Siasa

Mtikila amuonya Makamu wa Rais

MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amepinga hatua iliyofikiwa kati ya Tanzania na nchi za Iran na Misri ya kutaka kufufua tume za ushirikiano.

na Mobini Sarya


MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amepinga hatua iliyofikiwa kati ya Tanzania na nchi za Iran na Misri ya kutaka kufufua tume za ushirikiano.


Makubaliano hayo yalifikiwa hivi karibuni wakati wa ziara ya Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, alipozitembelea nchi hizo na kukubaliana kuimarisha ushirikiano wa pamoja.


Pia, Mchungaji Mtikila ameitaka serikali kutijihusisha na suala la kutafuta uanachama wa Jumuiya ya Kiislamu (OIC), kwani kufanya hivyo ni kinyume cha katiba ya nchi.


Hoja hiyo ya Mchungaji Mtikila inafuatia kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyoitoa hivi karibuni akiwajibu wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kuwa suala la Zanzibar kujiunga na OIC sasa linazungumzika.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mchungaji Mtikila alisema kuwa hatua ya kuanzisha ushirikiano baina ya Tanzania na Iran na Misri, anaipinga kwa nguvu zote, kwani inaonekana ni ajenda ya siri inafanywa ili kuiingiza nchi katika Umoja wa Nchi za Kiislamu.


Katika maelezo yake, Mtikila alimshangaa Dk. Shein kwa kuunga mkono mpango wa kuwa na ushirikiano wa karibu na Iran ambayo inashutumiwa hivi sasa kutokana na hatua yake ya kurutubisha madini yanayoweza kutumika kutengeneza silaha za nyukilia.


“Tunachunguza taarifa za Dk. Ali Shein kupita akiwaelekeza Waislamu wa misikiti kadhaa wachore na kuwasilisha ramani za misikiti yao ili wajengewe kwa msaada kutoka Iran,” alisema.


Wakati akiishutumu Iran kwa kujihusisha na silaha za nyukilia, Mchungaji Mtikila alisema hana imani na Misri, akiituhumu kuwa ni moja ya nchi ambazo ni kitovu cha ugaidi.


“Tunamuonya Dk. Shein… Misri na Iran wanazozipigia debe ni za malengo yale yale ya OIC, kwa hiyo ni hatari kwa taifa letu kama Wakristo na wapenda haki na amani duniani,” alisema.


Alisema kuwa mpango huo wa Dk. Shein unafanana na wa Kanali Muhammar Gaddafi na anaoutumia akiwa na malengo ya jihad ya kuwasilimisha Waafrika wote kupitia mpango wake wa African Islamic Organisation (AIO), ikiwa Afrika itaungana na kumpa uongozi jambo ambalo limeshitukiwa na Wakristo.


Katika hatua nyingine, Mtikila ameonya juhudi zinazofanywa kinyemela ili kuona Tanzania inaingizwa katika OIC, hoja ambayo iliibuliwa wiki iliyopita na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.


Mchungaji Mtikila alisema kuwa, hatua ya Membe kusema kuwa suala la Tanzania kuingia OIC linazungumzika, ni kinyume cha katiba, ambayo Membe aliapa kuilinda akiwa ameshikilia Biblia na kuwataka wale wenye mawazo kama yake kuacha mara moja.


Alisema kuwa Tanzania haiwezi kujiunga na OIC kwa sababu huo ni Umoja wa Nchi za Kiislamu na Tanzania si nchi ya Kiislamu.


Pia, aliwataka Wazanzibari kutozungumzia suala la nchi yao kujiunga na OIC wakiwa ndani ya Muungano, na kusema kuwa iwapo wanataka kujiunga na jumuiya hiyo, ni vema wajiondoe kwanza katika Muungano.


“Tunamuonya Waziri Membe kwamba suala la OIC kamwe halizungumziki katika nchi hii, kwa sababu OIC ni Umoja wa Nchi za Kiislamu na Tanzania haiwezi kuwa ya Kiislamu na katiba ya nchi yetu inalinda haki na misingi ya uhuru wa kuabudu,” alisema.


Pia alionya kuwa ikiwa akina Waziri Membe wataendelea na juhudi zao za kuiingiza nchi katika umoja huo, Rais Jakaya Kikwete atapoteza uongozi wake, na Membe hatakuwa tena waziri.


Mchungaji Mtikila amesema hayo ikiwa ni siku chache baada ya hoja hiyo kuibuka Zanzibar ambako akijibu hoja hizo, Waziri Membe alisema suala la Zanzibar kuruhusiwa kujiunga na OIC, bado linazungumzika na linahitaji mjadala kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.


“Si kama Serikali ya Muungano haipendelei Zanzibar ijiunge na jumuiya hiyo, lakini bado kunahitajika baadhi ya mambo ya msingi yakaangaliwa kati ya pande zote mbili, ili utekelezaji wake usiathiri katiba ya nchi,” alisema Waziri Membe.


Alisema kwamba wakati suala hilo lilipoibuka lilionekana linagusa masuala ya dini, lakini tayari limekuwa likitekelezwa na nchi za Afrika, ikiwemo Uganda na Msumbiji ambazo ni wanachama katika jumuiya hiyo.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents