siku moja atafanikiwa na muziki utaendesha maisha yake.

Pengine alikuwa akiwatazama wasanii kama Quick Rocka, Sugu na Izzo Bizness kutoka Mbeya wakifanya vizuri ikawa ni sababu ya yeye kuamini kuwa atafikia alipo kwa sasa. Katikati ya imani hiyo ghafla anabadili upendo na kuwa msanii wa kuimba, hiki ni kitu kinachohitaji ufundi na umakini wa hali ya juu vinginevyo unajipoteza.

Wakati wote ni rahisi kuyapima mafanikio, ila ni mbali kutoka mwanzo hadi kuyafikia. Mwaka 2011 Rayvanny aliibuka mshindi katika mashindano ya Free Style pale Coco Beach, pia tumesikia alivyofanya vizuri pindi aliporudia wimbo wa Sugu, hii inaonyesha ingawa kwa sasa ameamua kuimba ila bado uwezo wa kurap upo pale pale.

Ni wasanii wachache sana wanaotoka kwenye rap na kuamua kisha kufanya vizuri, lakini yeye ameweza kuimba, na kuimba huko kumemletea mafanikio makubwa tena makubwa zaidi. Acha niendelee kukushangaa, itanichukua muda kukuelewa.

  1. Kiwango cha uvumilivu

Moja ya nukuu kutoka kwa Bob Brown ni ile isemayo, “kila aliyefanikiwa nyuma yake kuna miaka mingi ya kutokufanikiwa,”. Hii ina maana kuwa mafanikio ni mchakato unaohitaji uvulivu ili kufika pale unapotaka vinginevyo huwezi kufanikisha lolote katika ulimwengu huu ulioumbwa kwa misingi ya changomoto lukuki.

Sanaa kwa ujumla ni jambo ambalo linahitaji uvumilivu ili kufanikiwa kwa sababu sanaa ni yale mawazo yako unayoyatoa, hivyo mapokeo ya watu ndio kufanikiwa kwako.

Kuwashawishi watu hadi kuamini kile ambacho unakitoa katika fikra zako si jambo jepesi hata kidogo,  ndio maana idadi kubwa ya wasanii wengi waliofanikiwa zaidi duniani maisha yao yamejaa simulizi zenye maumivu makali.

Rayvanny tangu mwaka 2011 amekuwa akipigania kile anachokiamini katika vilinge mbali mbali Dar es Salaam lakini mwaka 2016 ndio tunakuja kumsikia rasmi, miaka ya hapo katikati ilikuwa ya mapambano.

Hakutaka sanaa yake iishie katika historia kama ya Vincent Willem van Gogh, huyu alikuwa mchoraji raia wa Uholanzi ambaye alifariki mwaka 1890 kwa kujipiga risasi baada ya kusubiri kwa kipindi kirefu bila kuona faida ya kazi zake za uchoraji.

Moja ya picha alizochora Vincent van Gogh kipindi cha uhai wake

Vincent Willem van Gogh ana historia ya kuwa mtu maarufu baada ya kufariki, miaka miwili baada ya kifo chake kazi zake za uchoraji ziliuzwa mamilioni ya dola na kushinda tuzo mbali mbali.

Kukosa uvulimvu ndiko kulimkosesha kufaida matunda ya kazi ya mikono yake. Inaelezwa aliacha picha 864 na vichoro zaidi ya 1,000 ambazo alichora miaka 10 ya mwisho ya uhai wake lakini leo wanafaidi watu wengine.

Nimpongeze Rayvanny kwa kulikataa hilo katika maisha yake ya sanaa, naamini anajivunia uvumilivu wake uliomletea tuzo ya BET kabla hata ya kushinda tuzo yoyote hapa Bongo.

Hapo ndipo nashindwa kukuelewa Rayvanny, huna tuzo kutoka nyumbani, Afrika Mashariki, Afrika ila unayo ya dunia, nikupongeze kwa hilo kwani umekuwa mwanaume kabla ya mvulana.

By Peter Akaro

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents