Siasa

Mfungwa aliyesamehewa akuta nyumba imeuzwa

Mmoja wa wafungwa walioachiwa kwa msamaha wa Rais Jakaya Kikwete katika sikukuu ya Uhuru, Bw. James Barnabas (42), hana mahali pa kuishi baada ya kukuta nyumba yake imeuzwa.

Na Bigambo Jeje, PST, Serengeti



Mmoja wa wafungwa walioachiwa kwa msamaha wa Rais Jakaya Kikwete katika sikukuu ya Uhuru, Bw. James Barnabas (42), hana mahali pa kuishi baada ya kukuta nyumba yake imeuzwa.


Alikuwa akitumikia kifungo cha miaka mitano baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia.


Bw. Barnabas alihukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa Oktoba 10 mwaka 2004 baada ya kupatikana na hatia ya kuua, hali iliyomfanya akate rufaa mahakama ya rufaa kanda ya Mwanza ambapo hukumu hiyo ilitenguliwa na kuwa ya kuua bila kukusudia.


Mfungwa huyo tayari alishatumikia robo tatu ya kifungo chake hadi msamaha ulipomkuta.


Aliwaambia waandishi wa habari mjini Mugumu kuwa alikuta nyumba yake iliyokuwa kiwanja namba 12 kitalu EHD imeuzwa na ndugu zake kwa kile walichodai kuwa ni kupata fedha kwa ajili ya kumwekea wakili wa kumtetea katika rufaa yake hiyo iliyosikilizwa mwaka jana.


Alisema sababu hiyo aliyopewa na ndugu zake si sahihi kwa kuwa hakuwahi kuona wakili wala pesa tangu mwaka 1997 alipokamatwa na kuwekwa mahabusu hadi alipokuwa anaachiwa kwa msamaha wa Rais mwezi huu.


Alisema kufuatia hali hiyo, familia yake ya watoto nane na wake wawili ililazimika kutawanyika kila mmoja na watoto wake jambo lililosababisha watoto kukosa huduma muhimu ikiwemo Elimu.


Alisema alikuta watoto wake hawajapelekwa shule kutokana na hatua ya wake zake kutangatanga wakitafuta pa kuishi.


Mnunuzi wa nyumba hiyo, Bi. Lilian Nyakangara ambaye ni katibu muhtasi ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Serengeti, alikiri kununua nyumba hiyo kutoka kwa waliojitambulisha kuwa ni familia ya mfungwa huyo na kwamba taratibu zote za kisheria zilifuatwa.


Bw. Barnabas alisema amefikisha suala hilo mbele ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishina wa Magereza Tanzania Ofisa Ardhi Wilaya akiomba asaidiwe kupata nyumba na mali zake ingawa mpaka sasa hajajibiwa.


Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano Jakaya Kikwete kwa kutoa msamaha na kuomba msamaha uende hadi kwa wafungwa waliokaa muda mrefu gerezani tangu mwaka 1997.


Bw. Barnabas alikamatwa mwaka 1997 kutokana na tuhuma ya kumchoma kisu Bw. Sese wakiwa baa kufuatia ugomvi baina yao na katika hukumu ya mwaka 2004.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents